Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 
Baada Ya Kuhamia Madiynah: Mwenendo Wa Mitume ('Alayhimus Salaam)
 
Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy

Ndugu zangu Waislam, katika kalenda ya Hijri (Kalenda ya Kiislam) imeanza, na kwa ajili hiyo tutajikumbusha kidogo juu ya umuhimu wa siku hizi kwa ajili ya kuelewa umuhimu wake na kwa ajili ya kujifunza angalau machache juu ya Hijrah ya Mtume wetu mtukufu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhu).

Mwaka jana katika mnasaba huu, tulisoma namna gani tukio la Hijrah lilivyokuwa muhimu kupita matukio yote yaliyopata kutokea katika historia ya Kiislam, na hii ni kwa sababu kutokana na Hijrah, taifa la mwanzo la Kiislam liliweza kuundwa, na Waislamu wakaweza kuweka miguu yao juu ya ardhi, madhubuti kwa ajili ya kuisimamisha dini yao, kuilinda itikadi yako, na kuweza kuieneza ulimwenguni kote.

Mtume Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wa mwanzo waliokuwa wachache sana, wakiongozwa na Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhiya Llaahu ‘anhum), walihiari kuhatarisha maisha yao, kupoteza mali zao, milki zao pamoja na kila walichokuwa nacho kwa ajili ya kutaka radhi za Mola wao Subhaanahu wa Ta’ala.


Allaah Anasema:

{{Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Allaah.}} [Al-Fath: 29]


Tukasema kuwa kwa ajili ya umuhimu wake, ndiyo maana Waislam walikubaliana kuianzisha Kalenda ya Hijrah ya Kiislam kuanzia mwaka huo.


Siku tukufu ambayo Mtume wetu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akifuatana na Sahibu yake Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu), walihama kutoka Makkah kwenda Madiynah, wakitanguliwa na kufuatiliwa na Maswahaba watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum).


Waislamu ambao wakati huo walikuwa wachache sana, walipata mtihani mkubwa kutokana na mateso waliyopata pamoja na kudharauliwa na kunyanyaswa na makafiri wa Makkah. Lakini mara baada ya kutakiwa na Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuihama nchi yao hiyo na kwenda Madiynah, wakaanza kukumbana na mtihani mwingine. Mtihani wa kuiacha nchi yao, nchi waliyozaliwa na kulelewa na kucheza juu ya mchanga wake. Iliwabidi waiache nchi hiyo pamoja na kuacha nyuma mali zao, nyumba zao na kila walichomiliki isipokuwa vichache sana walivyoweza kuvibeba katika safari ndefu iliyojaa kila aina ya hatari na mashaka. Walikuwa tayari kupambana na yote hayo kwa ajili ya utiifu wao kwa Mola wao na kwa ajili ya kuinusuru na kuiendeleza dini yao.


Kwa vile wengi wao walitoka nyakati za usiku kwa kujificha wakihofia maisha yao, iliwabidi waache vitu vyao vingi vilivyokuwa vizito na vengine vya thamani, ili waweze kukimbia kwa wepesi na haraka na ili wasalimike na mateso ya Maquraysh. Waliacha vyote hivyo nyuma yao na kuianza safari ndefu iliyowawezesha kufika kwa ndugu zao waliokuwa wakiwasubiri kwa hamu na shauku kubwa sana huko Madiynah ili washirikiane nao katika kuiendeleza mbele dini yao hii tukufu na mpya.


Anasema Ibn Kathiyr katika Al-Bidaayah wan Nihaayah kuwa:

"Katika mwaka wa kumi na sita na inasemekana katika mwaka wa kumi na saba wa Ukhalifa wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu), Waislam walikubaliana kuianzisha Kalenda yao, kutokana na matatizo yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara baina yao wakati watu wakiandikiana mikataba ya madeni au ya aina nyengine.


Waarabu walikuwa wanayohesabu ya miezi yao, lakini hawakuwa na hesabu ya miaka, na kwa ajili hiyo wengine walikuwa wakitumia kalenda za Kifursi na wengine za Kirumi na wengine wakitumia matukio ya wakati wa ujahilia.


‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) alipowataka Waislam kutoa rai zao kuhusu jambo hilo, wengine wakapendekeza ianzie mwaka aliozaliwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na wengine wakapendekeza ianzie pale alipopewa Utume na wengine wakapendekeza siku aliyokufa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini Khalifa wa Waislam ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) akapendelea rai zilizosema kuwa ianzie siku ile ya Hijrah na wengi wakakubaliana naye.


Kwa vile mwezi wa Muharram ndio mwezi wa mwanzo wa Kiarabu, wakakubaliana kuhesabu kuanzia mwezi huo."


Ufuatao ni mpangilio wa Miezi ya Kiislam:

MUHARRAM (Mfunguo nne)

Swafar

Rabiy’ul Awwal (Mfunguo sita)

Rabiy’uth Thaaniy

Jumaadal Awwal

Jumaadath Thaaniy

RAJAB

Sha’abaan

Ramadhaan

Shawwaal

DHUL QA’DAH (Mfunguo pili)

DHUL HIJJAH (Mfunguo tatu)


Baada ya kutoa dalili mbali mbali, Mwanachuoni Ibn Kathiyr katika kitabu chake hicho mashuhuri kiitwacho Al-Bidaayah wan Nihaayah akamaliza kwa kusema:


"Nimekuelezeeni kwa ushahidi wa kutosha ulioandamana na isnadi zake na njia zake kutoka katika Siyrah ya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) na AlhamduliLlaah na kusudi langu ni kuwa wao (Maswahaba) walikubaliana wote kwa Ijmai kuianzisha Kalenda ya Kiislam kuanzia Mwaka wa Hijrah na wakakubaliana kuufanya mwezi wa mwanzo uwe mwezi wa Muharram na hii pia ni kauli za Maimaam wote waliobaki".


Ama kuhusu rai ya Imaam Maalik, Ibn Kathiyr ameandika yafuatayo:


"Amesema As-Suhayliy na wengineo kuwa Imaam Malik amesema kwamba mwanzo wa Mwaka wa Kiislam ungeanzia mwezi wa Rabiy’ul-Awwal (na si Muharram), kwa sababu mwezi huo ndio aliohama ndani yake Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), na akaegemea ushahidi wake katika kauli ya Allaah Subhanahu wa Ta’ala pale Aliposema:


{{Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa kumcha Allaah tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame humo.}} [At-Tawbah: 108]


(Kusudi la 'Siku ya mwanzo' katika Aayahhii, ni siku ile Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipowasili Madiynah).


"Bila shaka kauli ya Imaam Malik ndio inayonasibiana, lakini (Maswahaba kabla yake) walikwishakubaliana kuwa Mwaka wa Kiislam uanzie Mwaka aliohama Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ndani yake (Mwaka wa Al-Hijrah), na wakakubaliana Mwezi wa mwanzo uwe mwezi wa Muharram ili wasibabaike. Wa-Allaahu Ta’ala A’alam”.


Hivi ndivyo alivyomaliza Imaam Al-Haafidh Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah).


Safari za jangwani zilikuwa zikiwatoa jasho majabari na mashujaa wakubwa wa wakati ule wanaosafiri wakiwa katika amani, kwa hivyo munaweza kukisia hatari za namna gani zilizokuwa zikimkabili Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyeondoka akiwa na sahibu yake Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) huku wakiwa wanasakwa na makafiri waliokwishaamua kuwa lazima auliwe, wakatangaza zawadi ya ngamia mia moja kwa yeyote atakayeweza kumkamata Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa hai au amekwishakufa.


Hawezi kuyakisia haya ila yule aliyewahi kuuonja moto wake.


Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kulikata jangwa lile alipokuwa mdogo akiwa amefuatana na mama yake siku ile walipokwenda Madiynah kwa ajili ya kulizuru kaburi la baba yake, kisha akarudi Makkah peke yake kwa sababu mama yake alifariki dunia alipowasili Madiynah. Lakini safari hii Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) analikata tena jangwa hilo hilo akiwa na umri uliopindukia miaka hamsini pamoja na Sahibu yake Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu), si kwa ajili ya matembezi wala kwa ajili ya biashara, bali kwa ajili ya kuuendeleza ujumbe aliokuja nao.


Anasafiri ili aweze kuusimamisha ujumbe huo juu ya ardhi ya Yathrib (Madiynah), na kuiweka mizizi yake hapo baada ya kung'olewa katika mji wa Makkah.


Aliondoka Makkah kuelekea Madiynah akiwa na yakini kupita mtu yeyote yule kuwa Mola wake Atamnusuru na kuidhihirisha dini Yake, na alikuwa na uhakika pia kuwa Mola wake atamrudisha tena Makkah.


Allaah Alikwishamwambia:


{{Na hakika wewe uko mbele ya macho Yetu.}} [Atw-Twuur: 48]


Na Akasema:


{{Hakika Yeye Aliyekulazimisha (kufuata) Qur-aan, kwa yakini Atakurudisha mahali pa kurejea.}} [Al-Qaswasw: 85]


Mwenendo Wa Mitume ('Alayhimus Salaam)


Kutokana na Hijrah hii Mtume wetu mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) atakuwa ametimiza Sunnah ya Mitume wenzake waliomtangulia, kwani Mitume yote ('Alayhimus Salaam) kuanzia Nabii Ibraahiym mpaka kufikia kwa ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), wote waliihama miji yao waliyozaliwa, wakateswa na kusubiri ili wawe mfano mwema kwa watu wao.


Na hii ndiyo maana Waraqah bin Nawfal siku ile alimwambia Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam):


"Yareti ningeliishi mpaka siku ile watu wako watakapokutowa katika nchi yako".

Na Allaah Amesema:


{{Na wale waliokufuru wakawaambia Mitume yao: "Tutakutoeni katika nchi yetu au lazima murudi katika mila yetu.}} [Ibraahiym: 13]


Tofauti Ya Kuhama Kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Na Kuhama Kwa ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘Anhu)


"Inaweza kumpitikia mtu kutaka kufananisha baina ya kuhama kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuhama kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu), akajiuliza:

"Kwa nini ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akahama mchana tena mbele ya watu bila kuogopa, huku akiwabishia makafiri pale alipowaendea na kuwaambia:

‘Zimedhalilika nyuso zenu, zimedhalilika nyuso zenu, yeyote kati yenu anayetaka mamake ampoteze na wanawe wawe mayatima na mkewe awe kizuka, basi na akutane nami nyuma ya bonde hili.’

Wakati Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alihama kwa kificho bila kumjuulisha mtu. Mtu anaweza kujiuliza:

"Hivyo ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) anaweza kuwa shujaa kuliko Mtume?


Jibu lake litakuwa:

"Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) au Muislam yeyote yule, hukmu yao ni tofauti na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwani matendo ya mtu yeyote yule awe ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) au mwengine yanahesabiwa katika dini kuwa ni matendo yake mwenyewe binafsi, na kwamba si hoja inayoweza kusimama katika dini kama yalivyo matendo ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Kwani mtu mwingine asiyekuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) anaweza kutumia njia zozote zile azitakazo anazoziona kuwa ni mnasaba kwake, ama Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yeye matendo yake ni Shari’ah, na hii maana yake ni kuwa matendo yake yote yanayohusiana na dini yanahesabiwa kuwa ni Shari’ah kwetu, na kwa ajili hiyo Mafundisho yake (Sunnah zake) yakawa ni asili ya pili ya Shari’ah, yakiwemo matendo yake, maneno yake, sifa zake na yale yaliyofanywa mbele yake na akayakubali.

Lau kama Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) angefanya kama alivyofanya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu), baadhi ya watu wangedhania kuwa hivyo ndivyo anavyowajibikiwa kila Muislam kufanya, na kwamba haina haja mtu kuchukua tahadhari wala kuogopa pale anapokuwa katika hatari.

Baada Ya Kuhamia Madiynah

Tuliona huko nyuma kuwa mara baada ya kuwasili mjini Madiynah, jambo la mwanzo alilofanya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kufungisha udugu baina ya watu wa Makkah na watu wa Madiynah, na jambo la pili ni kuujenga Msikiti uliokuwa mfano wa Chuo Kikuu kilichokuwa kikifundisha Imani, udugu, umoja, ushujaa, fiqhi pamoja na tabia na mwenendo mwema, na kutokana na hayo Chuo hicho kikaweza kutoa mashujaa walioweza kuzifungua nchi nyingi pamoja na nyoyo nyingi.


 Posted By Posted juu ya Thursday, May 10 @ 22:54:06 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis:
Jinsi Ya Kumfurahisha Mkeo


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa RafikiMada zinazohusiana

Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis

 

EsinIslam The Muslim World Portal For Islamics, News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Quranic Islamic Articles, Radio, Audio Quran, TV Channels, Fatwa Rulings, Muslim News Newspapers Magazines Headlines Articles Forums Schools, Universities, Colleges, Mosques, Qur'an, Hadith, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Fasting Ramadan, Vidoes, Books On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com