Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watakushikilia
unishirikishe Mimi na usiyo kuwa na ujuzi nayo, basi usiwat'ii. Kwangu Mimi ndio
marejeo yenu, na nitakwambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Na katika watu wapo wanao sema: Tumemuamini Mwenyezi Mungu. Lakini wanapo pewa
maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wanayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya
Mwenyezi Mungu. Na inapo kuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi husema: Hakika
sisi tulikuwa pamoja nanyi. Kwani Mwenyezi Mungu hayajui yaliomo vifuani mwa
walimwengu?
Na walio kufuru waliwaambia walio amini: Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba
makosa yenu. Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni
waongo.
Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi.
Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote.
Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake
Yeye ndio mtarudishwa.
Sema: Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyo anzisha uumbaji; kisha
Mwenyezi Mungu ndiye anaye umba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza
juu ya kila kitu.
Basi haikuwa jawabu ya watu wake ila ni kusema: Muuweni au mchomeni moto!
Mwenyezi Mungu akamwokoa na moto. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanao
amini.
Na alisema: Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa
mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Kiyama
mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makaazi yenu
ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuruni.
Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuriya zake
Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera
bila ya shaka ni katika watu wema.
Je! Nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu
mnafanya maovu? Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipo kuwa kusema: Tuletee hiyo
adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wasemao kweli.
Na wajumbe wetu walipo mjia Ibrahim na bishara, walisema: Hakika sisi hapana
shaka tutawahiliki watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhaalimu.
Akasema: Hakika humo yumo Lut'i. Wao wakasema: Sisi tunajua zaidi nani yumo
humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipo kuwa mkewe aliye
miongoni mwa watao kaa nyuma.
Na wajumbe wetu walipo mfikia Lut'i, alihuzunika kwa ajili yao, na moyo uliona
dhiki kwa ajili yao. Wakasema: Usiogope, wala usihuzunike. Hakika sisi
tutakuokoa wewe na ahali zako, ila mkeo aliye miongoni mwa watao kaa nyuma.
Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema: Enyi watu wangu!
Muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msende katika ardhi
mkifisidi.
Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha kubainikieni kutokana na maskani
zao. Na Shet'ani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa
wenye kuona.
Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tulio
wapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walio nyakuliwa na ukelele;
na kati yao wapo ambao tulio wadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tulio
wazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa
wenyewe wakijidhulumu nafsi zao.
Mfano wa walio wafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui
alivyo jitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la
buibui, laiti kuwa wanajua.
SOMA uliyo funuliwa katika Kitabu, na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo
machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa
kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayo yatenda.
Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa
wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu
na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni
wenye kusilimu kwake.
Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu
(cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo
watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri.
Na walisema: Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema:
Ishara ziko kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye
kubainisha tu.
Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi baina yangu na nyinyi. Anayajua
yaliomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanao amini upotovu na wakamkataa
Mwenyezi Mungu, hao ndio walio khasiri.
Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu
ulio wekwa, basi adhabu ingeli wajia, na ingeli watokea kwa ghafla, na hali wao
hawana khabari.
Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa
ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo
ujira wa watendao,
Na ukiwauliza; Nani aliye umba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kuti'ii
amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanako geuzwa?
Na ukiwauliza: Ni nani anaye teremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi
baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu
Lillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Bali wengi katika wao hawafahamu.
Je! Hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine
wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je! Wanaamini upotovu, na neema za Mwenyezi
Mungu wanazikataa?
Na nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu au anaye
kanusha Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya
makafiri?