Na hakika tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha tukawaambia Malaika:
Msujudieni Adam. Basi wakasujudu isipo kuwa Iblisi, hakuwa miongoni mwa walio
sujudu.
Mwenyezi Mungu akasema: Nini kilicho kuzuia kumsujudia nilipo kuamrisha?
Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa
udongo.
Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo fichiwa, na
akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au
msije mkawa katika wanao ishi milele.
Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na
wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je,
sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa
dhaahiri?
Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo.
Na nguo za uchamngu ndio bora. Hayo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu mpate
kukumbuka.
Eny wanaadamu! Asije Shet'ani kukufitinini kama alivyo watoa wazazi wenu Peponi,
akawavua nguo zao kuwaonyesha tupu zao. Hakika yeye na kabila yake wanakuoneni,
na nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashet'ani kuwa ni marafiki wa
wasio amini.
Na wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu, na Mwenyezi
Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi mambo machafu.
Mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua?
Sema: Mola Mlezi wangu ameamrisha uadilifu, na mumuelekeze nyuso zenu kila mnapo
sujudu, na muombeni Yeye kwa kumsafia Dini. Kama alivyo kuumbeni mwanzo ndivyo
mtavyo rudi,
Hali ya kuwa kundi moja amelihidi, na kundi jengine limethibitikiwa na upotofu.
Kwa hakika hao waliwafanya mashet'ani kuwa ndio marafiki walinzi badala ya
Mwenyezi Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka.
Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na
kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao
fanya israfu.
Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo watolea waja wake,
na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio amini katika uhai wa
duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara
kwa watu wanao jua.
Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na ya siri, na
dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asicho kiletea
uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua.
Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au
anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia sehemu yao waliyo andikiwa, mpaka
watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi mlio kuwa
mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na watajishuhudia
wenyewe kwamba walikuwa makafiri.
Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo pita kabla yenu za
majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake. Mpaka watakapo
kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi!
Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema: Itakuwa
kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi hawatafunguliwa
milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu ya
sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu.
Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe inapita mito. Na watasema:
Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia
haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi Mungu
hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Na watanadiwa
kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyafanya.
Na watu wa Peponi watawanadia watu wa Motoni: Sisi tumekuta aliyo tuahidi Mola
wetu Mlezi kuwa ni kweli. Je, na nyinyi pia mmekuta aliyo kuahidini Mola wenu
Mlezi kuwa ni kweli? Watasema: Ndiyo! Basi mtangazaji atawatangazia: Laana ya
Mwenyezi Mungu iwapate walio dhulumu,
Na baina ya makundi mawili hayo patakuwapo pazia. Na juu ya Mnyanyuko patakuwa
watu watakao wajua wote kwa alama zao, na wao watawaita watu wa Peponi: Assalamu
Alaykum, Amani juu yenu! Wao bado hawajaingia humo, lakini wanatumai.
Na hao watu wa Mnyanyukoni watawaita watu wanao wajua kwa alama zao. Watasema:
Kujumuika kwenu hakukufaini kitu, wala hicho mlicho kuwa mnafanyia kiburi.
Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumimieni maji, au chochote alicho
kuruzukuni Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika Mwenyezi Mungu ameviharimisha
hivyo kwa makafiri,
Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo, na maisha ya dunia
yakawadanganya. Basi leo Sisi tunawasahau kama walivyo usahau mkutano wa Siku
yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu.
Je, lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake? Siku yatapo fika matokeo yake
watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu walileta Haki! Je,
tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye yasiyo kuwa yale tuliyo
kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri nafsi zao, na yamewapotea waliyo
kuwa wakiyazua.
Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi katika
siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana,
ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake.
Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa
viumbe vyote.
Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa. Na
muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu
na wanao fanya mema.
Na Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara kabla ya kufika
rehema yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito tunayachunga mpaka kwenye
nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio kama hivyo tukatolesha kila
aina ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.
Na ardhi njema, yenye udongo wa rutba, hutoa mimea yenye kukua vizuri yenye
uhai, kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Na ardhi mbaya haitoi ila mimea michache,
isiyo na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo tunavyo zipambanua Ishara (Aya)
kwa watu wanao shukuru.
Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi kaumu yangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu
ya Siku iliyo kuu.
Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi wenu kwa njia ya
mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na ili mumchemngu, na ili mpate
kurehemewa?
Basi walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye katika jahazi.
Na tukawazamisha wale walio kanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu
vipofu.
Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi kwa mtu aliye
mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo kufanyeni mshike pahala pa
kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi
Mungu ili mpate kufanikiwa.
Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na tuyaache
waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa
miongoni mwa wasemao kweli.
Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha kukuangukieni kutoka kwa
Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu mliyo yaita nyinyi na
baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uthibitisho? Basi ngojeni,
mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja.
Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni
Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara
iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu
aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala
msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu.
Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na akakuwekeni vizuri
katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga
majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala msitende
uovu katika nchi kwa ufisadi.
Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa wenye kuamini
miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake?
Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa.
Basi Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu! Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola
wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi hamwapendi wenye nasaha.