Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora
mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu,
ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu
yao kundi la Waumini.
Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na
mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mshirikina. Na hayo
yameharimishwa kwa Waumini.
Na wanao wasingizia wanawake mahashumu, kisha wasilete mashahidi wane, basi
watandikeni bakora thamanini, na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio
wapotovu.
Na wale wanao wasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi
ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudilia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu
ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
Hakika wale walio leta uwongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu,
bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyo yachuma katika
madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu
kubwa.
Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na
Akhera, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyo
jiingiza.
Enyi mlio amini! Msizifuate nyayo za Shet'ani. Na atakaye fuata nyayo za
Shet'ani basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau kuwa si fadhila ya
Mwenyezi Mungu na rehema yake juu yenu, asingeli takasika miongoni mwenu kabisa
hata mmoja. Lakini Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Na wale katika nyinyi wenye fadhila na wasaa wasiape kutowapa jamaa zao na
masikini na walio hama kwa Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe, na waachilie
mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Wanawake waovu ni wa wanaume waovu, na wanaume waovu ni wa wanawake waovu. Na
wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao
wameepushwa na hayo wanayo yasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
Na msipo mkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini!
Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayo yatenda.
Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala
wasionyeshe uzuri wao isipo kuwa unao dhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya
vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba
wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa
kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao
ya kuume, au wafwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo
yaliyo khusu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajuulikane mapambo waliyo
yaficha. Na tubuni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.
Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.
Wakiwa mafakiri Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye kujua.
Na wajizuilie na machafu wale wasio pata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu
awatajirishe kwa fadhila yake. Na wanao taka kuandikiwa uhuru katika wale ambao
mikono yenu ya kulia imewamiliki, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na
wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyo kupeni. Wala msiwashurutishe vijakazi
vyenu kufanya zina kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao
wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya
kulazimishwa kwao huko, atawasamehe, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
Mwenyezi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi. Mfano wa Nuru yake ni kama shubaka
lenye kuwekwa ndani yake taa. Taa ile imo katika tungi. Tungi lile ni kama nyota
inayo meremeta, inayo washwa kwa mafuta yanayo toka katika mti ulio barikiwa,
mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakaribia mafuta yake kung'aa
wenyewe ingawa moto haujayagusa - Nuru juu ya Nuru. Mwenyezi Mungu humwongoa
kwenye Nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu,
na kushika Sala, na kutoa Zaka. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.
Na walio kufuru vitendo vyao ni kama sarabi (mazigazi) uwandani. Mwenye kiu
huyadhania ni maji. Hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu
hapo naye amlipe hisabu yake sawa sawa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa
kuhisabu.
Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyo funikwa na mawimbi juu ya mawimbi, na
juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mtu mkono wake anakaribia
asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru hawi na nuru.
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na
ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwisha jua Sala yake na namna ya
kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua wayatendayo.
Je! Huoni ya kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatisha,
kisha huyafanya mirundi? Basi utaona mvua ikitoka kati yake. Na huteremsha
kutoka juu kwenye milima ya mawingu mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na
akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmetuko wa umeme wake kupofua macho.
Na Mwenyezi Mungu ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao
huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda
kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza
wa kila kitu.
Haiwi kauli ya Waumini wanapo itwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili ahukumu
baina yao, ila ni kusema: Tumesikia, na tumet'ii! Na hao ndio wenye kufanikiwa.
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kiapo chao ya kwamba ukiwaamrisha kwa
yakini watatoka. Sema: Msiape! Ut'iifu unajuulikana. Hakika Mwenyezi Mungu anazo
khabari za mnayo yatenda.
Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume. Na mkigeuka, basi yaliyo juu
yake ni aliyo bebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyo bebshwa nyinyi. Na mkimt'ii
yeye mtaongoka. Na hapana juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe wazi wazi.
Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walio amini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya
kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla
yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia
amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na
chochote. Na watao kufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.
Enyi mlio amini! Nawakutakeni idhini iliyo wamiliki mikono yenu ya kulia na
walio bado kubaalighi miongoni mwenu mara tatu - kabla ya Sala ya alfajiri, na
wakati mnapo vua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Sala ya isha. Hizi ni nyakati
tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi,
kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyo kuelezeni Aya
zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
Na watoto wanapo fikilia umri wa kubaalighi basi nawatake ruhusa, kama walivyo
taka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo anavyo kubainishieni Mwenyezi Mungu Aya
zake, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.
Na wanawake wazee wasio taraji kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao, bila
ya kujishaua kwa mapambo. Na wakijihishimu ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
Si vibaya kwa kipofu, wala si vibaya kwa kiguru, wala si vibaya kwa mgonjwa,
wala kwenu nyinyi, mkila katika nyumba zenu, au nyumba za baba zenu, au nyumba
za mama zenu, au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami
zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za dada
wa mama zenu, au za mlio washikia funguo zao, au rafiki yenu. Si vibaya kwenu
mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba, toleaneni salamu, kuwa
ni maamkio yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, yenye baraka na mema. Hivyo ndivyo
Mwenyezi Mungu anavyo kubainishieni Aya zake mpate kuelewa.
Hakika Waumini wa kweli ni walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na wanapo
kuwa pamoja naye kwa jambo la kuwakhusu wote hawaondoki mpaka wamtake ruhusa.
Kwa hakika wale wanao kuomba ruhusa, hao ndio wanao muamini Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Na wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya kazi zao, mruhusu umtakaye
miongoni mwao, uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemmu.
Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika
Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wanao ondoka kwa uficho. Basi
nawatahadhari wanao khalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu
chungu.
Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika
Yeye anajua mlio nayo. Na siku mtapo rudishwa kwake atawaeleza waliyo yafanya.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.