Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 
Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 1
 
Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili Imekusanywa Na: Abu Faatwimah
 
Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 1

Kila sifa jema inamstahikia Allaah Aliyetukuka Muumba wa ulimwengu na walimwengu wake, Swalah na Salamu zimfikie kipenzi cha Waislamu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Sahaba zake kiraam (Radhiya Allaahu 'anhum) na kila anaewafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Mwisho.
Shari’ah, amri, makatazo na kanuni ni katika taratibu ambazo jamii haiwezi kiziepuka ikitaka kuwa na uadilifu, amani, usalama na uhuru kwa wana jamii wake.Jamii ni mchanganyiko wa wema, wabaya na kadhalika; hivyo huhitaji utaratibu wa kuwadhibiti, kuwazuia au kurekebisha na kuwatengeneza wale wenye kwenda kinyume na shari’ah ziliopo katika jamii ile; kwa kuwawekea adhabu, faini, fidia na kadhalika; lakini walio wema –raia wema- na wenye kufuata kanuni huwa hawana chao kitu, kwani hawawekewi –tunzo- kwa kufuata au kutunza kwao kanuni zaidi ya kuongezewa ushuru.
Uislamu ni mfumo kamili wa maisha kwa jamii, mfumo wenye kujitegemea usiohitaji mchango wa aina yo yote ile kutoka pahala popote pale katika jambo lolote lile; mfumo huo umekuja na mengi yakiwemo maamrisho na makatazo; shari’ah na kanuni; adhabu na malipo mazuri yasiyobagua baina ya kiongozi na mwenye kuongozwa; mfalme na raia; sharifu na dhaifu; tajiri na maskini; mweusi na mweupe, mwanamke na mwanamume na kadhalika; Qur-aan inasema:
“Na anayefanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini; basi hao wataingia Jannah wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya kokwa ya tende” [An-Nisaa 4: 124]; kwa lengo la kuhakikisha kuwa wote wananufaika katika maisha yao ya duniani; na kwa wale Waumini wa Allaah na Siku ya Qiyaamah kutarajia malipo mema kutoka kwa Mola wao kwa kule kutekeleza kwao Amri Zake na kujikataza na Makatazo Yake bila ya kuendekeza au kufuata matamanio ya nafsi zao; kwa kuelewa na kuwa na yakini kuwa iymaan yao haikamili bila ya kumtii Mola wao na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Amri Zake na kujikatza na Makatazo Yake tena bila ya kuwa na khiari au uchaguzi katika Aliyoyahukumu kama isemavo Qur-aan:
“Haiwi kwa Muumini wa kiume wala Muumini wa kike Anapohukumu Allaah na Mjumbe Wake jambo wakawa wanakhiari –ya kuchagua kinyume cha Alivyohukumu Allaah- katika jambo……” [Al-Ahzaab 33: 36].


Maamrisho na makatazo hayo yamekuja katika Qur-aan tukufu na katika Sunnah sahihi za Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); maamrisho au makatazo hayo huja na kumlenga mkusudiwa awe mwenye hadhi au cheo cha aina yoyote ile na adhabu yake haibagui kwa wenye kwenda kinyume na maamrisho awe sharifu au dhaifu; tajiri au maskini na kadhalika, kwani huko –kubagua kwa kuwaadhibi baadhi na kutokuwadhibu wengine- ni kuangamia kwa jamii kama tunavyoona katika ulimwengu wetu na kama alivyobainisha (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema:
“Kwa hakika waliangamia waliokuwa kabla yenu, wao walikuwa wakitekeleza al-hadd –adhabu- kwa wanyonge na wakiacha kuitekeleza kwa masharifu - waheshimiwa-; naapa kwa Yule Ambae nafsi yangu iko Mikono Mwake lau kama Faatwimah –binti Rassuli Allaahi- angelikuwa amefanya kosa –la kuiba- basi ningelimkata mkono wake.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiri Qur-aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 6319 na 6320; na Muslim, katika Kitabu cha Huduud, mlango wa kumkata -mkono-mwizi sharifu na asiyekuwa sharifu na kukatazwa kushufaia katika Huduud, Hadiyth namba 3202.].
Kauli kama hii na nyingine nyingi zilizojaa katika mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinathibitisha na kuweka bayana kuwa Uislamu si utaratibu wa maisha uliowekwa na serikali/chama/kikundi fulani, bunge/wawakilishi; bali ni Shari’ah/Dini ya Allaah, Shari’ah/Dini ya kweli na ya Haki, kwani hata huyo aliyepewa huo ujumbe ambae ni Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndie Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ndie kiongozi wa juu kabisa wa Uislamu wakati mwingine hujumuishwa na kuingizwa katika maamrisho au makatazo.
Mtume wetu mpenzi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamrishwa na kukatazwa kama ilivyo hali kwa wafuasi wake; kuna amri na makatazo yaliyomlenga yeye pekee yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama pele Allaah Aliposema:
Ee Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe Wake” [Al-Maaidah 5: 67].  
Pia Allaah Anasema:
“Ee Mtume! Mche Allaah wala usiwatii makafiri na wanafiki” [Al-Ahzaab 33: 1].


 Pia Allaah Anasema:
“Ee Mtume! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao…” [Al-Ahzaab 33: 59].  
Pia Allaah Anasema:
“Ee Mtume! Kwa nini unaharamisha Alichokuhalilishia Allaah? Unatafuta kuwaridhisha wake zako…” [At-Tahriym 66: 1].  
Pia Allaah Anasema:
“Wala usimswalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake” [At Tawbah 9: 84].
Wakati mwengine -na ndio kawaida ya Qur-aan- amri na makatazo huja kwa kumjumuisha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumtanguliza mbele ya wafuasi wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama pele Allaah Aliposema:
“Ee Nabii! Mtakapowapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Allaah, Mola wenu. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allaah, msiikiuke…” [Atw-Twalaaq 65: 1].  
Pia Allaah Anasema:
“Haimpasii Mtume na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina, ijapokuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu wa Motoni” [At-Tawbah 9: 113].
Pia Allaah Anasema:
”Allaah Hakujaalia mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala Hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala Hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu hasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Allaah ndiye Anayesema kweli, naye ndiye Anayeongoa Njia. Waiteni kwa –majina ya- baba zao, huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Allaah ...” [Al-Ahzaab: 33: 4-5].
Pia maamrisho au makatazo hayo huja kwa ujumla na kwa makhsusi; kuna maamrisho au makatazo yenye kuwahusu watu wote –Waumini na wasio waumini- kama pale Allaah Anaposema:
“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu Aliyekuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate kuokoka.” [Al-Baqarah 2: 21].  
Pia Allaah Anasema:
“Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shaytwaan…” [Al-Baqarah 2: 168].  
Pia Allaah Anasema:
“Enyi watu! Hakika Ahadi ya Allaah ni ya kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Allaah” [Faatwir 35: 5].
Wakati mwengine maamrisho au makatazo huja kwa kuwahusu waumini pekee -wake kwa waume- kama pale Allaah Anaposema:
“Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za shaytwaan; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.” [Al-Baqarah 2:208].  
Pia Allaah Anasema:
“Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Allaah wala Siku ya Mwisho.….” [Al-Baqarah 2: 264].  
Pia Allaah Anasema:
“Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowapo ushahidi kwa ajili ya Allaah, ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu...” [An-Nisaa 4:135].  
Pia Allaah Anasema:  
“Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa.” [An-Nuur 24:31].  
Pia Allaah Anasema:
“Enyi mlioamini! Jiepusheni sana na dhana, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msipelelezane, na wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Tawwaabur Rahiym.” [Al-Hujuraat 49:12]
Kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mwanamume asitazame utupu wa mwanamume; na wala mwanamke asitazame utupu wa mwanamke; na wala mwanamume asilale na mwanamume mwenziwe katika nguo moja; na wala mwanamke asilale na mwanamke mwenzie katika nguo moja.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Hedhi, mlango wa uharamu wa kutazama sehemu za siri, Hadiyth namba 517; na katika Kitabu cha tafsiyril Qur-aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 5465 na 6361].

Na kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wenye kujifananisha na wanawake na wanawake wenye kujifananisha na wanaume.” na katika riwayah: Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani mukhannithyina -makhanithi- miongoni mwa wanaume na vidumedume miongoni mwa wanawake na akasema: Watoweni katika nyumba zenu...” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Mavazi, mlango wa al-Mutashabbihuuna -wanaume wenye kujishabihisha- na wanawake na al-Mutashabbihaat -wanawake wenye kujishabihisha- na wanaume, Hadiyth namba 5464; na katika Kitabu cha tafsiyril Qur-aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 5465 na 6361].

Pia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mwanamume mwenye kuvaa mavazi ya mwanamke na mwanamke mwenye kuvaa mavazi ya mwanamume” [Imepokelewa na Abu Daawuud, katika Kitabu cha Mavazi, mlango wa katika mavazi ya wanawake, Hadiyth namba 3578; na Ibnu Hibbaan, katika Kitabu cha Al-Hadhr na Al –Ibaahah –yenye kukayazwa na yaliyohalali-, mlango wa Laana, Hadiyth namba 5870].
Ni katika desturi za watu wengi siku hizi kuiga hata jambo lenye kwenda kinyume na mafundisho ya Dini au hata mila na desturi zao; na lenye kufungamana na kuiga ni kujifananisha; hivyo utawaona watu wanafanya kila waliwezalo ikiwemo kutoa fedha kwa lengo la kufikia kuweza kufanana na anayetaka afanane naye iwe kufanana huko katika mavazi au sauti au mapambo au mitindo au hata mwendo na kadhalika.
Kilichojitokeza kwa masikitiko makubwa katika karne hizi ni kuwa si kutaka kufanana tu, bali wengine wamekwenda zaidi ya hilo na kuvuka mipaka kwa kujibadilisha maumbile waliyoumbiwa; kwa njia ya operesheni na kubandikwa sehemu za siri zisizokuwa katika maumbile yao, kwa kisingizio tu hapendi kuwa na maumbile Aliyomuumba nayo Muumba. Haya yote ni haramu na yamelaaniwa; huenda ikiwa chanzo cha mtu kuelekea na kuweza kufikia hayo ni huku kupenda kujifananisha; ambako kumekuwa hakuna mipaka, lau Waislamu tungelijifananisha na Swahaba au Swahabiyyaat (Radhiya Allaahu ‘anhum) au watu wema; badala ya kujifananisha na wasiokuwa wema basi tungelifanikiwa katika mambo ya maisha yetu karibu yote.
Wakati mwengine maamrisho au makatazo huwa maalumu kwa waumini wa kiume pekee; kama pale Allaah Anaposema:
“Enyi mlioamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili muwapokonye baadhi ya mlivyo wapa” [An-Nisaa 4:19].  
Pia Allaah Anasema:
“Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao. Hakika Allaah ni Khabiyru kwa wayafanyayo.” [An-Nuur 24:30].
Pia Allaah Anasema:
“Wala msiwaoe mushrikaat –washirikina- mpaka waamini. Na Mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Wala msiwaoze (mabinti zenu) mushrikiyna –washirikina- mpaka waamini. Na Mtumwa Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni. Hao wanaitia kwenye Moto, na Allaah Anaitia kwenye Jannah na maghafira kwa idhini Yake...” [Al-Baqarah 2: 221].  
Pia Allaah Anasema:
“Na mtakapowataliki wanawake, wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa ma’aruuf –wema- au waachilieni kwa maarufi. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake. Wala msizichukuwe Aayah za Allaah kwa kuzifanyia istihzai/maskhara…” [Al-Baqarah 2:231].  
Pia Allaah Anasema:  
“Na mtakapo wataliki wanawake, wakamaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao endapo baina yao wamepatana kwa wema...” [Al-Baqarah 2:232].
Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) amesema kuwa:  
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza Shighaar: Shighaar -ndoa ya kubadilishana- ni kwa mwanamume kumuozesha binti/dada yake  kwa –sharti la- huyo mwanamume mwengine -aliyeozeshwa- amuozesha yeye binti/dada yake pia, bila ya kuwepo Swadaqah -mahari- baina yao” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha tafsiyril Qur-aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 4747; na Muslim, katika Kitabu cha Ndoa, mlango wa kuharamishwa kwa ndoa ya Shighaar na kubatilika kwake, Hadiyth namba 2545.].
Kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Hakika katika watu wenye shari kupita wote -watakaokuwa katika hali mbaya- kabisa mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah: Mwanamume anaekwenda kwa mke wake –kuingiliana- kisha akatangaza siri ya mkewe” [Imepokelewa na Muslim, kitabu cha Nikaah, mlango wa uharamu wa kutangaza siri za mwanamke Hadiyth namba 2605 na namba 2606].
Imaam an-Nawawiy amesema: Katika Hadiyth hii kumethibiti uharamu wa mwanamume kutangaza yanayotokea –katika tendo la ndoa- baina yake na mkewe, na kuelezea au kutoa wasifu yaliyotokea kwa undani, na yaliyotokea kutoka kwa mwanamke katika hilo tendo lao la ndoa miongoni mwa maneno, vitendo, sauti, na kadhalika.
Ndugu yangu katika Uislamu makemeo haya hayamuhusu mwanamume pekee, bali pia yanamuhusu mwanamke; wakati wo wote atapokutana na kustarehe na mumewe kisha akatangaza siri ya makutano yao huwa anaingia katika makemeo; kwa ujumla ni kuwa wote wanatarajiwa kuhifadhi siri za makutano yao na kwa kila mmoja kuhifadhi heshima ya mwenzake kwa watu wa nje.
Wakati mwengine maamrisho au makatazo huwa maalumu kwa waumini wa kike pekee –na hili ndio kusudio la waraka wetu huu- kama pale Allaah Anasema:
“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasionyeshe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenzao, au iliyo wamiliki mikono yao ya kiume, au wafuwasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yaliyo husu uke. Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyo yaficha...” [An-Nuur 24:31].  
Pia Allaah Anasema:
“Na wanawake walioachwa wangoje kwa nafsi zao -peke yao- mpaka qurui -twahara au hedhi- tatu zipite. Wala si halali kwao –haiwajuzii- kuficha Alichoumba Allaah katika matumbo yao, ikiwa wanamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki ya kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya sulhu...” [Al-Baqarah 2: 228].
Kuna wakati maamrisho au makatazo huja makhususi kwa vijana; kama pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
“Enyi kundi la vijana atakayekuwa na uwezo wa kuoa miongoni mwenu basi na aoe, kwani huko kuoa kutampelekea kuinamisha macho yake na kuhifadhi tupu yake. Ikiwa hana uwezo wa kuoa basi na afunge kwani hiyo ni kinga kwake. [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha an nikaah -ndoa–, mlango wa asiye kuwa na uwezo wa kuoa basi afunge, Hadiyth namba 4705].
Na kwa kuwa Uislamu ni Dini ya Muumba wa walimwengu wote, hivyo basi maamrisho au makatazo yake wakati mwingine huja hata kwa waliopewa vitabu kabla ya Qur-aan na wasiopewa vitabu, jambo lenye kubainisha uhakika na ukweli kuwa Dini hii ni Dini yenye kumheshimu na kumthamini kila kiumbe hata awe na kiburi, inadi na ukaidi wa aina yake pekee; kama pale Allaah Anaposema:
“Enyi wana wa Israaili! Kumbukeni Neema Yangu Niliyokuneemesheni, na timizeni Ahadi Yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na Niogopeni Mimi tu. Na aminini Niliyoyateremsha ambayo yanasadikisha mliyonayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze Aayah Zangu kwa thamani ndogo. Na Niogopeni Mimi tu. Wala msichanganye kweli na uongo na mkaificha kweli nanyi mnajua. Na simamisheni Swalah, na toeni Zakaah, na rukuuni –inameni- pamoja na wanao rukuu” [Al-Baqarah 2: 40-43].  
Pia Allaah Anasema:
“Enyi mlio pewa Kitabu! Aminini tuliyo yateremsha yenye kusadikisha yale mliyo nayo, kabla Hatujazigeuza nyuso Tukazipeleka kisogoni, au Tukawalaani kama Tulivyo walaani watu wa Jumaamosi…” [An-Nisaa 4: 47].
Pia Allaah Anasema:
“Enyi watu wa Kitabu! Msipindukie mipaka katika Dini yenu, wala msimseme Allaah ila kwa lilio kweli. Hakika Masiyhi ‘Iysaa mwana wa Maryam ni Mtume wa Allaah, na neno Lake tu Alilopelekea Maryam, na ni Roho iliyotoka Kwake. Basi Muaminini Allaah na Mitume Yake. Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Allaah ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana.” [An-Nisaa 4: 171].
Katika waraka huu tumejaribu kukusanya MAKATAZO YA KISHARI’AH YENYE KUWAHUSU WAUMINI WA KIKE PEKEE ijapokuwa katika hayo kuna yanayowagusa pia Waumini wa kiume; lakini lengo hasa ni kukusanya makatazo yenye kuwahusu dada zetu katika Iymaan; kwani wengi wao huenda wakawa hawaelewi kuwa kuna makatazo na yenye makemeo makali, na pia kwa kuwa wengi katika dada zetu huwa si wenye hima wala hamu ya kutaka kuelewa mafundisho ya Dini yao wachilia mbali kuelewa maamrisho au makatazo ya Mola.
Twamuomba Allaah Aujaalie waraka huu uwe wenye manufaa kwa dada zetu na Awalipe kila la kheri wote walioandika kuhusu mada kama hii jambo lililosaidia na kupelekea kuweza kuyakusanya makatazo haya kwa wepesi; pia twamuomba ar-Rahmaan Awafunue macho, akili na nyoyo kila ataejaaliwa kuusoma na kuwafikishia wengine ujumbe unaotarajiwa au uliokusudiwa na waraka huu.
Allaah na Mjumbe wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuhadharisha na kwenda kinyume na Hukumu za Allaah au za Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); Allaah Amesema:
“Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake, usije ukawapata msiba au ikawapata adhabu iumizayo.” [An-Nuur 24: 63].  
Pia Allaah Anasema:
“Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho” [Al-Hashr 59: 7].


 Posted By Posted juu ya Friday, June 29 @ 17:26:36 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili:
Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa RafikiMada zinazohusiana

Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili

 

EsinIslam The Muslim World Portal For Islamics, News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Quranic Islamic Articles, Radio, Audio Quran, TV Channels, Fatwa Rulings, Muslim News Newspapers Magazines Headlines Articles Forums Schools, Universities, Colleges, Mosques, Qur'an, Hadith, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Fasting Ramadan, Vidoes, Books On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com