Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliye wafanya
Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili-mbili, na tatu- tatu, na nne-nne.
Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila
kitu.
Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu hapana wa kuizuia. Na anayo
izuia hapana wa kuipeleka isipo kuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye
hikima.
Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwengine
asiye kuwa Mwenyezi Mungu anaye kupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi?
Hapana mungu ila Yeye tu. Basi wapi mnako geuzwa?
Je! Yule aliye pambiwa a'mali zake mbaya na akaziona ni njema - basi hakika
Mwenyezi Mungu humwacha akapotea amtakaye, na humwongoa amtakaye. Basi nafsi
yako isijihiliki kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anajua wanayo yafanya.
Na Mwenyezi Mungu ndiye anaye zituma Pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha
kwenye nchi iliyo kufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndivyo kama hivyo
kutakavyo kuwa kufufuliwa.
Mwenye kutaka utukufu basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye
hupanda neno zuri, na a'mali njema Yeye huitukuza. Na wanao panga vitimbi vya
maovu watapata adhabu kali. Na vitimbi vya hao vitaondokea patupu.
Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni kutokana na udongo. Kisha kwa tone la manii. Kisha
akakufanyeni mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba, wala
hazai, ila kwa ilimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu, wala
hapunguziwi katika umri wake, ila yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni mepesi
kwa Mwenyezi Mungu.
Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri kunywa. Na haya
ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama mpya (isiyo
chacha). Na mnatoa mapambo mnayo yavaa. Na unaona ndani yake marikebu zinakata
maji ili mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.
Anauingiza usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika usiku. Na amelifanya
jua na mwezi kutumikia. Kila kimojapo kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye
Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnao waomba badala yake
hawamiliki hata ugozi wa kokwa ya tende.
Mkiwaomba hawasikii maombi yenu; na hata wakisikia hawakujibuni. Na Siku ya
Kiyama watakataa ushirikina wenu. Na hapana atakaye kupa khabari vilivyo kama
Yeye Mwenye khabari.
Na mbebaji habebi mzigo wa mwingine. Na aliye topewa na mzigo wake akiomba
uchukuliwe hautachukuliwa hata kidogo, na angamwomba jamaa yake. Hakika wewe
unawaonya wale wanao mcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na wanashika Sala. Na anaye
jitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi
Mungu.
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo
tumeyatoa matunda yenye rangi mbali mbali. Na katika milima imo mistari myeupe
na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana.
Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinakhitalifiana. Kwa
hakika wanao mcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.
Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Sala, na wakatoa
kwa siri na kwa dhaahiri katika tulivyo waruzuku, hao hutaraji biashara isiyo
bwaga.
Na hayo tuliyo kufunulia kutoka Kitabuni ni Kweli yenye kusadikisha yaliyo kuwa
kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye khabari na Mwenye
kuona.
Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateuwa miongoni mwa waja wetu. Kati
yao yupo aliye jidhulumu nafsi yake, na yupo wa katikati, na yupo aliye tangulia
katika mambo ya kheri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.
Na watasema: Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye
tuondolea huzuni zote. Hakika Mola wetu Mlezi bila ya shaka ni Mwenye kusamehe,
Mwenye shukrani.
Na walio kufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu, hawahukumiwi wakafa, wala
hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyo mlipa kila mwenye kuzidi
ukafiri.
Na humo watapiga makelele: Mola wetu Mlezi! Tutoe tufanye mema sio yale tuliyo
kuwa tukiyafanya. Kwani hatukukupeni umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka?
Na akakujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
Yeye ndiye aliye kufanyeni manaibu katika ardhi. Na anaye kufuru, basi kufuru
yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila
kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila khasara.
Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnao waomba badala ya Mwenyezi
Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi? Au wana ushirika wowote
katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na hoja zilizo wazi?
Lakini madhaalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu.
Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye zuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na
zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipo kuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole
Mwenye kusamehe.
Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji bila
ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipo wajia
mwonyaji hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki,
Kwa kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu
havimsibu ila mwenyewe aliye vifanya. Hebu hawangojei yalio wasibu watu wa kale?
Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko
katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.
Je! Hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa walio kuwa kabla
yao? Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hapana kitu kinacho weza
kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye
kujua, Mwenye uweza.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa waliyo yachuma, basi
asingeli muacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye anawachukulia mpaka
ufike muda maalumu. Basi ukifika muda wao basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kuwaona waja wake baraabara.