Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 
Mtume (Swalla Llaahu ĎAlayhi Wa Sallam) Akiwa Madiynah
 
Habari Idadi ya habari na hadithi Makala
Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Akiwa Madiynah


Anasema Shaykh Abu Bakr Al-Jazairiy:


"Hakika ya miaka yote kumi na tatu aliloishi Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pale Makkah tokea alipopewa utume mpaka siku ile aliyohama kwenda Madiynah, yote ilikuwa ni maumivu na machozi na huzuni. Hakupata kufurahi hata kwa muda wa saa moja au kustarehe angalau kwa siku moja.Ama miaka kumi aliloishi Madiynah, yote ilikuwa ni miaka ya Jihaad iliyokamatana. Hakupata hata siku moja kukaa bure wala kustarehe. Hata maisha; kwake yalikuwa magumu, hakupata hata siku moja kushiba mkate au tende wala hata kula vizuri mara mbili katika siku moja.

Naam, ingawaje kwa siku alizoishi Madiynah zilikuwa ni siku za kuchomoza, lakini siku nyingi katika hizo zilikuwa ni za kuunguza".

Kusilimu Kwa ‘Abdullaah Bin Salaam (Radhiya Llaahu ‘Anhu)

Mara baada ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwasili mji wa Madiynah alikuja kwake ‘Abdullaah bin Salaam (Radhiya Llaahu ‘anhu) na kuzitamka shahada mbili.

Akasema:

"Nashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba wewe ni Mtume wa Allaah na kwamba uliyokuja nayo ni haki. Ee Mtume wa Allaah, Mayahudi ni watu waongo, wanajua kuwa mimi ni bwana wao na mwana wa bwana wao na wanajuwa pia kuwa mimi ni ‘Aalim wao na mwana wa ‘Aalim wao, kwa hivyo nakuomba (uniache nijifiche, kisha) uwaite na uwaulize juu yangu kabla ya kuwajulisha juu ya kusilimu kwangu, kwani wakijua kuwa nimesilimu watasema juu yangu yale nisiyokuwa nayo".
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaita Mayahudi, na walipohudhuria akawaambia:
((Enyi Mayahudi! Adhabu kali itakufikieni, mcheni Allaah, Naapa kwa yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, kuwa munajua vizuri kwamba mimi ni Mtume wa kweli wa Allaah na kwamba niliyokuja nayo ni haki, kwa hivyo ingieni katika dini ya Kiislam.))
Wakasema mara tatu:
"Sisi hatujui"
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:
((Ana daraja gani kwenu ‘Abdullaah bin Salaam?))
Wakasema:
"Yule ni bwana wetu na mwana wa bwana wetu, na ‘Aalim kutupita sote na mwana wa ‘aalim kutupita sote".
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:

((Munaonaje akisilimu?))
Wakasema:
"Haiwezekani hata siku moja akasilimu"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza hivyo mara tatu, kisha akasema:
((Ee ‘Abdullaah bin Salaam, watokee.))
Akawatokea na kusema:
"Enyi Mayahudi, mcheni Allaah kwani naapa kwa yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, mnajua vizuri kuwa huyu ni Mtume wa Allaah na kwamba amekuja na haki".
Wakasema:
"Muongo! wewe si bwana wetu wala si ‘Aalim wetu".
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaamrisha watolewe nje.

[Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Mwenye Kumtii Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Atakuwa Pamoja Naye

Maswahaba wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na hususan watu wa Madiynah walikuwa wakimpenda Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kupita kiasi, na walikuwa tayari wakati wote kuzitanguliza roho zao na nafsi zao kwa ajili ya kumlinda Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na yale aliyokuja nayo. Ni wao waliohatarisha maisha yao hapo mwanzo walipomfuata Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) huko Makkah katika usiku ule wa hatari na kumpa ahadi ya kumnusuru na kumlinda ikiwa atahamia kwao Madiynah. Kisha wakafungamana naye kwa siri mahali panapoitwa Al-’Aqabah katika mafungamano yaliyokokuja kujulikana baadaye kama 'Fungamano la ‘Aqabah' (la mwanzo na la pili).
Watu wa Madiynah waliitimiza ahadi yao hiyo ya kumlinda Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na kuwalinda Waislam wote waliohamia kwao na kuwasaidia kwa hali na mali. Na pale Allaah Subhaanahu Wa Ta’ala Alipoiteremsha kauli Yake:
{{Wameruhusiwa (kupigana vita) wale wanaopigwa kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Allaah ni Muweza wa kuwasaidia. Ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema; "Mola wetu ni Allaah.}} [Al-Hajj: 39-40]
Watu wa Madiynah wakaingia katika mapambano mbali mbali na majeshi ya makafiri mpaka pale Allaah alipowawezesha Waislamu kuuteka mji wa Makkah na kuyabomoa masanamu yaliyokuwepo ndani ya Al-Ka’abah na kuidhihirisha Haki na kuiangamiza Baatwil.
Hadiyth ifuatayo inatuwezesha kuihisi angalau kwa uhaba ladha ya namna Maswahaba (Radhiya Llaahu ‘anhum) na hasa watu wa Madiynah walivyokuwa wakimpenda na kumuenzi na kumthamini Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na namna gani walivyokuwa tayari kujitolea kwa hali na mali kumtii Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Imetolewa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim na Atw-Twabaraaniy na wengineo kuwa mara baada ya kumalizika vita vya kuuteka mji wa Makkah, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwakusanya mateka na kuwauliza:
((Mnadhani nitakufanyeni nini?))
Wakajibu:

((Utatufanyia kila la kheri, ewe ndugu mwema na mwana wa ndugu mwema.))
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:
((Nendeni, nyote nimekuacheni huru.))
Karibu mateka wote hao wakasilimu kwa hiari yao na kujiunga na jeshi la Kiislamu lililoondoka hapo Makkah kuelekea mji wa Hunayn kwa ajili ya kupambana na majeshi ya watu wa Huwzan waliokuwa njiani kuelekea Makkah kuwashambulia Waislam.
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zayd (Radhiya Llaahu ‘anhu) kuwa baada ya Waislam kushinda katika vita vya Hunayn, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwagawia ngawira iliyopatikana katika vita hivyo watu wa Makkah tu hasa wale waliosilimu hivi karibuni kwa ajili ya kuwalainisha nyoyo zao, na watu wa Madiynah hawakupewa chochote.

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alijuwa kuwa watu wa Madiynah hawakufurahi kwa sababu na wao pia walitegemea kupewa chochote katika ngawira ile kama walivyopewa wenzao watu wa Makkah.
Alipojulishwa juu ya hayo, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaita watu wa Madiynah na kuwahutubia, akasema:
((Nini haya maneno niliyosikia kuwa mlikuwa mkiyasema?))
Viongozi wao wakasema:
"Ama wakubwa wetu hawakusema lolote, isipokuwa watu wengine wanasema; "Allaah Amghufirie Mtume wake, anawapa Maquraysh ngawira kwa mamia na sisi hatupi chochote wakati damu zao bado hata hazijakauka juu ya panga zetu?"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
((Mmekasirika kwa sababu ya faida ndogo tu ya kidunia enyi watu wa Madiynah? Mimi nimewapa hawa kwa sababu wao ndio kwanza wametoka katika ukafiri na kuingia katika Uislam ili niwalainishe nyoyo zao, nikakuacheni nyinyi kwa kuutegemea Uislam wenu. Enyi watu wa Madiynah! Si niliwakuta mmepotoka Allaah Akakuongozeni kupitia kwangu? Na nikawakuta masikini na Allaah Akakutajirisheni kupitia kwangu? Mmegawanyika na Allaah Akakuunganisheni kupitia kwangu? Mafakiri na Allaah Akakuneemesheni kupitia kwangu?))
Walikuwa kila wanapoulizwa wakijibu:
"Allaah Ametufanyia ihsani zaidi na Mtume Wake ametufanyia Ihsani zaidi"
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:

((Mbona hamnijibu?))

Wakasema:
"Tukujibu nini ee Mtume wa Allaah?"
Akasema:
((Kama mngenijibu kwa maneno mengine zaidi ya haya mngekuwa mnasema kweli. Mngetaka, mngeweza kusema; "Na wewe pia ulikuja kwetu ukiwa ume*****uzwa na watu wako na sisi tukakupokea, umekadhibishwa na sisi tukakusadiki. Ulikuja peke yako umo hatarini na sisi tukakunusuru, na tukayakubali yale watu wako waliyoyakataa. Kisha mkawa mnanihesabia mema yote mliyonitendea.))
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:
((Hamridhiki wakati wenzenu wanaondoka wakiwa na ngamia na kondoo na nyinyi mtaondoka mkiwa na Mtume wa Allaah mpaka makwenu? Watu wa Madiynah (Al-Answaar) ni mfano wa nguo iliyokamatana na ngozi na waliobaki ni mfano wa guo la juu, Enyi watu wa Madiynah! Si Allaah Amekuiteni majina mazuri mazuri (kama vile) 'Answaar wa Allaah' na 'Answaar wa Mtume Wake?' Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, lau kama nisingehajiri basi ningelikuwa mmoja kati ya watu wa Madiynah, na lau kama watu wote watafuata njia zao katika mabonde na mitaa, na watu wa Madiynah watafuata njia nyingine, basi mimi ningefuata njia ya watu Madiynah. Allaah Warehemu ma-Answaar (watu wa Madiynah) na wana wa Answaar na wajukuu wa Answaar.))
Anasema Ibn Is-haaq aliyoisimulia sehemu ya mwisho ya Hadiyth hii kuwa:
"Waliohudhuria wakaanza kulia kwa kwikwi mpaka ndevu zao zikarowa, wakasema:
"Tumeridhika na Allaah kuwa Mola wetu na Mtume Wake kuwa sehemu yetu."
Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaondoka na wao wakatawanyika.
Sehemu ya mwisho ya Hadiyth hii imepokelewa kwa njia ya Imaam Ahmad peke yake na kusimuliwa na Ibn Is-haaq.
Ndugu zangu Waislam, anayetaka kuwa pamoja na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum) siku ya Qiyaamah, lazima awe mtiifu wa maamrisho aliyokuja nayo Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Imepokelewa na Atw-Twabaraaniy na Ibn Mardawiya na Abu Na’iym kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhiya Llahu anhum) kuwa: Siku moja mtu mmoja alimwendea Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:

"Ee Mtume wa Allaah, kwa hakika mimi nakupenda kuliko ninavyoipenda nafsi yangu na kuliko ninavyowapenda wanangu. Ninapokuwa nyumbani basi nikikukumbuka tu, siwezi kustahamili tena, lazima nije nikutazame. Lakini kila ninapokumbuka kuwa siku moja mimi nitakufa na wewe utakufa, kisha nikakumbuka kwamba wewe daraja yako itakuwa juu pamoja na Mitume, na mimi nikiingia Peponi naogopa (daraja yangu haitokuwa ya juu kama yako) nisiweze kukuona tena huko".
Katika riwaya nyingine:
"Swahaba yule aliyekuwa katika watu wa Madiynah alilia sana, na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipomuuliza:
((Nini kinachokuliza?))
Akamjibu:
"Kila ninapokumbuka kuwa wewe daraja yako itakuwa ya juu pamoja na Mitume, na mimi nikiingia Peponi naogopa (daraja yangu haitokuwa ya juu kama yako) na sitoweza kukuona tena huko".
Kabla Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwahi kumjibu Swahaba yule (Radhiya Llaahu ‘anhu), Jibriyl (‘Alayhis Salaam) aliteremka na kauli ya Allaah isemayo:

{{Na Mwenye kumtii Allaah na Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Aliowaneemesha Allaah; Manabii na Swddiqiyn na Mashahidi na Swaalihiyn (watu wema). Na uzuri ulioje (kwa mtu) watu hao kuwa rafiki (zake).}} [An-Nisaa: 69]

Yaani atakayefanya yale aliyoamrishwa na Mola wake na Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na akayaacha yale alokatazwa na Mola wake na aliokatazwa na Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), basi Allaah Atamuingiza katika Pepo yake na atakuwa pamoja na Manabii na Swiddiqiyn na Mashahidi na Swaalihiyn (watu wema).

 Posted By Posted juu ya Thursday, May 10 @ 22:46:03 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Habari Idadi ya habari na hadithi Makala
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Habari Idadi ya habari na hadithi Makala:
Vidokezo Muhimu Kwa Wazazi Wenye Wasichana Na Wavulana


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa RafikiMada zinazohusiana

Habari Idadi ya habari na hadithi Makala

 

EsinIslam The Muslim World Portal For Islamics, News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Quranic Islamic Articles, Radio, Audio Quran, TV Channels, Fatwa Rulings, Muslim News Newspapers Magazines Headlines Articles Forums Schools, Universities, Colleges, Mosques, Qur'an, Hadith, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Fasting Ramadan, Vidoes, Books On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com