Na wanapo kutana na walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao na
mashet'ani wao husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu.
Mfano wao ni kama mfano wa aliye koka moto, na ulipo tanda mwangaza wake kote
kote Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawawacha katika giza, hawaoni.
Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina giza na radi na umeme; wakawa
wakitia vidole vyao masikioni mwao kwa ajili ya mingurumo, kwa kuogopa kufa. Na
Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.
Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea mwangaza huenda, na unapo
wafanyia giza husimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu angeliondoa kusikia kwao na
kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni hii ardhi kuwa kama tandiko, na mbingu
kama paa, na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa matunda yawe
riziki zenu. Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua.
Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyo mteremshia mja wetu basi leteni sura moja ya
mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema
kweli.
Na wabashirie walio amini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo
mito kati yake; kila watapo pewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyo
pewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyo fanana; na humo watakuwa na wake walio
takasika; na wao humo watadumu.
Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake.
Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi,
lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano
huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila
wale wapotovu,
Wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyo
amrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio
wenye khasara.
Na pale Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi
Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakaye fanya uharibifu humo na
kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu
wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyo yajua.
Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipo waambia majina yake alisema:
Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua
mnayo yadhihirisha na mliyo kuwa mnayaficha?
Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa
popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu.
Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyo kuwamo, na
tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa
makaazi yenu na starehe kwa muda.
Kisha Adam akapokea maneno kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia
toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.
Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uwongofu utokao kwangu, basi
watakao fuata uwongofu wangu huo haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.
Na aminini niliyo yateremsha ambayo yanasadikisha mliyo nayo, wala msiwe wa
kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa thamani ndogo. Na niogopeni Mimi
tu.
Na vile tulipo kuokoeni kwa watu wa Firauni walio kupeni adhabu mbaya,
wakiwachinja wana wenu wa kiume na wakawawacha hai wanawake; na katika hayo
ulikuwa ni mtihani mkubwa ulio toka kwa Mola wenu Mlezi.
Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu
nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na
ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu. Naye akapokea toba
yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba na Mwenye kurehemu.
Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni Manna na Salwa;
tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyo kuruzukuni. Nao hawakutudhulumu
Sisi lakini walikuwa wanajidhulumu nafsi zao.
Na tulipo sema: Ingieni mji huu, na humo mle mpendapo maridhawa, na ingieni
katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni: Tusamehe! Tutakusameheni makosa
yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
Lakini walio dhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa waliyo ambiwa. Kwa hivyo
tukaiteremsha juu ya wale walio dhulumu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya
walivyo kuwa wamepotoka.
Na Musa alipo omba maji kwa ajili ya watu wake, tulimwambia: Lipige jiwe kwa
fimbo yako. Mara zikatimbuka chemchem kumi na mbili; kila kabila ikajua mahali
pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe riziki ya Mwenyezi Mungu, wala
msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.
Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi
tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea katika ardhi, kama mboga
zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema:
Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo
viomba. Na wakapigwa na unyonge,na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya
Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi
Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na wakapindukia
mipaka.
Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini
Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa
Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
Na tulipo chukua ahadi yenu, na tukaunyanyua mlima juu yenu (tukakwambieni):
Shikeni kwa nguvu haya tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili
mpate kujilinda.
Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje
ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa
Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni ng'ombe gani? Akasema:
Hakika Yeye anasema kwamba ng'ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa
katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini rangi yake? Akasema: Yeye
anasema, kuwa ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza
wanao mtazama.
Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona
ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda,
tutaongoka.
Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni ng'ombe asiye tiwa kazini kulima ardhi wala
kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi
wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.
Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, hata zikawa kama mawe au ngumu
zaidi; kwani kuna mawe yanayo timbuka mito, na kuna mengine yanayo pasuka
yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa sababu ya khofu ya
Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayo yafanya.
Na wanapo kutana na wale walio amini husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao,
wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyo kufunulieni Mwenyezi Mungu ili wapate
kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi? Basi hamfahamu nyinyi?
Basi ole wao wanao andika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka
kwa Mwenyezi Mungu, ili wachumie kwacho pato dogo. Basi ole wao kwa yale iliyo
andika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayo yachuma.