Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 
Kumtii Allaah Na Mtume Ni Njia Pekee Ya Uongofu
 
bakom domstolens rättspraxis ya Kii Imetayarishwa na Shani Ahmad

BismiLlaahir-Rahmaanir-Rahiym

Namshukuru Mwenyezi Mungu, ambae Ametuumba na Akatuweka katika ulimwengu ili tumuabudu Yeye pekee. Na Akatupa miongozo yenye kutuwezesha kuishi katika huu ulimwengu Aliotuumbia. Kisha Akatuletea wajumbe ili watufunze na kutubainishia miongozo hiyo ili tupate kuongoka.Napenda kuchukua nafasi hii, pia nakuomba na wewe msomaji kuchukua nafasi hii kumsalia Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), mbashiri wetu na muonyaji wetu.


Kisha ningependa kuanza kwa kusema;

Mwenyezi Mungu Mtukufu Alipotuumba akatuweka katika huu ulimwengu hakutuwacha tuu, bali alituwekea miongozo ambayo itaweza kutufikisha katika mafanikio ya upeo wa ubora wa maisha duniani.

Akatuletea Mitume ili waje kutufunza na kutuongoza, Akawapa vitabu na sahifa zilizojaa uongofu na rehema Zake.

Ili tupate mafanikio hapa duniani ni lazima tufuate miongozo hii itokayo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na tuwafuate Mitume salawatu Llaahi wasalaamuhu ‘alayhim.

Amesema Mwenyezi Mungu:

وَلَوْ أَنَّهُمْ أَقَامُوا التَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْهِم مِّن رَّبِّهِمْ لَأَكَلُوا مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِم ۚ مِّنْهُمْ أُمَّةٌ مُّقْتَصِدَةٌ ۖ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ سَاءَ مَا يَعْمَلُون    

“Na kama wangalisimamisha Taurati na Injili na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao (Qur-aan), kwa yakini wangalikula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. Lakini wako watu miongoni mwao washikao njia nzuri. Lakini wengi wao wanayoyafanya ni mabaya kabisa.”[Al-Maaidah 5: 66]
 
Na mwenye kufuata miongozo isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mitume Wake (‘Alayhimus Salaam), basi huyo atakuwa amekhiari njia ya upotofu na ataharibikiwa hapa duniani kwa kutomfuata Muumba wa dunia na vilivyomo.

Mwenyezi Mungu Amewasifu wale wanaowacha miongozo yake kuwa na ni Makafiri, Mafaasiq, na Madhaalim. [Al-Maaidah 5: 44-47]

Madhumuni ya kuandika makala hii adhimu ni kuitanabahisha nafsi yangu kwanza kisha kuwatanabahisha ndugu zangu waislam juu ya jambo hili adhimu la kumtii Allaah na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Vile vile nimekusudia kuweka wazi kwa kiasi Mola Atakachoniwezesha maana ya Sunnah, kwani inadhihirika katika maisha yetu ya kila siku kwamba, neno hili linawachanganya Waislam walio wengi.

Katika kumtii Allaah Mtukufu, Amesema ((Subhaanahu wa Ta’ala)) katika aya kadhaa, katika Qur-aan tukufu:
“na mtiini Allaah na mtiini Mtume…”

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾

“Sema: Mtiini Allaah na Mtiini Mtume, juu yake huo (mzigo) aliotwikwa (wa utume) na juu yenu mliotwikwa -kutii. Na mkimtii mtaongoka; hapana juu ya Mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi.” [An-Nuur 24: 54].
 
Kumtii Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) ni kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake, kama yalivyokuja katika Qur-aan na Sunnah. Pasi na kuzidisha au kupunguza, au kubadilisha.

Amesema katika aya ya 3 ya Suuratul A’araaf:

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٣﴾

“Fuateni mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu, wala msifuate (hao mnaowaitakidi kuwa) walinzi badala yake, ni machache mnayoyakumbuka.” [Al-A’araaf  7: 3]

Katika hizi aya mbili tukufu, kuna mazingatio makubwa lakini sisi tutajaribu kubainisha kiasi cha haja ya makala hii.

Kwanza kabisa tujue vipi Mwenyezi Mungu Anawasiliana nasi; katika Qur-aan Tukufu, Amewasiliana nasi kwa njia tofauti, kama vile simulizi za umma zilizotutangulia, au kutupa miongozo, kwa mfano Aliposema:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ﴿٨٠﴾

“Mwenye kumtii Mtume basi huyo amekwishamtii Mwenyezi Mungu. Na anaekengeuka (yule asietii anajidhuru mwenyewe). Basi  hatukukupeleka wewe uwe mlinzi kwake.” [An-Nisaa 4:  80]

Au kutuwekea hukumu za kishari’ah ambazo zinatokana ama na maamrisho au makatazo Yake (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwa mfano zile zilizokuja kukataza maovu katika jamii kama vile wizi na zile zilizokuja kutuamrisha kufanya mema katika jamii kama vile Zakaah n.k.  

Amri  maana yake ni kutaka jambo lifanyike kwa kawaida haraka iwezekanavyo kama ilivyothibiti katika Sunnah pasi na kuwa na khiari, na kuna wakati huwa ni maombi, ruhusa au pendekezo kulingana na mahitaji ya mwenye kutoa amri ile, vile vile inategemea na hali au hadhi ya muamrishaji kwa yule  anayeamrishwa.

Endapo jambo linatakiwa kufanyika kutoka kwa mkubwa kwenda kwa mdogo, hii hujulikana kuwa ni amri, kwa kawaida yule anayepewa amri ile huwa hana budi kuitekeleza. Na endapo jambo linatakiwa kufanyika kutoka kwa mdogo kwenda kwa mkubwa hii hujulikana kama ni ombi, kwa kawaida yule aombwaye ana khiari yake kutekeleza ombi hilo.

Hivyo basi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuja kwetu huwa ni amri au makatazo, na kutokana na Ukubwa Wake na Utukufu Wake Anapotuamrisha jambo ni lazima tulitimize na Anapotukataza ni lazima tuwe mbali na makatazo Yake.

Tukizingatia aya mbili tulizotangulia kuzitaja hapo juu, Mwenyezi Mungu Anatuamrisha kumtii Yeye na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kama tulivyotangulia kusema hapo juu kuwa kumtii Yeye ni kufuata maamrisho na kujiepusha na makatazo Yake, na kwa vile ni dhaahir kuwa maamrisho Yake tunayapata kupitia Qur-aan na Sunnah, hapa ana maana kuwa tushikamane na Qur-aan na Sunnah.

Na Akatilia mkazo aliposema na mumtii Mtume. Tunasema ametilia mkazo kwani ile amri ya mwanzo ya kumtii Yeye ilikwishatosheleza, kuwa tunatakiwa tumtii na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kama ilivyokuja katika miongozo Yake (Subhaanahu wa Ta’ala) Aliposema katika Suuratun Najm:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

“Na wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake). Hayakuwa haya anayoyasema ila ni ufunuo (Wahyi) uliofunuliwa kwake.” [An-Najm 53: 3-4]

Hivyo basi tunafahamu kutokana na aya hizi kuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hazungumzi ila huwa ni wahyi na si matamanio yake, kwa hali hiyo anayoyasema yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo katika kumtii Mwenyezi Mungu ni lazima tumtii na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Na katika suurat An-Nisaa:

مَّن يُطِعِ الرَّسُولَ فَقَدْ أَطَاعَ اللَّـهَ ۖ وَمَن تَوَلَّىٰ فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ﴿٨٠﴾

“Mwenye kumtii Mtume basi huyo amekwishamtii Mwenyezi Mungu. Na anaekengeuka (yule asietii anajidhuru mwenyewe). Na wala hatukukupeleka wewe uwe mlinzi kwao.” [An-Nisaa 4: 80]

Hukumu ya maamririsho ya Mwenyezi Mungu katika hukumu za shari’ah ya Kiislam ni Wajibu kuzitekeleza, maana yake ni kuwa inamuwajibikia kila Mwanaadamu kutekeleza amri za Muumba wake, pasi na kuwa na khiari.

Mambo yote yaliyo Wajibu katika Uislam hukumu yake ni kupata malipo ya ‘amali ile yule mwenye kutekeleza jambo la Wajibu au kuingia katika makosa yule mwenye kuliwacha jambo lile, ambapo humuwajibikia ghadhabu za Mwenyezi Mungu.


Madhara Ya Kutotii Amri Ya Allaah Na Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam)

Kumtii Allaah na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni Wajibu kwa Muislam kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. (angalia aya hapo juu)

Kutokumtii Mwenyezi Mungu na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuna madhara makubwa kwa Waislam au kwa wanaadamu.

Mwenyezi Mungu Ametuhadharisha na kumuasi kwa kusema katika Qur-aan:

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

“Na watahadhari wale wanaopinga amri zake (Mtume) itawapata fitnah au itawapata adhabu iumizayo.” [An-Nuur 24: 63]

Amesema Ibn ‘Uthaymiyn katika Uswuul min ‘Ilmil-Uswuul, ‘kutokana na aya hii tunapata dalili ya kuwajibika twaa ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa vile Mwenyezi Mungu Anawahadharisha wale wanaopinga amri za Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa itawapata fitnah ambayo ni misukusuko katika maisha ya dunia au adhabu iumizayo huko Akhera.

Maonyo kama haya hayaji ila kwa kuacha jambo la Wajibu, yaani ni kwamba amri ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pekee ni Wajibu kuitekeleza’.

Endapo mwanaadamu ataacha kumtii Mwenyezi Mungu atakuwa ameacha kutekeleza Wajibu wake, hali ya kuwa amepinga amri ya Mola wake ya kumtii, hali hiyo itampelekea;

Kwanza, kuingia katika dhambi ya uasi, ambayo Mwenyezi Mungu Ametuonya kwa adhabu kali ya moto kama Alivyosema katika Surat An-Nisaa:

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾

“Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akakiuka mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) Atamuingiza mtu huyo (katika) moto akae humo milele (hali ya kuwa anapata) adhabu yenye kudhalilisha.” [An-Nisaa 4: 14]

Pili, kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume kunafungamana na iymaan, ili iymaan ya mtu itimie ni lazima mtu huyo ahakikishe twaa (utiifu) inatimia, kinyume cha hivyo atakuwa katika kujidanganya, Amesema Mwenyezi Mungu katika Surat An-Nisaa:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

“Enyi Mlioamini mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wale wenye amri miongoni mwenu, na mtakapokhitilafiana juu ya jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa nyinyi ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho…” [An-Nisaa 4: 59]

Aya hii imetuwekea ubainifu kwamba yule ambae hatorudisha khitilafu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume basi huyo si katika Waumini. Hali kadhaalika tunapata mafunzo kama haya katika Surat An-Nisaa:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

“Si hivyo, naapa kwa mola wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe kuwa ndie hakimu juu ya yale yanayotokea miongoni mwao, kisha wasipate katika nafsi zao kipingamizi juu ya yale uliyohukumu na wajisalimishe kikamilifu.” [An-Nisaa 4: 65]

Haya ni mafunzo kutoka Mola muumba yaliyo wazi yasiyo na shaka, yenye kututhibitishia kuwa twaa ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ndio mhimili mkuu wa iymaan zetu na Uislam wetu mafunzo haya ni ubainifu ulio dhaahir kuwa bila ya twaa iymaan zetu na kujisalimisha kwetu ni bure na vipi utakuwa Muislam yaani mwenye kujisalimisha ikiwa bado hutekelezi amri za yule unayedai kuwa umejisalimisha kwake?

Tatu, kutokufanikiwa katika yale anayokusudia kuyafanya kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu katika Suurat Twaahaa:

قَالَ اهْبِطَا مِنْهَا جَمِيعًا ۖ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ ۖ فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ ﴿١٢٣﴾

”Akasema tokeni humo nyote, (kutakuwa na) uadui miongoni mwenu,  na ama pale utakapokufikieni kutoka kwangu uongofu, basi atakayefuata  uongofu wangu huo, basi huyo hatapotea wala hatotaabika.” [Twaahaa 20 : 123]

Katika aya hii kuna mazingatio makubwa, Mwenyezi Mungu Anatufahamisha kuwa hata baba yetu Nabii Aadam na mama yetu Hawwaa walipokiuka mipaka yake na kuacha twaa Yake, Aliwatoa katika pepo, pamoja na kuwa walitubu. Aya imeendelea na kutufunza kuwa tutakapokubali kufuata miongozo ya Mwenyezi Mungu hatutopotea wala hatutotaabika.

Na mwenye kupuuza amri za Mwenyezi Mungu basi huyo atapata maisha dhiki na taabu hata kama atakuwa na utajiri wa mali na watoto, kwa kutotii amri za Mwenyezi Mungu na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) mali yake na watoto wake watamtia katika dhiki ameahidi hivyo Mwenyezi Mungu katika Surat Twaahaa kwa kusema:

وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ

“Na atakaejiepusha na mawaidha Yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na siku ya Qiyaaamah Tutamfufua hali ya kuwa kipofu.” [Twaahaa 20: 124]

Na khatari kubwa tunayojifunza hapa ni kwamba kwa kutotii madhara yake hayaishii hapa duniani tu bali na Akhera mtu huyo atafufuliwa kipofu hali yakuwa alikuwa anaona hapa duniani.

Na katika Surat Al-Qaswas tunajifunza kuwa tutakapowacha kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na tukafuata matamanio yetu tutakuwa miongoni mwa wale waliopotea upotofu mkubwa na Mwenyezi Mungu katika hali hiyo hatotuongoa:

فَإِن لَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكَ فَاعْلَمْ أَنَّمَا يَتَّبِعُونَ أَهْوَاءَهُمْ ۚ وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّنِ اتَّبَعَ هَوَاهُ بِغَيْرِ هُدًى مِّنَ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٠﴾

“Na wasipokuitika (kufuata) basi tambua kuwa wao wanafuata matamanio yao, na ni nani aliye muovu kuliko yule anayefuata matamanio yake pasi na kuwa na uongozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi madhalimu.” [Al-Qaswas 28: 50]


Faida Za Kumtii Mwenyezi Mungu Na Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam)

Katika kumtii Mwenyezi Mungu kuna kurehemewa ndani yake kama alivyosema katika Suurat Aali ‘Imraan:

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿١٣٢﴾

“Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa.” [Aali ‘Imraan 3: 132]

Katika mafunzo ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kwamba hatoingia peponi ila yule aliepata Rehma za Mwenyezi Mungu, hivyo tukumbuke kuwa kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni jambo kubwa mno kwetu, ila kwa yule asie taka pepo katika maisha yake ya Akhera.

Na katika kumtii Mwenyezi Mungu tunapata Uongofu kama Alivyosema katika Suuratun Nuur: 54:
“na mkimtii mtaongoka”

Na katika faida za kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni kupata utukufu wa kufufuliwa pamoja na watu wema waliohakikishiwa neema za Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, Masadiki, Mashahidi na Maswaalih. Kama Alivyosema (Subhaanahu wa Ta’ala) katika Suurat An-Nisaa:

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا ﴿٦٩﴾

“Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Aliowaneemesha Mwenyezi Mungu: Manabii, na Masadiki na Mashahidi na Maswaalih (watu wema) na uzuri ulioje kwa mtu watu hao kuwa marafiki (zake).” [An-Nisaa 4: 69]

Na katika aya nyingine Suuratul Ahzaab 71 Mwenyezi Mungu Ameambatisha kumtiii Yeye na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kufuzu au kufaulu kuliko kukubwa kabisa, kufuzu huku bila shaka ni katika kupata radhi na rehema Zake (Subhaanahu wa Ta’ala), lakini, kubwa zaidi ni kupata Pepo na kuepushwa na adhabu kali zaMoto wa Mwenyezi Mungu kama Alivyosema katika Suurat An-Nisaa:

تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ ۚ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١٣﴾ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٤﴾

“Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, Yeye (Mwenyezi Mungu) Atamwingiza katika Bustani zipitazo mito mbele yake; wakae humo milele. Na huko ndiko kufaulu kukubwa.”
“na anayemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na kuiruka mipaka Yake, (Mwenyezi Mungu) Atamwingiza Motoni, humo atakaa milele na atapata adhabu zifedheheshazo.” [An-Nisaa 4: 13-14]

Ndugu zangu faida nyingi na hatuwezi kuzidhibiti zote katika makala hii, ni juu yetu kuzijua hivyo tufanye jitihada kuzitafuta ikiwa ni moja ya kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ya kutafuta elimu.

Inatupasa tukumbuke kuwa sisi ni Waislam na maana ya kuwa Muislam ni kujisalimisha au kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala), na kuyakubali yale yote aliyokuja nayo Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Kama ilivyopokelewa katika vitabu mbali mbali, amesema Abu Ja’afar At-Twahaawiy, katika ‘Aqiidat At-Twahaawiyyah, ‘Aqiydah namba 36,

“Na Uislam wa mtu hautathibiti pasi na kujisalimisha na kujiweka chini ya nguvu za Mwenyezi Mungu...”

Na kujisalimisha maana yake ni kuwa chini ya twaa ya Mwenyezi Mungu, kufanya kila Alilotuamrisha na kuwacha kila Alilotukataza, kumkusudia yeye tu katika ibada na mambo yetu yote ya maisha yetu.

Ikiwa hatuwezi kuitimiza ahadi hii adhimu tuliyompa Mwenyezi Mungu ya kujisalimisha Kwake au kuwa tayari kutekeleza maamrisho Yake yote na kuyakubali yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) wapi tunashika katika kujivunia Uislam wetu?


Maana Ya Sunnah

Ni ufahamu wa wengi miongoni mwetu kuwa Sunnah ni vitendo au ibada ambazo tunapozitekeleza tunapata ujira, na tunapo yawacha hatutopata adhabu bali tutakosa ujira tu.

Kutokana na ufahamu huu watu wengi wamejengeka na tabia ya kutotekeleza Sunnah na kusema ‘hiyo ni Sunnah tu si wajibu’, pale wanapotakiwa kutekeleza amri kati ya maamrisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Kwa hakika Sunnah ni mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), ikiwa ni miongoni mwa maneno, vitendo au yale yaliyofanywa mbele yake nae akayakiri.

Na juu ya haya ndipo tunalazimika kutekeleza Sunnah katika hali ya kuwajibika juu yetu kama ilivyobainishwa katika aya zilizokwisha tangulia hapo juu. Aya ambazo zinatuhimiza kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Hali hiyo ya kuwajibika kwetu katika Sunnah inaondoka pale tu Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anapotubainishia, au kubainishwa na wanavyuoni kwa kufuata taratibu zake zinazokubalika.


Sunnah Kama Inavyofahamika Kwa Wanachuoni Wa Fiqh

Kwanza kabisa tufahamu kuwa Sunnah ni neno la Kiarabu lenye maana ya njia ‘mwenendo’ yaani ni jambo ambalo limetokea kisha watu wakafuata mwenendo au jambo hilo. Kama ilivyopokewa kutoka kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):
 
“Mwenye kuweka mwenendo mzuri basi atapata ujira wa mwenendo huo na ujira wa watakaofuata mwenendo huo, na mwenye kuweka mwenendo mbaya atapata ujira wa mwenendo huo na ujira wa watakao fuata mwenendo huo...”

Hii ni maana ya Sunnah katika lugha.

Ama katika matumizi ya Sunnah kwa wataalamu wa Fiqh, ni amali zilizo chini ya Waajib, zinakusanya kila kile ambacho Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amekipendekeza ambacho hakiwajibiki kukifanya.
Sunnah kwa mtazamo huu hujulikana kama Manduub (mapendekezo) na hupata ujira mwenye kuzitekeleza na hatoingia makosani yule mwenye kuziacha. (M. H. Kamali, Hadith Studies)

Na huu ndio mtazamo ambao wengi wetu tunaufahamu, mtazamo wa ki- Fiqh ambao umelenga katika kutoa hukumu za kishari’ah, na si maisha ya Wanaadamu ya kila siku kwa ujumla.


Sunnah Kama Inavyofahamika Kwa Wanachuoni Wa Hadiyth

Vivile katika historia ya Dini, neno Sunnah limetumika kwa namna kadha, kwa mfano Wanachuoni wa Ahlul-Hadiyth, wanaitambua Sunnah ni chochote kile kilicho thubutu kutoka kwa Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), Semi zake , Matendo yake, Yote yaliotendeka mbele yake na akayanyamazia, historia yake, Tabia na Maumbile yake. Baadhi ya Maulamaa wamewaita Wanachuoni wa Hadiyth ndio Ahlu-Sunnah.

Baadhi ya Wanachuoni wakubwa wa karne ya tatu Hijriyyah waliandika vitabu kuhusiana na ‘Aqiydah na kuyapa majina As-Sunnah. Zama hizo watu walikuwa wanajulikana ni watu wa Sunnah kama ni katika Manhaj sahihi ya ki-’Aqiydah. Pia ilitumika kinyume cha Sunnah; Bid'ah (Uzushi) kwa kubainisha wale ambao si katika Manhaj sahihi ya ki-’Aqiydah.


Sunnah Kama Inavyofahamika Kwa Wanachuoni Wa Uswuuliyyuun

Amma Wanachuoni wa Uswuliyyuun, wanaitambua Sunnah yakuwa ni sehemu kuu ya pili baada ya Qur-aan kuwa ndio chimbuko la shari’ah ya Dini yetu, hivyo Sunnah kwao ni Semi zote za Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), Matendo yake na yale yote yaliotendeka mbele yake na akayanyamazia. Na hii ndio maana halisi ya neno Sunnah inayopaswa itumike na kufahamika.

Sunnah katika maana yake pana ni Maneno naVitendo vyake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na yale yaliyotendeka mbele ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) naye akayakubali.

Katika mtazamo huu Sunnah ina maana pana na inakusanya maisha yetu ya kila siku na si Hukumu za kishari’ah pekee.


Sunnah Imegawika Sehemu Mbili Kuu:

Sunnah zinazowajibisha na zile zinazopendekeza;

Sunnah zinazowajibisha ni zile kauli au vitendo vya  Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) zinazobainisha amri za Mwenyezi Mungu au yale mafunzo ya  Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) miongoni mwa maamrisho na makatazo, miongoni mwa Ibada, Mu’amala na maisha kwa ujumla, kwa mfano, Swalah, alipotufundisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kwa kusema:

صلوا كما رأيتموني أصلي

“Swalini kama mlivyoniona mimi ninavyoswali”

Amesema katika Hajj:

خذوا عني مناسككم

 “Chukueni kutoka kwangu ibada yenu (ya Hajj).

Katika Zakaah na Miyraath ameainisha vigawanyo vyake, katika Swawm ametubainishia wakati wake, inavyoanza Swawm na inavyokwisha na ibada nyingi tunazozijua. Na kimaumbile kama ndevu n.k.

Na Sunnah za kujitolea (tatwawuu’) nazo ni aina mbili, kwanza zilizotiliwa mkazo (Muakkadah), hizi ni zile ambazo Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amezidumisha mpaka mwisho wa uhai wake kama baadhi ya Swalah za Qabliyyah na Ba’adiyyah na kuna zisizotiliwa mkazo (nawaafil) nazo ni baadhi ya Swalah za Qabliyah na Ba’adiyah, kusoma sura baada ya Suuratul Faatihah katika rakaa mbili za mwanzo n.k.

Hivyo basi kwa wale wanaotegemea kuwa Sunnah ni yale tunayopata ujira tunapotekeleza na kutopata pale tunapowacha, watakuwa wanaamini kuwa ibada zoote hizi hazina ulazima  na itakuwa taabu kwao kupata ibada ambayo inawawajibikia pasi na kuwa ni Sunnah ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Baada ya kuona udhaifu huu wa kuamini kuwa Sunnah ni yale ambayo mja ana khiari kuyatekeleza ni vizuri kuweka ufahamu wa Sunnah sawa.

Kwa hakika Sunnah ni mafundisho ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), ikiwa ni miongoni mwa maneno, vitendo au yale yaliyofanywa mbele yake nae akayakiri.

Na juu ya haya ndipo tunalazimika kutekeleza Sunnah katika hali ya kuwajibika juu yetu kama ilivyobainishwa katika aya zilizokwishatangulia hapo juu. Aya ambazo zinatuhimiza kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Hali hiyo ya kuwajibika kwetu katika Sunnah inaondoka pale tu Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anapotubainishia, au kubainishwa na wanavyuoni kwa kufuata taratibu zake zinazokubalika.

Kama tulivyotanguliza hapo juu kuwa katika Sunnah kuna yaliyo Waajib na yale ya kujitolea.
Yaliyo Waajib ni yale yote ambayo Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametufundisha na kutuamrisha kuyafanya au kutukataza, kwa mfano, Swalah, Swawm, katika Ibada.
Na katika Mu’amalah ni kufuata mafundisho yake, mfano katika biashara, kuepuka Ribaa, kuwepo na makubaliano na makabidhiano n.k. katika maisha yetu ya kila siku mfano adabu za kula (mkono wa kulia), kuvaa mavazi ya kishari’ah kama nguo isiyoburura kupita chini ya mafundo ya miguu, na za kimaumbile kama vile kutahiri, kuweka ndevu n.k.

Haya yanabainika kwa kusoma taathira za kutokufuata mafunzo ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwa mfano, Hadiyth iliyopokelewa alipomuamrisha mtu kula kwa mkono wa kulia, mtu yule kwa ujeuri akasema hawezi, kwa kujua jeuri na kibri chake mtu yule, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema, anakataa kwa jeuri basi hatoweza kuunyanyua mkono wake tena, na ikawa kama Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alivyosema mtu yule alipata ulemavu na mkono wake wa kulia ukapooza na hakuweza kuutumia tena.

Pia imepokelewa kuwa Ibn ‘Abbaas aliwahi kusema nakhofia watu kuja kushukiwa na mawe kutoka mbinguni kuwangamiza, mimi nasema Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema wao wanasema Abu Bakr amesema, ‘Umar amesema. Hii ni kuonyesha umuhimu wa kufuata kauli za Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuacha kauli za wasiokuwa yeye hata kama ni Swahaba.

Vipi Tutabainisha Sunnah?

Tunaweza kubainisha Sunnah zilizo Waajib na Manduub au Tatwawuu’, kutokana na maneno yaliyotumika kwa mfano maamrisho na makatazo siku zote huwa yana wajibisha kufanya au kuwacha kufanya jambo, mpaka pale itakapopatikana njia nyingine itakayoonesha kuwa amri ile ni pendekezo la Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Kwa vile huu ni mlango mzima wa elimu si rahisi kuufungua katika makala hii, hivyo nawaomba wasomaji tufanye hima kuutafuta mlango huu ili tuweze kujua Sunnah za Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na tuweze kuzifuata kwa usahihi ili tuepuke kuingia katika fitnah au tuweze kutoka katika fitnah ambazo tumo ndani yake na Mwenyezi Mungu Atatuonyesha njia yake iliyo sahihi na kutupa radhi Zake Atatuepusha na adhabu yake iumizayo.


 Posted By Posted juu ya Thursday, May 10 @ 20:34:19 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi bakom domstolens rättspraxis ya Kii
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu bakom domstolens rättspraxis ya Kii:
Simulizi (Kisa) Ya Hijaab Ya Khawla: Maoni ya Hijaab


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa RafikiMada zinazohusiana

bakom domstolens rättspraxis ya Kii

 

EsinIslam The Muslim World Portal For Islamics, News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Quranic Islamic Articles, Radio, Audio Quran, TV Channels, Fatwa Rulings, Muslim News Newspapers Magazines Headlines Articles Forums Schools, Universities, Colleges, Mosques, Qur'an, Hadith, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Fasting Ramadan, Vidoes, Books On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com