MWENYEZI MUNGU amekwisha sikia usemi wa mwanamke anaye jadiliana nawe juu ya
mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia majibizano
yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
Wale miongoni mwenu wanao watenga wake zao, hao si mama zao. Hawakuwa mama zao
ila wale walio wazaa. Na hakika hao wanasema neno linalo chusha, na la uwongo.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kusamehe.
Na wale wanao jitenga na wake zao, kisha wakarudia katika yale waliyo yasema,
basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa maonyo kwa hayo. Na Mwenyezi
Mungu anayajua yote mnayo yatenda.
Na asiye pata mtumwa kumkomboa, basi na afunge miezi miwili mfululizo kabla
hawajagusana. Na asiye weza hayo basi awalishe masikini sitini. Hayo ni hivyo
ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi
Mungu. Na kwa makafiri iko adhabu chungu.
Hakika wanao pinzana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, watadhalilishwa kama
walivyo dhalilishwa wale walio kuwa kabla yao. Na tulikwisha teremsha Ishara
zilizo wazi. Na makafiri watapata adhabu ya kufedhehesha.
Siku atapo wafufua Mwenyezi Mungu, na awaambie yale waliyo yatenda. Mwenyezi
Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia
kila kitu.
Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo
katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wane wao, wala wa
watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio
wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama
atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Kwani huwaoni wale walio katazwa kunong'onezana kisha wakayarudia yale yale
waliyo katazwa, na wakanong'ona juu ya mambo ya dhambi, na ya uadui, na ya
kumuasi Mtume? Na wakikujia hukuamkia sivyo anavyo kuamkia Mwenyezi Mungu. Na
husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi hatuadhibu kwa haya tuyasemayo? Basi
Jahannamu itawatosha; wataingia humo! Na hayo ndiyo marejeo maovu yaliyoje!
Enyi mlio amini! Mnapo nong'ona msinong'one kwa sababu ya mambo ya madhambi, na
uadui, na kumuasi Mtume. Bali nong'onezane kwa kutenda mema na kuacha maovu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa nyote.
Kwa hakika minong'ono hiyo inatokana na Shetani ili awahuzunishe walio amini, na
wala haitawadhuru chochote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi
Mungu tu ndio wategemee Waumini.
Enyi mlio amini! Mkiambiwa: Fanyeni nafasi katika mabaraza, basi fanyeni nafasi.
Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi. Na mkiambiwa: Ondokeni, basi
ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua walio amini miongoni mwenu, na walio pewa
ilimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Enyi mlio amini! Mnapo sema siri na Mtume, basi tangulizeni sadaka kabla ya
kusemezana kwenu. Hiyo ni kheri kwenu na usafi zaidi. Na ikiwa hamkupata cha
kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kusemezana kwenu? Ikiwa hamkufanya
hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi shikeni Sala, na toeni Zaka, na
mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo
yatenda.
Huwaoni wale walio fanya urafiki na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia?
Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uwongo, na hali kuwa
wanajua.
Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda
wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto
wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na
amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo
mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe
radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la
Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.