Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 


Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 4
 
Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili Imekusanywa Na: Abu Faatwimah


Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 4

Katazo La Kutokuwa Na Shukurani [Kukanusha] Ihsaan


Huu dada yangu Muislamu ni uwanja mwingine wenye hatari kubwa, na kwa bahati mbaya ni kuwa wengi miongoni mwa wanawake kwa masikitiko makubwa wameuingia na kuamua kuwa ni katika sehemu zao za kuishi na kutafuta kuridhiwa au kupewa ruhusa ya kwenda watakapo hata kama ni kwenye maasi na pasipo mridhia Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Wanawake wengi siku hizi wanapotaka jambo ambalo wanaelewa kuwa mume hatoridhika nalo au halipendi au hata wakati mwingine hayuko tayari nalo kwa sababu moja au nyingine au hata kama hataki ni haki yake; huwa silaha yao kubwa ya kutaka wakubaliwe walitakako kusema usemi wao mashuhuri na wenye kupendeza katika midomo yao: Sikupata kuiona kheri hata siku moja kutokana nawe; yote kwa kuwa amekataliwa siku hiyo alitakalo au amezuiliwa kufanya alitakalo au kwenda atakapo.
Mke ni mwepesi wa kusahau au kujisahaulisha kwa alitakalo na kwa wakati autakao na wakati huo huo ni mwepesi kukumbuka kila alitakalo hasa hasa yasiyokuwa na faida wala maana yoyote katika Dini wala dunia yake.
Mke hununa na kuusawijisha uso wake kwa kuwa tu mume amemkatalia jambo au amemueleza jambo ambalo mke hayuko tayari au hataki kulisikia kwa kuwa ana lake ameliweka na analiona ndio sawa; pengine keshapanga na shoga zake walifanye au wende, hivyo huona kuwa shoga zake watamuona kuwa hana kauli mbele ya mumewe au hapendwi au hana ujanja na mbinu za kumpelekea mume amkubalie na kumridhia kwa alitakalo; hivyo hugeuka na kuwa kama asiyekuwa na akili yake wakati huo na kutoa kauli kama hizo na nyingine mbaya zisizokubalika, kama vile mke kumwambia mumewe unanihangaisha tu kwa kuwa amemtaka huduma na kadhalika; kauli zenye kumpelekea mume kufikia wakati mwingine kujiuliza masuala mengi tu likiwemo hili, hivyo ni kweli hakuwahi kumtendea jema mkewe hata mara moja katika miaka yao yote waliyokaa kama mke na mume?! Hivyo ni kweli kwa kumtaka mkewe amtekelezee huduma fulani [kama vile kumtayarishia chakula kumsogezea maji] ni kweli huwa anamuhangaisha?
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nimeonyeshwa Moto, tahamaki wengi watu [wakaazi] wake ni wanawake; wanakanusha; pakasemwa: “Wanamkanusha Allaah!” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Wanakanusha waume zao na wanakanusha ihsaan [wanazofanyiwa na waume zao]; lau ukimfanyia ihsaan mmoja kati yao dahr [milele], kisha akaja akaona kitu kidogo kwako, basi husema: Sikupata kuiona kheri yoyote katu [hata siku moja] kutokana nawe” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Iymaan, mlango wa Kufraanil ‘Ashiyrah na kufr duwna kufr, Hadiyth namba 28].
Na kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba nilishuhudia Swalaah pamoja na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya ‘Iyd; alianza (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swalaah kabla ya khutbah, kisha akasimama huku akimtegemea Bilaal (Radhiya Allahu ‘anhu); hadi alipowaendea wanawake akawawaidhi, akawakumbusha, na akawaamrisha kuwa na taqwa ya Allaah; akasema: “Toeni Swadaqah, akataja mambo katika mambo ya Jahannam [ikiwemo kuwa wakaazi wake wengi ni wanawake], akasimama mwanamke... akasema: Kwa sababu gani ee Mjumbe wa Allaah? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Kwa sababu nyinyi mnaeneza malalamiko na laana; na mnakanusha ‘ashiyrah” [Imepokelewa na Maalik, katika Muwattwaa, Kitabu cha Swalaah ya Kusuwf, mlango wa al ‘amali katika Swalaah ya Kusuwf, Hadiyth namba 442].
Dada yangu Muislamu kutokuwa na shukurani au kukanusha ihsaan ndio kukanusha neema kwenyewe huko; nako ni kukanusha yale yote aliyokutendea na kukutekelezea mumeo yakiwemo matumizi ya kila siku na kadhalika.

Katazo La Kukaa Faragha Na Asiye Kuwa Maharim
Uislamu unapendelea mahusiano yoyote yale baina ya mwanamme na mwanamke wenye kuweza kuoana yawe na mipaka na udhibiti wenye kuchunga heshima na kujiweka mbali na yenye kuweza kutokea ambayo ni haramu pindi tu wawili hawa wenye jinsi tofauti na wenye maumbile yaliyopambiwa na kupandikizwa kupenda matamanio ya kila mmoja kutaka kuelemea kwa jinsi iliyo tofauti na yake watapokuwa faragha; Allaah Anasema:
“Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Allaah ndio kwenye marejeo mema” [Aal-‘Imraan 3: 14].
Ni katika yenye kupendwa na wengi ukaaji wa faragha kwa wawili wenye jinsiya tofauti na wenye uwezo wa kuoana huku wakielewa fika kuwa ukaaji wao huo unaweza kuwapelekea kutenda kila lililokatazwa na Allaah na Mtumewe litalo wapelekea kufikia kuwa wenye kustahiki adhabu ilyowekwa na Allaah hapa duniani au huko Aakhirah.
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba alimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akihutubia kwa kusema: “Asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa [mwanamke huyo] awe na maharimu wake...”  [Imepokelewa na na Al-Bukhaariy, kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, Suwrat Qul A’uwdhu Birabbil Falaq, Hadiyth namba 4860; na Muslim, kitabu Kitabu cha Hajj, mlango wa Safari ya mwanamke pamoja na Maharimu wake kwenda Hajj, Hadiyth namba 2399].
Na kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asiingie katika Hammaam [mahodhi ya kuogea] isipokuwa awe amevaa miizar [shuka]; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asimuingize khaliylah wake [mkewe] katika Hammaam; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae kwenye meza yenye kunywewa ulevi; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae faragha [peke yake] na mwanamke asiyekuwa na maharimu wake pamoja naye, kwani watatu wao huwa shaytwaan” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad, Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, iliyobaki Musnad Mukthiriyna katika Swahaba (Radhiya Allahu ‘anhum), Hadiyth namba 14356].
Na katika desturi yenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hii desturi ya watu kukaa faragha na shemeji zao; aliulizwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu shemeji na majibu yalikuwa kwamba shemeji ndio hasa hatari [mauti] kubwa kwa kukaa faragha na mke wa ndugu yake, kwani yeye huwa na nafasi kubwa asiyokuwa nayo mtu mwingine wa nje asiyekuwa shemeji; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:”Tahadharini kuwaingilia [kuingia majumbani mwao] wanawake; akasema mtu mmoja miongoni mwa Answaar: Ee Mjumbe wa Allaah, vipi kuhusu Hamuu [shemeji]?! Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hamuu ni mauti. [Hamuu” Katika hali hii kunamaanishwa ndugu za mume (wa kiume). Haafidh Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) kasema: "Atw-Twabariy kasema: "Maana yake ni kwamba kuwepo kwa mwanamke katika nyumba au chumba na kaka wa mume au binamu ya mke wawili peke yao ni kama kifo, kwa kuwa Waarabu huzoea kuita kila kitu chenye hatari “kifo”]. [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Ndoa, mlango asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa awepo maharimu, Hadiyth namba 4859; na Muslim, katika Kitabu cha Salamu, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4044.].
Ni vyema ieleweka kuwa shemeji wa mtu, binamu ya mke wa mtu si miongoni mwa Maharimu zake kwa kuwa wao wanaweza kumuoa hali kadhalika wengi wa jamaa za mume si Maharimu wa mke.
Pia katika kawaida zenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hii desturi ya watu kulala kwenye nyumba za wanawake wajane; kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asilale mwanamme yeyote yule kwa mwanamke mjane (na katika Riwaayah): [katika nyumba] isipokuwa awe mwenye kumuoa au maharimu wake.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Salaam, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4043.].
Na katika mazoea na mila walizonazo watu zenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni haya mazoea ya kwenda au kuingia kwenye nyumba za watu ambao waume hawapo na kukaa kupiga domo [soga] au kutoa stori za kweli na uongo na mke wa mtu.
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba: “Watu kutoka bani Haashim waliingia kwenye nyumba ya Asmaa bint ‘Umays; basi akaingia Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu)... alipowaona hao watu hakufurahi [alichukizwa], akamueleza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: Sikuona isipokwa kheri. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika Allaah Amemuepusha [Asmaa] na hayo. Kisha akasimama Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye minbar akasema: Asiingie mwanamme yeyote yule baada ya siku ya leo kwa maghiybah [mwanamke aliyekuwa mumewe hayupo] isipokuwa awe pamoja nae mwanamme mwingine au wanaume wawili.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Salaam, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4046.].
Hadiyth hizi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ziko wazi katika kutufahamisha kuwa ni haramu kukaa faragha mwanamme na mwanamke wenye uwezo wa kuoana na kwenda au kuingia katika nyumba ambayo mume hayupo.
Dada yangu Muislamu huu pia ni uwanja mwengine wenye kufanywa mwepesi kufikiwa na kila mtu kwa madai tofauti yakiwemo ya kuwa ni mwenzangu katika kazi, au ni mwanafunzi mwenzangu, au mengineyo.
Hivyo ni wajibu kwa mwanamke Swaalihah (mwema) kutomruhusu kuingia katika nyumba yake isipokuwa yule anayemridhia mumewe wakati yupo huyo mume, na atakaporuhusiwa iwe kukaa kwake kwa vidhibiti vya kishari’ah; ikiwemo kutokaa naye faragha au kukaa naye bila ya kuvaa hijabu ya kishari’ah; au bila ya haja yenye kukubalika; hivyo haitakiwi kukaa pamoja na asiyekuwa maharimu yake [hata akiwepo mumewe au akiwepo mmoja kati ya maharimu zake] kwa kuzungumza tu na kuhadithiana yaliyopo au habari zilizopo.
Kinachojitokeza siku hizi [ambacho hakikubaliki pia] ni kwa wanawake kukaa faragha na wasiokuwa maharimu zao kwa kisingizio kuwa wako watoto wao wa kiume wadogo wadogo [wasio kuwa baleghe], hivyo hudai kuwa faragha imetoweka kwa kuwepo hao watoto wake wadogo; hii si sahihi, kwani kuwepo kwa mtoto mdogo na kutokuwepo ni sawa, kwani hakuna anayewaonea hayaa kwa sababu ya umri wao mdogo; na katika yanayofanywa pia ambayo yanakwenda kinyume na mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa miongoni mwa jumla ya yasiyokubalika katika Uislamu ambayo ni miongoni mwa namna fulani ya kukaa faragha kwa mwanamke na asiyekuwa maharimu wake, ni huku kwa baadhi ya watu [wenye kujiita au kuitwa mustaadh] kwenda kuwaombea [kuwazinguwa] wasichana wanaotarajiwa kuolewa au kuwasomea mabibi arusi huku wakiwa wamepambika kisawa sawa, ukaaji wa aina hii kwa hali yoyote ile ikiwa hakuna maharamu ni ukaaji faragha wa wanaume wengi na mwanamke mmoja pia hakukubaliki.
Ama mwanamme akimkuta mwanamke aliyepotea njia, itajuzu kwake kufuatana naye kwa vidhibiti vya kishari’ah, miongoni mwake ni kwa yule mwanamke kuwa nyuma ya yule mwanamme katika kwenda kwao na si kwenda sambamba au bega kwa bega huku wakizungumza na kucheka kama mke na mumewe.
Katazo La Kusalimiana Na Wanaume Kwa Kuwapa Mikono
Kama ilivyoeleweka kuwa si kila mtu anaruhusiwa na kukubaliwa kusalimia na kupeana mkono na Malkia; basi hivyo hivyo kwa mwanamke Muislamu ni malkia mwenye hadhi yake aliyopewa na Muumba wake, hadhi yenye kupita ile aliyojipandikiza nayo Malkia yeyote yule katika dunia; hivyo basi si kila mwanamme huruhusiwa kuugusa mkono wake na yeye mwanamke Muislamu asiwe wa kunyanyua na kunyoosha mkono wake wenye hadhi ya aina yake na kumnyooshea kila mwanamme.
Uislamu umeweka kanuni ya uharamu kwa mwanamme kuugusa mwili wa mwanamke na kinyume chake; ikiwemo mikono yake kwa kisingizio cha kuamkiana.
Kutoka kwa Ma’qal bin Yassaar (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema: Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mmoja wenu kutongwa [kudungwa] katika kichwa chake (na katika Riwaayah: (cha mwanamme) kwa makhiytt [msumari au sindano] ya chuma ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke asiyekuwa halali kwake.” [Imepokelewa na Atw-Twabaraaniyy, baqiyyatul Miym, Hadiyth namba 16916].
Kutoka kwa Ummul Muuminiyna ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) amesema kwamba: “Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akichukuwa [akikubali bila kushika mikono ya wanawake] Bay‘ah ya wanawake kwa matamshi [maneno] tu kwa Aayah hii: (“Ee Nabii! Watakapokujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Allaah na chochote, wala hawataiba,…” [Al-Mumtahinah 60: 12]); ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) akasema: Haukuwahi kugusa mkono wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mkono wa mwanamke yeyote yule isipokuwa mwanamke aliye chini ya milki yake. (Na katika Riwaayah: “Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hakika mimi sisalimiani na wanawake kwa kupeana nao mkono).” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suwrat Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 4907 na 6703; na Muslim, katika Kitabu cha Al-Imaarah, mlango wa namna ya Bay’ah ya wanawake, Hadiyth namba 3476 na 3477; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha Swalaah, milango ya nyakati za Swalaah, Hadiyth namba 2870].
Na kutoka kwa Umaymah bint Raqiyqah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) amesema kwamba nilikwenda kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikiwa pamoja na wanawake wenzangu tukambay’i Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya Uislamu; tukasema: “Ee Mjumbe wa Allaah! Tunakuaahidi kuwa hatutomshirikisha Allaah na kitu chochote, na wala hatutoiba, na wala hatutozini, na wala hatutoua watoto wetu, na wala hatutoleta uzushi tunaozusha tu wenyewe baina ya mikono na miguu yetu, na wala hatutokuasi katika ma’aruwf; basi Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Katika muyawezayo na msiyoyaweza.  Akasema: Wanawake wakasema: Allaah na Mjumbe Wake ni Ar-hamu kuliko nasfi zetu; njoo tukuahadi ee Mjumbe wa Allaah, [wakitaka akamate mikono yao kama ishara ya utii]; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hakika mimi sigusi mikono wanawake, kauli yangu kwa wanawake mia ni kama kauli yangu kwa mwanamke mmoja, au mfano wa kauli yangu kwa mwanamke mmoja.” [Imepokelewa na Maalik, katika Muwattwaa, Riwaayah ya Yahya Al-Laythiy, katika Kitabu cha Bay’ah, Hadiyth namba 1781; na Ahmad, katika Musnad, Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad ya Wanawake (Radhiya Allahu ‘anhuna), Hadiyth namba 26383 na 26384; na At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Ijumaa, milango ya Safari, Hadiyth namba 1522].
Hadiyth hizi dada yangu Muislamu zinathibitisha na kuweka wazi kuwa haijuzu kwa mwanamke Muislamu kusalimiana kwa kupeana mikono na mwanamme yeyote yule asiyekuwa maharimu yake, kwani kugusa ni katika vitangulizi ya faahishah [zinaa], na kama ilivyothibiti kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ameandikiwa mwanaadamu sehemu yake katika zinaa [kuzini]; hakuna njia ya kuiepuka; macho mawili yanazini [zinaa] zinaa yake ni kutazama, masikio mawili yanazini [zinaa] yake ni kusikiliza, na ulimi unazini [zinaa] yake ni kunena, na mkono unazini [zinaa] yake ni kugusa, na mguu unazini [zinaa] yake ni hatua zake, na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha (hutenda) au kukadhibisha [huacha].” [Imepokelewa Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suwrat Qul A’wudhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 6152; na Muslim, katika Kitabu cha Qadar, mlango wa imeandikwa juu ya mwanaadam sehemu yake katika zinaa, Hadiyth namba 4808 na namba 4809].
Kinachojitokeza siku hizi [ambacho hakikubaliki kabisa katika Uislamu] katika furaha au msiba ni kwa mwanamke kukumbatiana au kubusiana na wasiokuwa maharimu zao na wakati mwengine haya hutokezea mbele ya waume zao au kwa ruhusa ya wamume zao, kwani  na yeye mume hujipatia fursa ya kumbusu au kumkumbatia mke wa mtu mbele ya mkewe kwa kisingizio kuwa ni tamaduni na njia za kisasa za kimaendeleo za kufikisha ujumbe wa kusalimiana na kuamkiana zenye kuonyesha na kuthibitisha upendo na urafiki wa hali ya juu.
Dada yangu Muislamu ni vyema uelewe kuwa haya yote hayakubaliki katika Dini unayoifuata kwa ridhaa yako bali yamekatazwa na yote yale yenye kutangazwa na kuenezwa au kuonekana na wenye kudai kuwa ni wenye kutetea haki za wanawake au maendeleo ya wanawake na kuwa kuamkiana au kusalimia kwa kupeana mikono au kukumbatiana na kubusiana baina ya mwanamke na mwanamme asiyekuwa maharimu yake ni katika alama za urafiki na maendeleo na kuwa si kweli kuwa kutawapelekea kufikia kwenye faahishah; madai yao haya na mengine yote ni katika madai ya uongo na yenye lengo la kupotosha kwani hayana msingi wala dalili yoyote ile kutoka katika Qur-aan au Sunnah; hivyo dada yangu Muislamu elewa na kuwa na yakini kuwa mafundisho ya Uislamu yako hapa kwa lengo la kukutunza, kukuhifadhi, kukuenzi na kukupa hadhi ya aina yake pekee, na moja katika mafunzo hayo ni kutopeana mikono na mwanamme yeyote asiyekuwa maharimu yako ni mafundisho sahihi yaliyothibiti katika Sunnah za Mtume wako Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Katazo La Kusafiri Bila Maharimu
Mwanamke Muumini na Swaalihah haimpasi kwenda safari bila ya Maharimu wake kuwa pamoja naye hata ikiwa safari yenyewe ni ya kutekeleza ibada kama vile ibada ya Hijjah achilia mbali safari ya kutembea au kufanya biashara, kutalii na kadhalika.  Safari ni safari iwe wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) au wakati huu wa sayansi na ufundi wa hali ya juu; na iwe kwa chombo chochote kile; iwe kwa gari, treni, meli, ndege na kadhalika; bila ya shaka yoyote ile itakuwa ina mengi ndani yake baadhi yake ni ya hatari na mengine ni ya kashifa, fedheha na dhambi kuyaeleza.

Hekima ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumkataza mwanamke kusafiri peke yake bila ya kuwa na maharimu wake ni ya aina yake pekee, hivyo inawajibika kutekelezwa na kufuatwa na huko ndiko kumtii Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenyewe, lengo au sababu yake iwe inaeleweka au haieleweki kwa kila mwenye macho, akili na uume kamili [si dayuwth: mwanamme dhaifu asiyejiheshimu na hajali kuhusu tabia chafu ama mavazi mabaya ya wanawake waliko chini yake] na kwa kila mwenye kupenda kuwa miongoni mwa wale wataoingia katika Kauli Yake Allaah:
“Mwenye kumtii Mtume basi atakuwa amemtii Allaah.” [An-Nisaa 4: 80].
Na wala si kuwa miongoni mwa wale watoingia katika Kauli Yake Allaah:
“Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake; isije ikawapata fitnah au [ikawapata] adhabu iumizayo” [An-Nuwr 24: 63].
Katika hali ya kawaida tu achilia mbali safari mwanamke huhitaji wa kumsaidia, kumshauri na kubwa kumhurumia kwa anayokutana nayo; na hakuna Arhamu na mwenye huruma na kuwahurumia wanawake zaidi ya Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); kwani Allaah ni Arhamu kwa waja Wake kuliko mama kwa mtoto wake, na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutumwa isipokuwa awe Rahmah kwa viumbe vyote wakiwemo wanawake; Allaah Anasema:
“Nasi Hatukukutuma ila ni Rahmah kwa viumbe wote.“ [Al-Anbiyaa 21: 107].
Aliyetumwa kuwa Rahmah kwa viumbe amemkataza mwanamke mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kusafiri bila ya Maharimu wake.
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asisafiri mwanamke isipokuwa awe pamoja nae maharimu wake, na wala asiingie (katika Riwaayah: Asikae faragha) mwanamme kwa mwanamke isipokuwa awe na maharimu wake.” Mtu mmoja akauliza: ee Mjumbe wa Allaah, mimi natarajia kutoka katika jeshi [kwenda vitani] kadhaa wa kadhaa, na mke wangu anatarajia kwenda Hijjah?” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akamwambia: Nenda ukahiji pamoja na mkeo.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na malipo ya kiwindo, mlango wa Hajj ya wanawake, Hadiyth namba 1739; na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu wake kwenda Hajj, Hadiyth namba 2801].
Na kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kusafiri safari ya [katika Riwaayah: masafa ya siku mbili] siku tatu na kuendelea, isipokuwa awe pamoja nae baba yake, au mtoto wake [aliye baleghe] au mume wake, au ndugu/kaka yake au katika maharimu wake.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na malipo ya kiwindo, mlango wa Hajj ya wanawake, Hadiyth namba 1741; na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu kwenda Hajj, Hadiyth namba 2398 na lafdhi ni lake].
Na kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asisafiri mwanamke (na katika Riwayah): zaidi ya masiku tatu [siku tatu] isipokuwa awe pamoja na maharimu.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu kwenda Hajj, Hadiyth namba 2398 na namba 2393].

Katazo La Kuwatazama Wanaume


Allaah Amewaamrisha wanawake kuinamisha macho yao na wasiwaangalie wanaume wasio kuwa maharimu zao; Allaah Amesema: “Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao.” [An-Nuwr 24: 31].
Imaam Ibn Kathiyr katika tafsiyr ya Aayah hii amesema: “Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao.” kwa yale yote Aliyoyaharamisha Allaah kutazamwa na wanawake isipokuwa waume zao; ndio Ma’ulamaa wengi wakasema kuwa: Asili ni kuwa haijuzu kwa mwanamke kuwatazama wanaume wasiokuwa maharimu zake iwe kwa matamanio au bila ya matamanio.
Na sababu ya kukatazwa kutazama, ni kwa kuwa wanawake kuwatazama wanaume au wanaume kuwatazama wanawake ni katika vitangulizi vya zinaa, na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa kutazama ni katika zinaa ya macho kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) iliyotangulia.
Hivyo basi ni wajibu juu ya kila mwanamke Muislamu kulihifadhi jicho lake na kutazama wanaume wasiokuwa maharimu zake, na kutarajia malipo kwa Allaah kwani hilo bora na heri kwake katika uhai huu wa dunia na huko Aakhirah.


 Posted By Posted juu ya Friday, June 29 @ 17:39:00 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili:
Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa Rafiki





Mada zinazohusiana

Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili

 

Ẹsin Islam الدين الإسلامي Religion of Islam Addinin Musulunci Agama Islam Religión del Islam 伊斯兰教 Dini ya Kiislamu Религия Ислам Religião do Islã イスラム教 Esin Islam 이슬람의 종교 Portal African Muslim Website - Arabic English African Islamic Website For World News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Articles, Radio, Audio, Video, Quran, Hadith, TV Channels, Fatwas, Muslim News, Newspapers, Magazines Headlines, Forums, College, Schools, Universities, Mosques, Quranic, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Ramadan, Vidoes, Books, Fasting, PDFs On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com