Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na
akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume
na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana, na
jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.
Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnao wapenda
katika wanawake, wawili au watatu au wane. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya
uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya
hivi ndiko kutapelekea msikithirishe wana.
Wala msiwape wasio na akili mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia yawe ni
kiamu yenu. Walisheni katika hayo na muwavike, na mseme nao maneno mazuri.
Na wajaribuni mayatima mpaka wafike umri wa kuoa. Mkiwaona ni wekevu, basi
wapeni mali yao. Wala msiyale kwa fujo na pupa kwa kuwa watakuja kuwa watu
wazima. Na aliye kuwa tajiri naajizuilie, na aliye fakiri basi naale kwa kadri
ya ada. Na mtakapo wapa mali yao washuhudizieni. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa
Mhasibu.
Wanaume wana sehemu katika wanayo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Na
wanawake wanayo sehemu katika waliyo yaacha wazazi na jamaa walio karibia. Ikiwa
kidogo au kingi. Hizi ni sehemu zilizo faridhiwa.
Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeli acha nyuma yao watoto wanyonge
wangeli wakhofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme maneno yaliyo sawa.
Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu
la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi
mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu
lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho
kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio
warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi
mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni.
Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi
kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
Na fungu lenu ni nusu walicho acha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Wakiwa na mtoto
basi fungu lenu ni robo ya walicho acha, baada ya wasia waliyo usia au kulipa
deni. Na wake zenu watapata robo mlicho kiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna
mtoto basi sehemu yao ni thumni ya mlicho kiacha, baada ya wasia mlio usia au
kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anaye rithiwa hana mtoto wala
wazazi, lakini anaye ndugu mume au ndugu mke, basi kila mmoja katika hawa
atapata sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo basi watashirikiana katika
thuluthi, baada ya wasia ulio usiwa au kulipa deni, pasio kuleta dhara. Huu ndio
wasia ulio toka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.
Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko
kufuzu kukubwa.
Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake,
(Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha.
Na ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wane
katika nyinyi. Watakapo shuhudia, basi wazuieni majumbani mpaka wafishwe na
mauti au Mwenyezi Mungu awatolee njia nyengine.
Na wawili kati yenu wafanyao hayo waadhibuni. Na wakitubia wakatengenea basi
waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Hakika toba inayo kubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa
ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia toba
yao, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na ni Mwenye hikima.
Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha
hapo akasema: Hakika mimi sasa nimetubia. Wala wale wanao kufa na hali wao ni
makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.
Enyi mlio amini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala
msiwadhikishe ili mwapokonye baadhi ya mlivyo wapa - isipo kuwa wakifanya uchafu
ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia
kitu, na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake.
Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa chungu ya
mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhulma na kosa
lilio wazi?
Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na
khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio
kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu
wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia.
Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa
watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipo
kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye
kurehemu.
NA WANAWAKE wenye waume, isipo kuwa walio milikiwa na mikono yenu ya kulia.
Ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na mmehalilishiwa wasio kuwa hao,
mtafute kwa mali yenu kwa kuowa pasina kuzini. Kama mnavyo starehe nao, basi
wapeni mahari yao kwa kuwa ni waajibu. Wala hapana lawama juu yenu kwa mtakacho
kubaliana baada ya kutimiza waajibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua na
Mwenye hikima.
Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana Waumini, na
aoe katika vijakazi Waumini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia. Na Mwenyezi
Mungu ni Mjuzi wa imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni
kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kama ada, wawe wanawake wema, si
makahaba wala si mahawara. Na wanapo olewa kisha wakafanya uchafu basi adhabu
yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyo wekewa waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni
mwenu anaye ogopa kuingia katika zina. Na mkisubiri ndio bora kwenu. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
Mwenyezi Mungu anataka kukubainishieni na kukuongozeni nyendo za walio kuwa
kabla yenu, na akurejezeni kwenye ut'iifu wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi,
Mwenye hikima.
Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe biashara kwa
kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni.
Wala msitamani alicho wafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko wengine.
Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake wana fungu katika walio
vichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi
wa kila kitu.
Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyo yaacha wazazi wawili na jamaa. Na
mlio fungamana nao ahadi wapeni fungu lao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa
kila kitu.
Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhi yao
juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo yatoa. Basi wanawake wema ni wale wenye
kut'ii na wanao jilinda hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha
wajilinde. Na ambao mnachelea kutoka katika ut'iifu wanasihini, muwahame katika
malazi na wapigeni. Wakikut'iini msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure. Hakika
Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na Mkuu.
Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi
kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka
mapatano Mwenyezi Mungu atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye
khabari.
Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema
wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa
mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya
kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri,
Na ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu, wala hawamuamini Mwenyezi Mungu wala
Siku ya Mwisho; na yule ambaye Shet'ani amekuwa ndiye rafiki yake, basi ana
rafiki mbaya mno.
Na ingeli wadhuru nini wao lau wangeli muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho,
na wakatoa katika aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwajua vyema.
Enyi mlio amini! Msikaribie Sala, hali mmelewa, mpaka myajue mnayo yasema, wala
hali mna janaba - isipo kuwa mmo safarini #NAME? chooni, au mmewagusa wanawake -
na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu na mikono yenu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kughufiria.
Miongoni mwa Mayahudi wamo ambao hubadilisha maneno kuyatoa mahala pake, na
husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya kusikilizwa. Na husema:
"Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao ili kuitukana Dini. Na lau kama wangeli
sema: Tumesikia na tumet'ii, na usikie na "Undhurna" (Utuangalie), ingeli kuwa
ni kheri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru yao;
basi hawaamini ila wachache tu.
Enyi mlio pewa Kitabu! Aminini tuliyo yateremsha yenye kusadikisha yale mliyo
nayo, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni, au tukawalaani kama
tulivyo walaani watu wa Sabato (Jumaamosi). Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima
ifanyike.
Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo
kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi
kubwa.
Jee huwaoni wale wanao dai kuwa ati wametakasika? Bali Mwenyezi Mungu humtakasa
amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kadiri ya kijiuzi kilichomo ndani ya uwazi wa
kokwa ya tende.
Huwaoni wale walio pewa sehemu ya Kitabu? Wanaamini masanamu na Shet'ani! Na
wanawasema walio kufuru, kuwa hao wameongoka zaidi katika njia kuliko Walio
amini.
Hakika wale walio zikataa Ishara zetu tutawaingiza Motoni. Kila zitapo wiva
ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyengine ili waionje hiyo adhabu. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Na wale walio amini na wakatenda mema tutawaingiza katika Pepo zipitazo mito
kati yake kwa kudumu humo milele. Huko watakuwa na wake walio takasika, na
tutawaingiza katika vivuli vizuri kweli.
Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapo
hukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayo kuwaidhini Mwenyezi
Mungu ni mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye madaraka
katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na
Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi
na ndiyo yenye mwisho mwema.
Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa kwako na yaliyo
teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali
wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea mbali.
Basi inakuwaje unapo wasibu msiba kwa sababu ya yale iliyo tanguliza mikono yao?
Hapo tena hukujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hatukutaka ila wema na
mapatano.
Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Basi
waachilie mbali, uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri na kuingia katika
nafsi zao.
Na hatukumtuma Mtume yeyote ila at'iiwe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na lau
pale walipo jidhulumu nafsi zao wangeli kujia, wakamwomba Mwenyezi Mungu
msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka wangeli mkuta Mwenyezi Mungu
ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi
katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya
hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa.
Na lau kuwa tumewaamrisha: Jiueni, au tokeni majumbani kwenu, wasingeli fanya
hayo ila wachache tu miongoni mwao. Na lau kama wangeli fanya walio waidhiwa
ingeli kuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi.
Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wa pamoja na wale alio waneemesha
Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema.
Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!
Na ikikufikieni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema - kama kwamba hapakuwa
mapenzi baina yenu naye: Laiti ningeli kuwa pamoja nao nikafanikiwa mafanikio
makubwa.
Basi nawapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanao uza uhai wa dunia
kwa Akhera. Na anaye pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kisha akauliwa au
akashinda basi tutakuja mpa ujira mkubwa.
Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa,
wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji
huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako,
na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako.
Walio amini wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na walio kufuru wanapiana
katika njia ya upotofu. Basi piganeni na marafiki wa Shet'ani. Hakika hila za
Shet'ani ni dhaifu.
Je, huwaoni wale walio ambiwa: Izuieni mikono yenu, na mshike Sala na mtoe Zaka.
Na walipo amrishwa kupigana, mara kundi moja kati yao liliwaogopa watu kama
kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa khofu kubwa zaidi. Na wakasema: Mola Mlezi
wetu! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti unge tuakhirishia kiasi ya muda
kidogo hivi! Sema: Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye
kuchamngu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa ya tende.