Swahaba Sa'ad bin Hishaam alipomuuliza Mama wa Waumini 'Aaishah رضي الله عنها kuhusu tabia yake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alijibu:
Tabia yake ilikuwa ni Qur-aan, kwani husomi katika Qur-aan ((Na hakika wewe una tabia tukufu?)) [Abu Daawuud na An-Nasaaiy]
Jina lake pekee linatosha kuelezea tabia zake kwani Muhammad maana yake ni "Mwenye kusifiwa".
Kwa hiyo bila shaka anamiliki tabia njema zilizokamilika ambazo hakuna mtu yeyote mwingine aliyemiliki, ni cheo cha daraja ya juu kabisa hakuna atakayeweza kufikia.
Khulqah yake ya mwanzo iliyojulikana kabla ya kupewa utume ni ukweli na uaminifu hata akapewa jina na kujulikana kwa kuitwa 'Asswaadiqul-Amiyn' (Mkweli Muaminifu).
Alikuwa mpole, mwenye huruma kwa kila mtu hata kwa walio dhaifu kama masikini. Upole wake haukuwa kwa binaadamu tu bali hata kwa wanyama. Alikuwa mwenye bashasha, mkarimu, mvumilivu wa maudhi yanayomfika, alipokuwa akinyanyaswa alikuwa mwepesi wa kusamehe hata kama ni kutoka kwa mtu mjeuri kabisa na ingawa alikuwa ana uwezo wa kulipiza.
Hajapata hata siku moja kutukana au kutamka maneno mabaya. Mazungumzo yake yote yalikuwa ni ya maana yenye kufahamika.
Ni mwenye heshima, mwenye haya, hata ilibidi wakati mwingine kwa shida ya haya zake ilibidi Allaah سبحانه وتعالى Amsemee badala yake, kama siku ya harusi yake na Bibi Zaynab bint Jahsh wakati Maswahaba walibakia kuzungumza baada ya karamu naye alikuwa anataka kupumzika na mkewe:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتَ النَّبِيِّ إِلَّا أَن يُؤْذَنَ لَكُمْ إِلَى طَعَامٍ غَيْرَ نَاظِرِينَ إِنَاهُ وَلَكِنْ إِذَا دُعِيتُمْ فَادْخُلُوا فَإِذَا طَعِمْتُمْ فَانتَشِرُوا وَلَا مُسْتَأْنِسِينَ لِحَدِيثٍ إِنَّ ذَلِكُمْ كَانَ يُؤْذِي النَّبِيَّ فَيَسْتَحْيِي مِنكُمْ وَاللَّهُ لَا يَسْتَحْيِي مِنَ الْحَقِّ)) ((Enyi mlioamini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio kungojea kiwive. Lakini mtakapoitwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini Mwenyezi Mungu Hastahi kwa jambo la haki)) [Al-Ahzaab: 53]
UNYENYEKEVU WAKE
Alikuwa mnyenyekevu kabisa, akichanganyika na kila mtu akiwa Mwarabu au kabila lolote ikiwa ni mweupe au mweusi akiwa ni tajiri au masikini, watu wazima au watoto, hata watoto alikuwa akiwasikiliza na kuzungumza nao. Akicheza na vijukuu vyake na kuwaachia hata wakati akiswali wakimpandia juu ya mgongo wake.
Hakuwa akivaa nguo za fakhari za kumtambulisha utukufu wake au kumtofautisha na Maswahaba zake, wala hakuwa anaishi katika nyumba ya fakhari, wala kumiliki fenicha au vitu vya fakhari. Kitanda chake kilikuwa cha kamba.
Hakuwa na matamanio ya dunia, alikinaika nayo. Hima yake kubwa ilikuwa ni akhera tu. Siku moja aliingia 'Umar رضي الله عنه nyumbani kwake akasema 'Umar: "Sikuona chochote cha kutazama" nikasema: "Muombe Mola wako kwani Allaah Amewafungulia wafursi na warumi na Amewapa dunia (mali) na wao hawamuabudu Allaah". Akasema:
((Una shaka ewe Ibnul-Khatwaab, hao ni watu waliotanguliza mapambo katika maisha yao ya dunia)).
Pia alikuwa akisema:
((ما لي وللدنيا، ما أنا في الدنيا إلا كراكب استظل تحت شجرة، ثم راح وتركها)) صحيح سنن الترمذي
((Mimi na dunia ni wapi na wapi? Mimi si katika dunia ila kama mfano msafiri aliyepumzika chini ya mti, kisha akaondoka na kuuacha)) [Sunan At-Tirmidhiy].
Nyumbani kwake ilikuwa inawezekana kupita siku tatu bila ya moto wa kupikia chakula kuwashwa, ilikuwa ni kula tende na maji tu.
Alikuwa akitoa sadaka bila ya kukhofu umasikini, hata alipofariki hakuwa na chochote cha kumiliki wala dirham wala dinaar [Al-Bukhaariy]
Hakujiona kuwa ni mtu bora kuliko Maswahaba na juu ya kwamba ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu alikuwa haamui jambo peke yake bila ya kuchukua ushauri kwa Maswahaba zake.
UHUSIANO WAKE NA WATU WA NYUMBANI KWAKE
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa ni mpole kwa ahli zake na akimpa kila mmoja haki yake. Anapokuwa na wake zake hukaa nao na kuzungumza nao na kucheka nao, akicheza na mkewe Bibi 'Aishah رضي الله عنها kama wakati mmoja alifanya naye mashindano ya kukimbia, mara nyingine alimbeba mgongoni ili atazame wanaume waliokuwa wakicheza mchezo wa vita msikitini. Unapofika wakati wa Swalah huondoka ili kutimiza ibada hivyo kumpa Mola wake haki Yake, na alikuwa akimpa kila mtu haki yake.
Hakuwa mwenye makuu katika chakula, akila chochote alichopikiwa bila ya kulalamika.
Akisaidia kazi za nyumba kama kufagia na usafi mwingine. Hata na mfanya kazi wake alikaa naye kwa vizuri wala hakuwahi kumkaripia hata siku moja.
HEKIMA ZAKE
Alikuwa mwenye hikma katika kila hali. Anapokabiliwa na mambo mawili alikuwa akichagua lile lililokuwa jepesi maadam tu halikuvuka mipaka ya Allaah سبحانه وتعالى.
Hakujali kutoa hukumu kwa mtu yeyote hata kama ni mwanawe mpenzi maadam ni mkosa, alisema:
((والذي نفس محمد بيده، لو أن فاطمة بنت محمد سرقت لقطعت يدها)) البخاري ((Naapa kwa Yule Ambaye Nafsi ya Muhammad iko katika mikono yake (Allaah)! Ikiwa Faatwimah mtoto wa Muhammad ameiba basi nitamkata mkono wake)) [Al-Bukhaariy]
Bedui mmoja alikwenda msikitini akasimama kukojoa, Maswahaba walitaka kumkatiza na walikuwa tayari kumvamia, lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwakataza na akamuacha amalize haja yake, alipomaliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimwambia:
((إن هذه المساجد لا تصلح لشيء من هذا البول ولا القذر، إنما هي لذكر الله وقراءة القرآن)) رواه مسلم ((Msikiti huu haufai kukojolewa au kuchafuliwa bali ni kwa ajili ya kumkumbuka Allaah na kusoma Qur-aan)) [Muslim]
Maelezo hayo ni mtazamo mdogo tu kutoka katika mwanga mkubwa wa utume wake Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم. Lau kama ni kuelezea yote basi ingelihitaji vitabu na vitabu kuandikwa. Na sio sisi tu Waislamu tuliyemtambua kwa tabia zake hizo bali hata makafiri wangapi waliosoma wasifu wake Mtume صلى الله عليه وآله وسلم walikubali kuwa hakika Muhammad alikuwa ni bwana wa tabia na ni mtu wa aina ya pekee aliyekamilika kwa kila upande wa sifa.
Tunamuomba Allaah سبحانه وتعالى Atuzidishie mapenzi kwa Mtume wetu صلى الله عليه وآله وسلم na tuwe wenye kufuata tabia na nyendo zake hata tuweze kuwa karibu naye Peponi kama alivyosema mwenyewe:
عن جابر رضي اللَّه عنه أَن رسول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال: (( إِن مِنْ أَحَبِّكُم إِليَّ ، وَأَقْرَبِكُمْ مِنِّي مَجلساً يَومَ القِيَامَةِ ، أَحَاسِنَكُم أَخلاقا)(( الترمذي حديث حسنImetoka kwa Jaabir رضي اللَّه عنه kwamba Mtumeصلى الله عليه وآله وسلم amesema: (Hakika walio vipenzi kwangu na watakaokuwa karibu na mimi siku ya Qiyaamah ni wale wenye tabia njema)) [At-Tirmidhiy – Hadiyth Hasan].
Anasema Allaah سبحانه وتعالى:
(لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ)) (Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho)) [Al-Ahzaab: 21]