Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola wao Mlezi na
kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama hakika Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa Miji
na walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano, haina shaka hiyo.
Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni.
Na Mwenyezi Mungu angeli penda ange wafanya wote umma mmoja, lakini anamwingiza
katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu hawana mlinzi wala msaidizi.
Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi
khasa. Na Yeye ndiye anaye huisha wafu. Na Yeye ndiye Mweza wa kila kitu.
Na mkikhitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu.
Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi, ninaye mtegemea na kwake Yeye
narejea.
Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi, amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu,
na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama
mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
Amekuamrisheni Dini ile ile aliyo muusia Nuhu na tuliyo kufunulia wewe, na
tuliyo wausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane
kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayo waitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake
amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye.
Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia ilimu kwa sababu ya husuda iliyo kuwa
baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya
kuakhirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka palingeli hukumiwa baina yao.
Na hakika walio rithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayo wahangaisha.
Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wala usiyafuate
matamanio yao. Na sema: Naamini aliyo teremsha Mwenyezi Mungu katika Vitabu. Na
nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu Mlezi, na
Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa
vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu
atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.
Na wanao hojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa, hoja za hawa ni
baat'ili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo ghadhabu, na itakuwa kwao
adhabu kali.
Wasio amini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini wanao amini wanaiogopa, na
wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao wanao bishana katika
khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa.
Mwenye kutaka mavuno ya Akhera tutamzidishia katika mavuno yake, na mwenye
kutaka mavuno ya duniani tutampa katika hayo, lakini katika Akhera hana fungu.
Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini asiyo itolea idhini
Mwenyezi Mungu? Na lau lisinge kuwako neno la kupambanua basi wangeli katiwa
hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu.
Utawaona hao madhaalimu wanavyo kuwa na khofu kwa sababu ya waliyo yachuma, nayo
yatawafika tu. Na walio amini na wakatenda mema watakuwamo katika mabustani ya
Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.
Hayo ndiyo aliyo wabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walio amini na wakatenda
mema. Sema: Sikuombeni malipo yoyote kwenu ila mapenzi katika kujikurubisha. Na
anaye fanya wema tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye
shukrani.
Ati wanasema: Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu akipenda atapiga
muhuri juu ya moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta upotofu na anaithibitisha
Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliomo vifuani.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wakunjulia riziki waja wake, basi bila ya
shaka wangeli panda kiburi katika dunia. Lakini anaiteremsha kwa kipimo
akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
Basi vyote mlivyo pewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa
Mwenyezi Mungu ni bora, na cha kudumu kwa ajili ya walio amini, na wakawa
wanamtegemea Mola wao Mlezi,
Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe, na akasuluhisha,
basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye
kudhulumu.
Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama
kwa mtazamo wa kificho. Na walio amini watasema: Hakika wapatao khasara ni hao
walio khasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama. Ama hakika wenye kudhulumu
watakuwa katika adhabu ya daima.
Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyo epukika itokayo kwa
Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha
kukingia.
Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwangalizi wao. Si juu yako ila
kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu,
huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyo yatanguliza mikono yao, basi
hakika mtu huyu anakufuru.
Na haikuwa kwa mwanaadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo),
au kwa nyuma ya pazia, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini
yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hikima.
Na namna hivi tumekufunulia Qur'ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini,
wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunammwongoa tumtakaye
katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.