Hakika Dini Safi ni ya Mwenyezi Mungu tu. Na wale wanao wafanya wenginewe kuwa
ni walinzi wakisema: Sisi hatuwaabudu ila wapate kutujongeza tu kumkaribia
Mwenyezi Mungu - Hakika Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao katika wanayo
khitalifiana. Hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi aliye mwongo kafiri.
Lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka kuwa na mwana, basi bila ya shaka angeli
teua amtakaye katika alio waumba. Subhanahu, Ametakasika na hayo! Yeye ni
Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda atakalo.
Ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Hufunika usiku juu ya mchana, na hufunika
mchana juu ya usiku. Na amefanya jua na mwezi vitumike. Kila kimojapo kinakwenda
kwa kipindi kilicho wekewa. Jueni mtanabahi! Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye
kusamehe!
Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile
ile. Na akakuleteeni wanyama wa mifugo jozi nane. Anakuumbeni katika matumbo ya
mama zenu, umbo baada ya umbo, katika viza vitatu. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu
Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Hapana mungu isipo kuwa Yeye. Basi nyinyi
mnageuzwa wapi?
Mkikufuru basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa
waja wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala mbebaji habebi mzigo wa
mwingine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi. Hapo atakwambieni mliyo
kuwa mkiyafanya. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyomo vifuani.
Na taabu inapo mfikia mtu humwomba Mola wake Mlezi naye ameelekea kwake. Kisha
akimpa neema kutoka kwake, husahau yale aliyo kuwa akimwitia zamani, na
akamfanyia Mwenyezi Mungu washirika ili apoteze watu njia yake. Sema: Starehe na
ukafiri wako kwa muda mchache. Kwani hakika wewe utakuwa miongoni mwa watu wa
Motoni.
Je! Afanyae ibada nyakati za usiku kwa kusujudu na kusimama akitahadhari na
Akhera, na akitaraji rehema za Mola wake Mlezi...Sema: Ati watakuwa sawa wale
wanao jua na wale wasio jua? Hakika wanao kumbuka ni watu wenye akili.
Sema: Enyi waja wangu mlio amini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema
katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika
wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.
Basi nyinyi abuduni mpendacho badala yake Yeye. Sema: Hakika walio khasirika ni
wale walio jikhasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Tambueni kuwa hiyo
ndiyo khasara iliyo dhaahiri.
Lakini walio mcha Mola wao Mlezi watapata ghorofa zilizo jengwa juu ya ghorofa;
chini yake hupita mito. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu havunji
ahadi yake.
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni. Kisha
akayapitisha kwenye chemchem katika ardhi, kisha kwa maji hayo akatoa mimea
yenye rangi mbali mbali? Kisha hunyauka ukaiona imekuwa kimanjano, na kisha
huifanya mapepe. Bila ya shaka katika hayo upo ukumbusho kwa wenye akili.
Je! Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemfungulia kifua chake kwa Uislamu, na akawa
yuko kwenye nuru itokayo kwa Mola wake Mlezi (ni sawa na mwenye moyo mgumu?)
Basi ole wao wenye nyoyo ngumu zisio mkumbuka Mwenyezi Mungu! Hao wamo katika
upotofu wa dhaahiri.
Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na
kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi
zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndio uwongofu wa
Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi
Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa.
Je! Atakaye kuwa anapambana kwa uso wake na adhabu mbaya kabisa Siku ya Kiyama
(ni sawa na watenda wema?) Na wataambiwa wenye kudhulumu: Onjeni hayo mliyo kuwa
mkiyachuma!
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtu mwenye mabwana washirika wanao gombana, na
wa mtu mwengine aliye khusika na bwana mmoja tu. Je! Wako sawa katika hali zao?
Alhamdulillahi, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu! Lakini wengi wao hawajui.
BASI NI NANI dhaalimu mkubwa kuliko yule aliye msingizia uwongo Mwenyezi Mungu
na kuikanusha kweli imfikiapo? Je! Siyo katika Jahannamu makaazi ya hao
makafiri?
Je! Mwenyezi Mungu si wa kumtosheleza mja wake? Na ati wanakutishia kwa hao
wenginewe wasio kuwa Yeye! Na aliye hukumiwa na Mwenyezi Mungu kupotea hana wa
kumwongoa.
Na ukiwauliza: Ni nani aliye ziumba mbingu na ardhi. Bila ya shaka watasema:
Mwenyezi Mungu. Sema: Je! Mnawaonaje wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu,
ikiwa Mwenyezi Mungu akitaka kunidhuru, wao wanaweza kuniondolea dhara yake? Au
akitaka kunirehemu, je, wao wanaweza kuzuia rehema yake? Sema: Mwenyezi Mungu
ananitosheleza. Kwake Yeye wategemee wanao tegemea.
Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu kwa ajili ya watu wote kwa Haki. Basi mwenye
kuongoka ni kwa nafsi yake, na mwenye kupotoka bila ya shaka amepotoka kwa
khasara yake. Na wewe si mlinzi juu yao.
MWENYEZI MUNGU huzipokea roho zinapo kufa. Na zile zisio kufa wakati wa kulala
kwake, huzishika zilizo hukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike
wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao
fikiri.
Sema: Ewe Mwenyezi Mungu! Muumba mbingu na ardhi! Mjuzi wa yasiyo onekana na
yanayo onekana! Wewe utahukumu baina ya waja wako katika waliyo kuwa
wakikhitalifiana.
Na lau kuwa walio dhulumu wangeli kuwa na vyote viliomo duniani na pamoja navyo
vingine kama hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikomboa katika adhabu mbaya
hiyo Siku ya Kiyama. Na yatawadhihirikia kwa Mwenyezi Mungu wasiyo kuwa
wakiyatarajia.
Na dhara inapo mgusa mtu hutuomba. Kisha tunapo mpa neema zitokazo kwetu,
husema: Nimepewa haya kwa sababu ya ilimu yangu. Sio! Huo ni mtihani! Lakini
wengi wao hawajui!
Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni
Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na kwa yakini yamefunuliwa kwako na kwa walio kuwa kabla yako: Bila ya shaka
ukimshirikisha Mwenyezi Mungu a'mali zako zitaanguka, na lazima utakuwa miongoni
mwa wenye kukhasiri.
Na wala hawakumhishimu Mwenyezi Mungu kama anavyo stahiki kadiri yake. Na Siku
ya Kiyama ardhi yote itakuwa mkononi mwake, na mbingu zitakunjwa katika mkono
wake wa kuume. Subhanahu wa Taa'la Ametakasika na Ametukuka na hayo wanayo
mshirikisha nayo.
Na litapulizwa barugumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipo
kuwa aliye mtaka Mwenyezi Mungu. Kisha litapulizwa mara nyengine. Hapo watainuka
wawe wanangojea.
Na ardhi itang'ara kwa Nuru ya Mola wake Mlezi, na Kitabu kitawekwa, na
wataletwa Manabii na mashahidi, na patahukumiwa baina yao kwa haki, wala
hawatadhulumiwa.
Na walio kufuru wataongozwa kuendea Jahannamu kwa makundi. Mpaka watakapo ifikia
itafunguliwa milango yake, na walinzi wake watawaambia: Kwani hawakukujilieni
Mitume miongoni mwenu wakikusomeeni Aya za Mola wenu Mlezi na kukuonyeni mkutano
wa siku yenu hii? Watasema: Kwani! Lakini limekwisha thibiti neno la adhabu juu
ya makafiri.
Na walio mcha Mola wao Mlezi wataongozwa kuendea Peponi kwa makundi, mpaka
watakapo fikilia, nayo milango yake imekwisha funguliwa. Walinzi wake
watawaambia: Salaam Alaikum, Amani iwe juu yenu! Mmet'ahirika. Basi ingieni humu
mkae milele.
Nao watasema: Alhamdulillah, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu aliye
tutimizia ahadi yake, na akaturithisha ardhi, tunakaa katika Bustani popote
tupendapo. Basi ni malipo mazuri yaliyoje ya watendao!
Na utawaona Malaika wakizunguka pembeni mwa Kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu,
wakimtakasa na kumsifu Mola wao Mlezi. Na patahukumiwa baina yao kwa haki na
patasemwa: Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote!