Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi
mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mt'iini Mwenyezi Mungu
na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.
Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu,
na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
Na Mwenyezi Mungu alipo kuahidini kuwa moja katika makundi mawili ni lenu. Nanyi
mkapenda lisilo na nguvu ndio liwe lenu; na Mwenyezi Mungu anapenda ahakikishe
Haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.
Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara na ili nyoyo zenu zituwe.
Na haupatikani ushindi ila kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu, na Mwenye hikima.
Alipo kufunikeni kwa usingizi uwe ni uaminisho kutoka kwake, na akakuteremshieni
maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo na kukuondoleeni uchafu wa
Shet'ani, na kuzipa nguvu nyoyo zenu, na kuitia imara miguu yenu.
Mola wako Mlezi alipo wafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi
watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi
wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.
Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo kuwa kwa mbinu za vita au
kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na
pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.
Hamkuwauwa nyinyi lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye wauwa. Na wewe hukutupa,
walakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye tupa, ili awajaribu Waumini majaribio mema
yatokayo kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Msikizi na Mjuzi.
Kama mnataka hukumu basi hukumu imekwisha kujieni. Na mkiacha itakuwa ndio kheri
kwenu. Na mkirejea Sisi pia tutarejea. Na jeshi lenu halitakufaeni kitu, japo
likiwa kubwa. Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na Waumini.
Enyi mlio amini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapo kuitieni jambo la
kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na
moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye tu mtakusanywa.
Na kumbukeni mlipo kuwa wachache, mkionekana wanyonge katika nchi, mnaogopa watu
wasikunyakueni, naye akakupeni pahala pazuri pa kukaa, na akakutieni nguvu kwa
nusura yake, na akakupeni riziki nzuri ili mpate kushukuru.
Na walipo kupangia mpango walio kufuru wakufunge, au wakuuwe, au wakutoe.
Wakapanga mipango yao, na Mwenyezi Mungu akapanga yake. Na Mwenyezi Mungu ndiye
mbora wa mipango.
Lakini wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu, na hali ya kuwa
wanawazuilia watu Msikiti Mtakatifu? Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake, bali
walinzi wake hawakuwa ila wacha-Mngu tu. Lakini wengi katika wao hawajui.
Hakika wale walio kufuru hutoa mali yao ili kuzuilia Njia ya Mwenyezi Mungu.
Basi watayatoa, kisha yatakuwa juu yao majuto, na kisha watashindwa. Na wale
walio kufuru watakusanywa kwenye Jahannam.
Ili Mwenyezi Mungu apate kuwa pambanua walio waovu na walio wema, na kuwaweka
waovu juu ya waovu wengine, na kuwarundika wote pamoja, na kuwatupa katika
Jahannam. Hao ndio walio khasirika.
Na piganeni nao mpaka isiwepo fitna na mateso, na Dini yote iwe kwa ajili ya
Mwenyezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayo
yatenda.
NA JUENI ya kwamba ngawira mnayo ipata, basi khums (sehemu moja katika tano) ni
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na
wasafiri, ikiwa nyinyi mmemuamini Mwenyezi Mungu na tuliyo yateremsha kwa mja
wetu siku ya kipambanuo, siku yalipo kutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni
Muweza wa kila kitu.
Kumbukeni pale mlipo kuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao
wakawa ng'ambo ya mbali, na msafara ulipo kuwa chini yenu. Na ingeli kuwa
mmeagana mngeli khitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Mwenyezi Mungu
atimize jambo lilio kuwa lazima litendeke, kwa sababu aangamie wa kuangamia kwa
dalili zilizo dhaahiri, na asalimike wa kusalimika kwa dalili zilizo dhaahiri.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Kumbuka alipo kuonyesha usingizini mwako kwamba wao ni wachache - na lau angeli
kuonyesha kuwa ni wengi, mngeli ingiwa na woga, na mngeli zozana katika jambo
hilo. Lakini Mwenyezi Mungu kakuvueni. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua yalio
vifuani.
Na mlipo kutana akakuonyesheni machoni mwenu kuwa wao ni wachache, na
akakufanyeni nyinyi ni wachache machoni mwao, ili Mwenyezi Mungu atimize jambo
lilio kuwa liwe. Na mambo yote hurejezwa kwa Mwenyezi Mungu.
Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na
zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanao
subiri.
Wala msiwe kama wale walio toka majumbani mwao kwa fakhari na kujionyesha kwa
watu, na wakawazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
ameyazunguka yote wanayo yafanya.
Na pale Shet'ani alipo wapambia vitendo vyao, na akawaambia: Hapana watu wa
kukushindeni hii leo, na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipo onana majeshi mawili,
akarudi nyuma, na akasema: Mimi si pamoja nanyi. Mimi naona msiyo yaona. Mimi
namwogopa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
Na walipo sema wanaafiki, na wale wenye ugonjwa nyoyoni mwao: Watu hawa dini yao
imewadanganya. Na Mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye nguvu Ametukuka, na Mwenye hikima.
Kama ada ya watu wa Firauni na walio kuwa kabla yao - walizikataa Ishara za
Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa sababu ya madhambi yao. Na
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na mkali wa kuadhibu.
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha
watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwwnyezi
Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Ni kama ada ya watu wa Firauni na walio kabla yao - walizikanusha Ishara za Mola
wao Mlezi, basi tukawateketeza kwa madhambi yao. Na tukawazamisha watu wa
Firauni. Na wote walikuwa wenye kudhulumu.
Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari,
ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo ambao
hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya
Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa.
Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli
weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika
Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Ewe Nabii! Wahimize Waumini wende vitani. Wakiwapo kati yenu ishirini wanao
subiri watawashinda mia mbili. Na wakiwapo kati yenu mia watawashinda elfu moja
katika walio kufuru. Kwa sababu wao ni watu wasio fahamu.
Sasa Mwenyezi Mungu amekupunguzieni, na anajua kuwa upo udhaifu kwenu. Kwa hivyo
wakiwa wapo watu mia moja kati yenu wenye kusubiri watawashinda mia mbili. Na
wakiwapo elfu moja watawashinda elfu mbili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi.
Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni
Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.
Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi akiona kheri
yoyote nyoyoni mwenu atakupeni bora kuliko vilivyo chukuliwa kwenu, na
atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Ikiwa wanataka kukufanyia khiana, wao walikwisha mfanyia khiana Mwenyezi Mungu
kabla yake, na Yeye akakuwezesha kuwashinda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
Mwenye hikima.
Hakika wale walio amini na wakahama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu kwa
mali yao na nafsi zao, na wale walio toa mahala pa kukaa, na wakanusuru, hao ni
marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walio amini lakini hawakuhama, nyinyi
hamna waajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada
kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipo kuwa juu ya watu ambao
yapo mapatano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Na walio amini wakahama na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na
walio toa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata
msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema.
Na watakao amini baadaye na wakahajiri, na wakapigana Jihadi pamoja nanyi, basi
hao ni katika nyinyi. Na jamaa wa nasaba wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe
zaidi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
kila kitu.