Yeye ndiye aliye teremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili wazidi Imani juu
ya Imani yao. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye majeshi ya mbingu na ardhi. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye ujuzi, Mwenye hikima -
Ili awaingize Waumini wanaume na Waumini wanawake katika Bustani zipitazo mito
kati yake, wadumu humo, na awafutie makosa yao. Na huko ndiko kufuzu kukubwa
mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na awape adhabu wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake, na washirikina wanaume
na washirikina wanawake, wanao mdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya. Utawafikia
mgeuko mbaya, na Mwenyezi Mungu awakasirikie, na awalaani, na awaandalie
Jahannamu. Na hayo ni marudio maovu kabisa.
Bila ya shaka wanao fungamana nawe, kwa hakika wanafungamana na Mwenyezi Mungu.
Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Basi avunjaye ahadi hizi anavunja
kwa kuidhuru nafsi yake; na anaye tekeleza aliyo muahadi Mwenyezi Mungu,
Mwenyezi Mungu atamlipa ujira mkubwa.
Watakuambia mabedui walio baki nyuma: Yametushughulisha mali yetu na ahali zetu,
basi tuombee msamaha. Wanasema kwa ndimi zao yasiyo kuwamo katika nyoyo zao.
Sema: Ni nani awezaye kukusaidieni chochote kwa Mwenyezi Mungu akitaka Yeye
kukudhuruni au akitaka kukunufaisheni? Bali Mwenyezi Mungu anazo khabari za
mnayo yatenda.
Lakini mlidhani kwamba Mtume na Waumini hawatarudi kabisa kwa ahali zao, na
mkapambiwa hayo katika nyoyo zenu, na mkadhania dhana mbaya, na mkawa watu wanao
angamia.
Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Humsamehe amtakaye, na
humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Walio baki nyuma watasema: Mtapo kwenda kuchukua ngawira, tuacheni tukufuateni!
Wanataka kuyabadili maneno ya Mwenyezi Mungu. Sema: Hamtatufuata kabisa.
Mwenyezi Mungu alikwisha sema kama hivi zamani. Hapo watasema: Bali nyinyi
mnatuhusudu. Siyo, bali walikuwa hawafahamu ila kidogo.
Waambie walio achwa nyuma katika mabedui: Mtakuja itwa kwenda pigana na watu
wakali kwa vita, mpigane nao au wasalimu amri. Basi mkimt'ii, Mwenyezi Mungu
atakupeni ujira mzuri. Na mkigeuka kama mlivyo geuka kwanza, atakuadhibuni kwa
adhabu iliyo chungu.
Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala mgonjwa hana lawama. Na mwenye
kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani yapitayo mito
kati yake. Na atakaye geuka upande atamuadhibu kwa adhabu chungu.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewapa radhi Waumini walipo fungamana nawe chini ya
mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na
akawalipa kwa Ushindi wa karibu.
Mwenyezi Mungu anakuahidini ngawira nyingi mtakazo zichukua, basi
amekutangulizieni hizi kwanza, na akaizuia mikono ya watu isikufikieni, na ili
hayo yawe ni Ishara kwa Waumini, na akakuongozeni Njia Iliyo Nyooka.
Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono yenu kwao, katika bonde la
Makka baada ya kukupeni Ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona
myatendayo.
Hao ndio walio kufuru na wakakuzuieni msiingie Msikiti Mtakatifu, na
wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao. Na lau si wanaume Waumini na wanawake
Waumini msio wajua mkawasaga na mkaingia makosani kutokana nao bila ya kujua
...Mwenyezi Mungu (amefanya haya) ili amuingize amtakaye katika rehema yake. Lau
wangeli tengana bila ya shaka tungeli waadhibu walio kufuru kwa adhabu chungu.
Pale walio kufuru walipo tia katika nyoyo zao hasira, hasira za kijinga,
Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu juu ya Mtume wake na juu ya Waumini, na
akawalazimisha neno la kuchamngu. Na wao walikuwa ndio wenye haki nalo na wenye
kustahili. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Hakika Mwenyezi Mungu amemtimizia Mtume wake ndoto ya haki. Bila ya shaka nyinyi
mtauingia Msikiti Mtakatifu, Inshallah, kwa amani, na hali mmenyoa vichwa vyenu
na mmepunguza nywele. Hamtakuwa na khofu. Yeye anajua msiyo yajua. Basi
atakupeni kabla ya haya Ushindi karibuni.
Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya
makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu
wakitafuta fadhila na radhi za Mwenyezi Mungu. Alama zao zi katika nyuso zao,
kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika
Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene,
ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa
ajili yao makafiri. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio amini na wakatenda mema
katika wao msamaha na ujira mkubwa.