Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi, na akafanya
giza na mwangaza. Tena baada ya haya walio kufuru wanawafanya wengine sawa na
Mola wao Mlezi.
Jee, hawaoni vizazi vingapi tulivyo viangamiza kabla yao? Tuliwaweka katika nchi
tusivyo kuwekeni nyinyi; tukawapelekea mvua nyingi na tukaifanya mito inapita
chini yao. Mwishoe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao
kizazi kingine.
Na wao husema: Mbona hakuteremshiwa Malaika? Na kama tungeli teremsha Malaika,
basi bila ya shaka ingesha hukumiwa amri, tena hapo wasingeli pewa muhula.
Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi
Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya
Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe hawaamini.
Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba
mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa
niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina.
Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo
ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila
kitu.
Sema: Kitu gani ushahidi wake mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye
shahidi baina yangu na nyinyi. Na nimefunuliwa Qur'ani hii ili kwayo nikuonyeni
nyinyi na kila inayo mfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na
Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika
Yeye ni Mungu mmoja tu, nami ni mbali na mnao washirikisha.
Na wapo miongoni mwao wanao kusikiliza; na tumezitia pazia nyoyo zao wasije
kuyafahamu. Na upo uziwi masikioni mwao, na wakiona kila Ishara hawaiamini. Hata
wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema walio kufuru: Hizi si chochote ila
hadithi za watu wa kale.
Na unge ona watakapo simamishwa kwenye Moto, wakawa wanasema: Laiti tungeli
rudishwa, wala hatutakanusha tena Ishara za Mola wetu Mlezi, na tutakuwa
miongoni wa Waumini.
Bali yamewadhihirikia waliyo kuwa wakiyaficha zamani. Na kama wangeli rudishwa
bila ya shaka wange yarejea yale yale waliyo katazwa. Na hakika hao ni waongo.
Na lau ungeli ona watavyo simamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, akawaambia: Je, si
kweli haya? Na wao watasema: Kwani? Tunaapa kwa Mola Mlezi wetu ni kweli. Yeye
atasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile mlivyo kuwa mnakataa.
Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, mpaka ilipo wajia
Saa kwa ghafla, wakasema: Ole wetu kwa tuliyo yapuuza! Nao watabeba mizigo yao
juu ya migongo yao. Ni maovu hayo wanayo yabeba.
Na hakika walikanushwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa, na
kuudhiwa, mpaka ilipo wafikia nusura yetu. Na hapana wa kubadilisha maneno ya
Mwenyezi Mungu. Na bila ya shaka zimekujia baadhi ya khabari za Mitume hao.
Na ikiwa ni makubwa kwako huku kukataa kwao, basi kama unaweza kutafuta njia ya
chini kwa chini ya ardhi, au ngazi kwendea mbinguni ili uwaletee Ishara -- Na
lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa angeli wakusanya kwenye uwongofu. Basi usiwe
miongoni mwa wasio jua.
Na wamesema: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema:
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuteremsha muujiza. Lakini wengi wao hawajui.
Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka kwa mbawa zake mbili, ila
ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao
Mlezi watakusanywa.
Na walio kanusha Ishara zetu ni viziwi na mabubu waliomo gizani. Mwenyezi Mungu
humwachia kupotea amtakaye, na humweka katika Njia iliyo nyooka amtakaye.
Basi walipo sahau walio kumbushwa tuliwafungulia milango ya kila kitu. Mpaka
walipo furahia yale waliyo pewa tuliwashika kwa ghafla, na mara wakawa wenye
kukata tamaa.
Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu akanyakua kusikia kwenu, na kuona kwenu, na
akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani asiye kuwa Mwenyezi Mungu ataye kuleteeni
hayo tena? Angalia vipi tunavyo zieleza Ishara, kisha wao wanapuuza.
Sema: Mimi sikwambiini kuwa ninazo khazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo
yaliyo fichikana. Wala sikwambiini kuwa mimi ni Malaika. Mimi sifuati ila yanayo
funuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa, kipofu na mwenye kuona. Basi
hamfikiri?
Wala usiwafukuze wanao mwomba Mola Mlezi wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi
yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata
kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye kudhulumu.
Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili waseme: Ni hao ndio Mwenyezi
Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanao
shukuru?
Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! Amani iwe
juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye fanya uovu
miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika
Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu Mlezi, nanyi
mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi
Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu kuliko wote.
Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua
kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje
katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho
bainisha.
Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho fanya mchana. Kisha Yeye
hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe. Kisha kwake Yeye ndiyo
marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya.
Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake. Na hukupelekeeni
waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha, nao hawafanyi
taksiri.
Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa
unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa
miongoni mwa wanao shukuru.
Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya
miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na kuwaonjesha baadhi yenu jeuri
ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili wapate kufahamu.
Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie
mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi
usikae pamoja na watu madhaalimu.
Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na pumbao, na uhai wa dunia
ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi ikaangamizwa kwa sababu ya iliyo
yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila Mwenyezi Mungu. Na ingatoa kila
fidia haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa kwa sababu ya yale waliyo yachuma.
Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa, na adhabu chungu.
Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae hatufai wala hatudhuru, na
turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi? Tuwe kama ambao mashet'ani
wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki wanao mwita ende kwenye
uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio
Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote,
Naye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na anaposema: Kuwa! Basi huwa.
Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku litapo pulizwa barugumu, Mjuzi
wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye Mwenye hikima na Mwenye
khabari.
Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa
kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayo
fanyia ushirikina.