Mwenyezi Mungu aliye ziinua mbingu bila ya nguzo mnazo ziona, ametawala kwenye
Ufalme wake, na amefanya jua na mwezi yamt'ii, kila kimoja kinakwenda kwa
kiwango maalumu. Anayapanga mambo, na anazipambanua Ishara ili mpate kuwa na
yakini kukutana na Mola wenu Mlezi.
Na ndiye aliye itandaza ardhi na akaweka humo milima na mito. Na katika kila
matunda akafanya dume na jike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika haya
zimo Ishara kwa watu wanao fikiri.
Na katika ardhi vimo vipande vilivyo karibiana, na zipo bustani za mizabibu, na
mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isio chipua kwenye
shina moja, nayo inatiliwa maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao bora kuliko
mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanao tia mambo
akilini.
Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Ati tukisha kuwa
mchanga kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio walio mkufuru Mola wao Mlezi.
Na hao ndio watao kuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio watu wa Motoni.
Humo watadumu.
Na wanakuhimiza ulete maovu kabla ya mema, hali ya kuwa zimekwisha pita kabla
yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye msamaha kwa
watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mkali wa kuadhibu.
Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili
wao yaliyomo naf- sini mwao. Na Mwenyezi Mungu anapo watakia watu adhabu hakuna
cha kuzuia wala hawana mlinzi yeyote badala yake.
Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia, kwa kumkhofu.
Naye hupeleka mapigo ya radi yakampata amtakaye. Nao wanabishana juu ya Mwenyezi
Mungu. Na Yeye ni Mwenye adhabu kali!
Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanao waomba badala yake hawawajibu
chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike
kinywani mwake, lakini hayafiki. Na maombi ya makafiri hayako ila katika
upotovu.
Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu. Sema: Basi
je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao hawajifai wenyewe kwa
jema wala baya? Sema: Hebu kipofu na mwenye kuona huwa sawa? Au hebu huwa sawa
giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walio umba kama alivyo
umba Yeye, na viumbe hivyo vikawadanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba
wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja Mwenye kushinda!
Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake.
Na mafuriko yakachukua mapovu yaliyo kusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyo
yayusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna
hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo anavyo piga mifano ya Haki na baat'ili. Basi lile
povu linapita kama takataka tu basi. Ama kinacho wafaa watu hubakia kwenye
ardhi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo piga mifano.
Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia, hata wangeli
kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangeli
vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu.
Na hapo ni pahala pabaya mno!
Na ambao husubiri kwa kutaka radhi ya Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na
wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika tulivyo wapa; na wakayaondoa maovu kwa
wema. Hao ndio watakao pata malipo ya Nyumba ya Akhera.
Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao,
na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango.
Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata
aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya fisadi katika nchi: hao ndio
watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.
Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa kipimo. Na
wamefurahia maisha ya dunia. Na uhai wa dunia kwa kulingana na Akhera si kitu
ila ni starehe ndogo.
Na wanasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake
Mlezi. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humwacha kupotea amtakaye, na humwongoa anaye
elekea kwake,
Ndio kama hivi tumekutuma kwa umma ambao wamekwsiha pita kabla yao umati
nyengine, ili uwasomee tunayo kufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani, Mwingi wa
Rehema! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Juu
yake nimetegemea, na kwake ndio marejeo yangu!
Na kama ingeli kuwako Qur'ani ndiyo inayo endeshewa milima, na kupasuliwa ardhi,
na kusemeshewa wafu, (basi ingeli kuwa Qur'ani hii). Bali mambo yote ni ya
Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua walio amini kwamba lau kuwa Mwenyezi Mungu ange
penda bila ya shaka angeli waongoa watu wote? Wala walio kufuru hawaachi
kusibiwa na balaa kwa waliyo yatenda, au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao,
mpaka ifike ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.
Je! Anaye isimamia kila nafsi kwa yale iliyo yachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi
Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au ndio mnampa khabari ya yale asiyo
yajua katika ardhi; au ni maneno matupu? Bali walio kufuru wamepambiwa vitimbi
vyao na wamezuiliwa njia. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha apotee basi hana wa
kumwongoa.
Mfano wa Bustani waliyo ahidiwa wachamngu, kati yake inapita mito, matunda yake
ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale walio walio jilinda.
Na mwisho wa makafiri ni Moto.
Na tulio wapa Kitabu wanafurahia uliyo teremshiwa. Na katika makundi mengine
wapo wanao yakataa baadhi ya haya. Sema: Nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu,
na wala nisimshirikishe. Kuendea kwake Yeye ndiyo ninaita, na kwake Yeye ndio
marejeo yangu.
Na ndio kama hivi tumeiteremsha Qur'ani kuwa ni hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na
ukifuata matamanio yao baada ya kukujia ilimu hii, hutakuwa na rafiki wala
mlinzi mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukajaalia wawe na wake
na dhuriya. Na haiwi kwa Mtume kuleta miujiza isipo kuwa kwa idhini ya Mwenyezi
Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake.
Je! Hawakuona kwamba tunaifikia ardhi tukiipunguza nchani mwake? Na Mwenyezi
Mungu huhukumu, na hapana wa kupinga hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhisabu.
Na walipanga walio kuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye mipango
yote. Yeye anajua inayo chuma kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani nyumba
ya mwisho Akhera!