Alif Lam Ra. (A.L.R.) Hichi ni Kitabu tulicho kiteremsha kwako ili uwatowe watu
kwenye giza uwapeleke kwenye muwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe
kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifiwa,
Wale wanao fadhilisha maisha ya dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia watu
wasifuate Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wamepotelea mbali.
Na hatukumtuma Mtume ila kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi
Mwenyezi Mungu humuacha akapotea amtakaye, na akamwongoa amtakaye. Naye ni
Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Na tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe watu wako kwenye
giza uwapeleke kwenye mwangaza. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika
katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri akashukuru.
Na Musa alipo waambia watu wake: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu aliyo
kujaalieni, pale alipo kuokoeni kutokana na watu wa Firauni walio kupeni adhabu
mbaya kabisa, wakiwachinja wenenu wanaume, na wakiwawacha hai wanawake. Na
katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unao toka kwa Mola wenu Mlezi.
Je! Hazikukufikieni khabari za walio kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na
Thamud, na walio baada yao, ambao hapana awajuaye ila Mwenyezi Mungu? Mitume wao
waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa
vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakataa hayo mliyo tumwa, na hakika sisi tuna
shaka kubwa na mnayo tuitia.
Mitume wao wakasema: Ati pana shaka na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi?
Yeye anakuiteni apate kukufutieni madhambi yenu, na akupeni muhula mpaka muda
ulio wekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni wanaadamu kama sisi. Mnataka
kutuzuilia na waliyo kuwa wakiabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja ilio wazi.
Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote ila ni wanaadamu kama nyinyi.
Lakini Mwenyezi Mungu humfanyia hisani amtakaye katika waja wake. Wala sisi
hatuwezi kuleta uthibitisho ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi
Mungu ndio wategemee Waumini.
Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa kwenye
Njia zetu. Na hapana shaka sisi tutayavumilia hayo maudhi mnayo tuudhi. Na juu
ya Mwenyezi Mungu wategemee wanao tegemea.
Na walio kufuru wakawaambia Mitume wao: Tutakutoeni katika nchi yetu, au mrudi
katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwaletea wahyi: Hakika tutawaangamiza
walio dhulumu!
Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yawe yanamjia kutoka kila
upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine kali vile vile.
Mfano wa walio mkufuru Mola wao Mlezi - vitendo vyao ni kama jivu linalo
peperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya mdharba. Hawawezi kupata chochote
katika waliyo yafanya. Huko ndiko kupotelea mbali!
Na wote watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia walio
takabari: Sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika
adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angeli tuongoa basi
hapana shaka nasi tungeli kuongoeni. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri;
hatuna pa kukimbilia.
Na Shet'ani atasema itapo katwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu alikuahidini ahadi
ya kweli. Nami nalikuahidini; lakini sikukutimizieni. Na sikuwa na mamlaka juu
yenu, isipo kuwa nilikuiteni, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali
jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamwezi kuwa
watetezi wangu. Hakika mimi nilikataa tangu zamani kunishirikisha na Mwenyezi
Mungu. Hakika madhaalimu watakuwa na adhabu chungu.
Na walio amini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani yapitayo mito kati
yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkio yao humo yatakuwa:
Salaam!
Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya
dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha kupotea hao wenye kudhulumu.
Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
Waambie waja wangu walio amini, washike Sala, na watoe katika tulivyo waruzuku,
kwa siri na dhaahiri, kabla haijafika Siku isiyo kuwa na biashara wala urafiki.
Mwenyezi Mungu ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi, na akateremsha maji kutoka
mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na akafanya
yakutumikieni majahazi yanayo pita baharini kwa amri yake, na akaifanya mito
ikutumikieni.
Na akakupeni kila mlicho muomba. Na mkihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamwezi
kuzidhibiti. Hakika mwanaadamu ni dhaalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema.
Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza watu wengi. Basi aliye nifuata
mimi huyo ni wangu, na aliye niasi, hakika Wewe ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu.
Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde
lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola wetu Mlezi, ili
washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda,
ili wapata kushukuru.
Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayo yaficha na tunayo yatangaza. Na
hapana kitu kinacho fichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika
mbingu.
Na waonye watu siku itapo wajia adhabu, na walio dhulumu waseme: Ewe Mola wetu
Mlezi! Tuakhirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate Mitume. Kwani
nyinyi si mliapa zamani kwamba hamtaondokewa?