Je! Imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia mmoja wao kuwa: Waonye watu, na
wabashirie wale walio amini ya kuwa watakuwa na cheo cha juu kwa Mola wao Mlezi?
Wakasema makafiri: Hakika huyu ni mchawi dhaahiri!
Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye ameziumba mbingu na ardhi kwa
siku sita, na ametawala kwenye ufalme wake, anaendesha mambo yote. Hapana
mwombezi ila baada ya idhini yake. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi.
Basi muabuduni Yeye. Je! Hamkumbuki?
Kwake Yeye tu ndio marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya
kweli. Hakika Yeye ndiye aliye anzisha uumbaji, na kisha ataurejesha ili awalipe
kwa uadilifu wale walio amini na wakatenda mema. Na walio kufuru, wao watapata
vinywaji vinavyo chemka, na adhabu chungu kwa sababu ya walivyo kuwa wakikufuru.
Yeye ndiye aliye lijaalia jua kuwa na mwangaza, na mwezi ukawa na nuru, na
akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hisabu. Mwenyezi Mungu hakuviumba
hivyo ila kwa Haki. Anazipambanua Ishara kwa watu wanao jua.
Wito wao humo utakuwa: Subhanaka Llahumma "Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu!" Na
maamkio yao humo ni "Salama". Na mwisho wa wito wao ni: Alhamdulillahi Rabbil
A'lamiin "Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote."
Na lau kama Mwenyezi Mungu angeli wafanyia watu haraka kuwaletea shari kama
wanavyo jihimizia kuletewa kheri, bila ya shaka wangelisha timiziwa ajali yao.
Lakini tunawaacha wale wasio tumainia kukutana nasi wakihangaika katika upotovu
wao.
Na mtu akiguswa na shida hutuomba naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama.
Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba hakupata kutuomba
tumwondoshee shida iliyo mpata. Ndio namna hiyo wamepambiwa warukao mipaka yale
waliyo kuwa wakiyatenda.
Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza kaumu za kabla yenu walipo dhulumu, na
waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi; lakini hawakuwa wenye kuamini. Ndio
kama hivyo tunavyo walipa watu wakosefu.
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi, wale wasio taraji kukutana na Sisi
husema: Lete Qur'ani isiyo kuwa hii, au ibadilishe. Sema: Hainifalii mimi
kuibadilisha kwa nitakavyo nafsi yangu. Mimi sifuati ila ninayo funuliwa kwa
Wahyi. Hakika mimi naogopa, nikimuasi Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku iliyo
kuu.
Nao, badala ya Mwenyezi Mungu, wanaabudu wasio wadhuru wala kuwanufaisha, na
wanasema: Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu! Sema: Je! Mnamwambia
Mwenyezi Mungu asiyo yajua ya katika mbingu wala katika ardhi? Subhanahu wa
Taa'la! Ametakasika na ametukuka na hao wanao mshirikisha naye.
Wala watu hawakuwa ila Umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si
neno lililo kwisha tangulia kutokana na Mola wako Mlezi, hapana shaka hukumu
ingeli kwisha katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana.
Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema:
Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu. Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja
nanyi katika wanao ngojea.
Na tunapo waonjesha watu rehema baada ya shida waliyo ipata, utawaona wana
vitimbi kuzipangia Ishara zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa
kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayo yapanga.
Yeye ndiye anaye kuendesheni bara na baharini. Hata mnapo kuwa majahazini na
yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, upepo mkali ukawazukia, na
yakawajia mawimbi kutoka kila upande, na wakaona wamesha zongwa, basi hapo
humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafishia niya: Ukituokoa na haya bila ya shaka
tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
Lakini akisha waokoa, mara wanafanya jeuri tena katika nchi bila ya haki. Enyi
watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Hii ni starehe ya maisha ya dunia tu.
Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyo yateremsha kutoka mbinguni,
kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayo ila watu na wanyama. Mpaka ardhi
ilipo kamilika uzuri wake, na ikapambika, na wenyewe wakadhani wamesha iweza,
iliifikia amri yetu usiku au mchana, tukaifanya kama iliyo fyekwa - kama kwamba
haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua Ishara zetu kwa watu wanao fikiri.
Na wale walio chuma maovu, malipo ya uovu ni mfano wake vile vile, na yatawafika
madhila. Hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu. Nyuso zao kama kwamba
zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio watu wa Motoni, wao humo
watadumu.
Sema: Ni nani anaye kuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Au ni nani anaye
miliki kusikia na kuona? Na nani amtoaye hai kutoka maiti, na akamtoa maiti
kutoka aliye hai? Na nani anaye yadabiri mambo yote? Watasema: Allah, Mwenyezi
Mungu. Basi sema: Je! Hamchi?
Sema: Je! Yupo katika miungu yenu ya ushirikina anaye ongoa kwendea Haki? Sema:
Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi, je, anaye stahiki kufuatwa ni yule
Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiye ongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna
nini? Mnahukumu namna gani?
Na haiwezekani Qur'ani hii kuwa imetungwa na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Lakini
hii inasadikisha yaliyo tangulia, na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka
ndani yake, kutokana na Mola Mlezi wa viumbe vyote.
Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema: Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite
(kukusaidieni) muwawezao, isipo kuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnasema kweli.
Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake.
Kadhaalika walio kabla yao walikanusha vile vile. Basi angalia jinsi ulivyo kuwa
mwisho wa madhaalimu hao.
Na wakikukanusha wewe, sema: Mimi nina a'mali yangu, na nyinyi mna a'mali yenu.
Nyinyi hamna jukumu kwa niyatendayo, wala mimi sina jukumu kwa myatendayo.
Na Siku atakapo wakusanya, itakuwa kama kwamba hawakukaa ila saa moja tu ya
mchana! Watatambuana. Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na Mwenyezi
Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.
Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayo waahidi, au tukakufisha kabla
yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa wanayo yafanya.
Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri ila apendavyo Mwenyezi Mungu.
Kila umma una muda wao walio wekewa. Ukifika muda wao hawakawii hata saa moja
wala hawatangulii.
Na lau kuwa kila nafsi iliyo dhulumu inamiliki kila kiliomo duniani, bila ya
shaka ingeli toa vyote kujikombolea. Na watakapo iona adhabu wataficha majuto.
Na patahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawatadhulumiwa.
Jueni kuwa hakika vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi ni vya Mwenyezi
Mungu. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Lakini wengi wao
hawajui.
Sema: Je! Mwaonaje zile riziki alizo kuteremshieni Mwenyezi Mungu, nanyi
mkafanya katika hizo nyengine haramu na nyengine halali. Sema: Je! Mwenyezi
Mungu amekuruhusuni, au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?
Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur'ani, wala
hamtendi kitendo chochote ila Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnapo shughulika
nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika
ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa ila kimo katika
Kitabu kilicho wazi.
Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote viliomo mbinguni na ardhinii. Na wala
hawawafuati hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ni washirika wake.
Wao hawafuati ila dhana tu, na hawasemi ila uwongo.
Wamesema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu, Aliye takasika! Yeye ni Mkwasi,
Mwenye Kujitosheleza. Vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi ni vyake peke
yake. Nyinyi hamna uthibitisho wowote wa haya! Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo
yajua?
Wasomee khabari za Nuhu alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Ikiwa kukaa
kwangu nanyi na kukumbusha kwangu kwa Ishara za Mwenyezi Mungu kunakutieni
mashaka basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Nanyi tengezeni mambo yenu pamoja
na washirika wenu, na wala mambo yenu yasifichikane kwenu. Kisha nihukumuni,
wala msinipe muhula.
Wakamkanusha. Basi tukamwokoa, pamoja na walio kuwa naye, katika jahazi. Na
tukawafanya wao ndio walio bakia, na tukawazamisha walio zikanusha Ishara zetu.
Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walio onywa.
Kisha baada yake tukawatuma Mitume kwa watu wao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizo
wazi. Lakini hawakuwa wenye kuyaamini waliyo yakanusha kabla yake. Ndio kama
hivyo tunapiga muhuri juu ya nyoyo za warukao mipaka.