Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha Furqani (Upambanuo). Hakika
walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu kali. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa.
Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye
maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama
wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna,
na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na
wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka
kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili.
- Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio kuwa kabla yao. Walikanusha
Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa madhambi yao; na Mwenyezi Mungu
ni Mkali wa kuadhibu.
Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi mawili yalipo pambana. Jeshi
moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jingine kafiri likiwaona zaidi
kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono
amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye macho.
Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu
na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya
duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema.
Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wachamngu ziko Bustani kwa Mola
wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na wake walio takaswa, na wanazo
radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake,
Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana
mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye
nguvu na Mwenye hikima.
Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu
hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa
baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu
ni Mwepesi wa kuhisabu.
Na pindi wakikuhoji, basi sema: Mimi nimeusalimisha uso wangu kumwelekea
Mwenyezi Mungu, na kadhaalika walio nifuata. Na waambie walio pewa Kitabu na
wasio na kisomo: Je! Mmesilimu? Wakisilimu basi wameongoka. Na wakikengeuka basi
juu yako ni kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake.
Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaitwa kukiendea Kitabu cha Mwenyezi
Mungu ili kiwahukumu baina yao; kisha baadhi yao wanageuka wanakikataa.
Hayo ni kwa sababu walisema: Hautatugusa Moto isipo kuwa kwa siku chache tu. Na
yakawadanganya katika dini yao yale ambayo wenyewe waliyo kuwa wakiyazua.
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu uliye miliki ufalme wote! Wewe humpa ufalme umtakaye,
na humwondolea ufalme umtakaye, na humtukuza umtakaye, na humuangusha umtakaye.
Kheri yote iko mikononi mwako. Hakika Wewe ni Muweza wa kila kitu.
Wewe huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku. Na humtoa
hai kutokana na maiti, na humtoa maiti kutokana na aliye hai. Na unamruzuku
umtakaye bila ya hisabu.
Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala ya Waumini. Na anaye fanya
hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Ila ikiwa kwa ajili ya
kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na marejeo ni
kwa Mwenyezi Mungu.
Sema: Mkificha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyafichua Mwenyezi Mungu anayajua; na
anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa
kila kitu.
Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyo yafanya yamehudhurishwa, na pia ubaya
ilio ufanya. Itapenda nafsi lau kungekuwako masafa marefu baina ya ubaya huo na
yeye. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa
waja wake.
Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu
atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta
madhambi na Mwenye kurehemu.
Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni
mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye
kujua.
Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke - na Mwenyezi Mungu
anajua sana aliye mzaa - Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na mimi nimemwita
Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na Shet'ani aliye
laaniwa.
Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na
akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya alipo ingia chumbani kwake
alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi? Naye
akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye
bila ya hisabu.
Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika kamnadia: Hakika Mwenyezi Mungu
anakubashiria Yahya, ataye kuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi
Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa watu wema.
Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata mwana na hali ukongwe
umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu
hufanya apendavyo.
Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema: Alama yako ni kuwa hutasema
na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu. Na mdhukuru Mola Mlezi wako
kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi.
Hizi ni khabari za ghaibu tunazo kufunulia; nawe hukuwa nao walipo kuwa wakitupa
kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa nao walipo kuwa wakishindana.
Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria
(mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu,
mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa
Mwenyezi Mungu).
Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa
Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha
nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa
tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na
ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika
haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini.
Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni
baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi
wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.
Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa
Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu.
Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu.
Pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nitakunyanyua
kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na nitawaweka wale walio kufuata
juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa
kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa mkikhitalifiana.
Watakao kuhoji katika haya baada ya kukufikilia ilimu hii waambie: Njooni
tuwaite watoto wetu na watoto wenu, na wake zetu na wake zenu, na sisi wenyewe
na nyinyi wenyewe, kisha tuombe kwa unyenyekevu tutake laana ya Mwenyezi Mungu
iwashukie waongo.
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi:
Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na
chochote; wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi
Mungu. Na wakigeuka basi semeni: Shuhudi- eni ya kwamba sisi ni Waislamu.
Na kikundi katika Watu wa Kitabu walisema: Yaaminini yale waliyo teremshiwa
wenye kuamini mwanzo wa mchana, na yakataeni mwisho wake; huenda wakarejea.
Wala msimuamini ila anaye fuata dini yenu. Sema: Hakika uwongofu ni uwongofu wa
Mwenyezi Mungu, kuwa apewe mtu mfano wa mlio pewa nyinyi au wakuhojini mbele ya
Mola wenu Mlezi. Sema: Hakika fadhila zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa
amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mjuzi.
Na miongoni mwa Watu wa Kitabu yupo ambaye ukimpa amana ya mrundi wa mali
atakurudishia, na miongoni mwao yupo ambaye ukimpa amana ya dinari moja
hakurudishii isipo kuwa ukimsimamia kumdai. Haya ni kwa kuwa wakisema: Hatuna
lawama kwa ajili ya hawa wasio jua kusoma. Na wanamzulia uwongo Mwenyezi Mungu,
hali nao wanajua.
Hakika wanao uza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao thamani ndogo, hao
hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema
nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu
chungu.
Na wapo baadhi yao wanao pindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa
hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa
Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wanamsingizia Mwenyezi
Mungu uwongo na wao wanajua.
Haiwezi kuwa mtu aliye pewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na Unabii kisha
awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu. Bali
atawaambia: Kuweni wenye kumuabudu Mola Mlezi wa viumbe vyote, kwa kuwa nyinyi
mnafundisha Kitabu na kwa kuwa mnakisoma.