SUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu
mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe
baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Na tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi mtafanya
fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi kikubwa.
Basi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia
wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie
Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa
uharibifu mkubwa.
Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta ishara ya usiku,
na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa
Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu
tumekifafanua waziwazi.
Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi
anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala
Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume.
Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi,
lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji
huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.
Anaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayo
yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo hali ya kuwa ni
mwenye kulaumiwa na kufurushwa.
Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi
wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote
wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa
hishima.
Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na aliye
uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite mpaka
katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa.
Haya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na
Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na
kufurushwa.
Zinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana
kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake.
Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira.
Na tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka kwenye
masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi
wao hugeuka nyuma wakenda zao.
Sisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo kusikiliza, na wanapo
nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati isipo kuwa mtu aliye
rogwa.
Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika
tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi.
Hao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi -
hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji rehema zake na wanaikhofu
adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo.
Na hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani
waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri,
lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.
Na tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka hao watu. Na
hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa
katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.
Akasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza juu yangu. Ukiniakhirisha
mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza dhuriya zake wasipo kuwa
wachache tu.
Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la
wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na wana, na
waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.
Na inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipo kuwa
Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni mwingi
wa kukanusha.
Au mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na kukupelekeeni
kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha msipate wa
kukunusuruni nasi.
Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini,
na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko
wengi miongoni mwa tulio waumba.
Siku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi
atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao
wala hawatadhulumiwa hata chembe.