Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 


Makatazo Ya Kishari'ah Kwa Wanawake - 5
 
Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili Imekusanywa Na: Abu Faatwimah
Makatazo Ya Kishari'ah Kwa Wanawake - 5

Katazo La Kumsifia Mwanamke Wa Nje Kwa Mumewe
Tabia ya kupenda kuelezea, kusifia na kuhadithia kila kitu ni moja kati ya tabia na desturi walizonazo wanawake wengi; hivyo basi tabia hiyo wakati mwingine huwapelekea kujisahau na kuanza kuelezea au kutoa wasifu wa wanawake wenziwao si kwa mashoga zao tu, bali hata kwa waume zao pia, wakijisahau kuwa jambo kama hilo ni katika yeye kupelekea kushitua na kuamsha hisia fulani kwa waume zao na kusababisha mengi katika akili, mwili na mioyo yao.



Ni katika kawaida za wanaume mara zote kuelemea kutaka au kutafuta mwanamke aliyesifiwa; iwe kasifiwa macho yake, au sura yake, au sauti yake, au mwendo wake, au mitindo ya mavazi yake, au mitindo ya nywele zake na kadhalika; kwani huenda wasifu wa uzuri wa umbo na mengineyo yakawa sababu tosha kwa waume kufikiria na kutamani kukutana na huyo aliyesifiwa au kufanya juu chini na kila waliwezalo wapate japo angalau basi kumuona tu huyo msifiwa, na huku ni kuzini kwa macho.
Wanawake wengi siku hizi kwa sababu moja au nyingine huwa hawako tayari kutoa wasifu wa wanawake wenziwao si kwa mashoga zao tu bali hata kwa waume zao, lakini huwa wako tayari bila ya kujijuwa kutoa wasifu wa wanawake wenziwao kwa waume zao kwa njia zenye kudaiwa kuwa zinakwenda na wakati, kwa kuweka video/cd za shughuli zenye kuwajumuisha wanawake wenye kujipamba au kuimba au kucheza kwa kujishauwa shauwa, na wakati mwingi wanawake hao huwa wenye kuvaa mavazi ya kimaajabu katika maajabu ya dunia, si za haramu tu, bali zisizoweza kuelezeka wala kuhadithika; kwani hazina hadhi wala sifa za kustahiki kuvaliwa na wenye kumwamini Allaah na Siku ya Qiyamaah, wachilia mbali kutizamwa kwa lengo la kununuliwa au kuuzwa na wenye kutakiwa kujifananisha na wake za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaabiyyat [Swahaba wa kike, Radhiya Allaahu ‘anhunna].
Na katika yenye kujumuisha mke kumsifia mumewe wanawake ni huku kuangalia au kutazama Tv pamoja na waume zao; video au filamu zenye kuonyesha wanawake wakiwa kwenye matangazo yawe ya biashara au mengineyo, au kusoma taarifa za habari, au mashindano ya mavazi au mashindano ya wanaodaiwa kuwa ni mrembo/mzuri wa dunia [hili ni baya zaidi kwani hujumuisha zinaa ya macho, masikio na pia wakati mwingine kuelekea katika kusadikishwa au kukadhibishwa na sehemu za siri za mume]. 

Wakati mwingi huyo mke huwa anatoa ufafanuzi na maelezo ya kina, na ya kuvutia na kupamba kwa kila mzuri na vazi lake anaeonyeshwa au kuonekana; hali hii haina tofauti na hali ya kumsifia mwanamke kwa mume kama vile anamuona inayokatazwa; bali hali hii huwa na athari zaidi kwa mume, kwani huwa anamuona na kumsikia na kumhisia vile anavyojishaua shaua na kujichezesha chezesha kunako mvutia zaidi kila mwanamume kamili; ndio akakatazwa mwanamke kutoa wasifu wa mwanamke mwenzake aliyechanganyika nae kwa mumewe iwe kwa hali hii au nyingine, na ndio kukakatazwa kwa wanaume pia kuangalia wanawake iwe katika tv au video au cd au hata barabarani na kadhalika, kama ilivyothibiti katika hadiythi ya Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Asichanganyike mwanamke na mwanamke kisha akaja kumsifia mumewe [akatoa wasifu wa huyo mwanamke] kama kwamba anamuona”[Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiri Qur aan, Suuratul Qul A’uwudhu Birabbil Falaq, Hadiyth namba 4867 na 4868; na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Adabu, mlango wa ukaraha wa kuchanganyika wanaume na wanaume na wanawake na wanawake.., Hadiyth namba 2736].
Katazo la Kutoka Nyumbani bila ya haja (dharura)


Allaah Amesema kuwaambia wake za Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wanaingia katika hilo wanawake Waumini na Waislamu pia, kwa kuwa wao hawana riwaza nzuri wala kigezo chema cha kukiiga na kujinasibu nacho isipokuwa wake wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au Swahaabiyyat [Radhiya Allaahu ‘anhunna], hivyo wanawake Waislamu wote wanatakiwa na wanatarajiwa kuelewa kuwa hawana wa kuwaiga wala wa kujifananisha nao isipokuwa hao wakeze Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na sio wingine, Allaah Anasema:
“Na kaeni majumbani kwenu, na wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani.”  [Al-Ahzaab 33:33]. 
Mwanamke yeyote yule kutoka nyumbani kwake [iwe amedharurika au bila ya kudharurika, kwa idhini au bila ya idhini] huwa anasababisha mengi kwa wanaume, kwani kwa kumuona tu wengi huanza kutaharuki, kubwa ya hilo ni kuwa ni vyema mwanamke aelewe kuwa anapotoka nyumbani kwake tu  mghururi na adui wake mkubwa [shaytwaan] humkalia mbele yake kwa kumuelekeza na bila shaka kumchezesha chezesha apendavo; kama ilivyothibiti katika hadiythi ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
”Mwanamke [mwili wake wote] ni uchi, hivyo akitoka [nyumbani kwake] shaytwaan humkalia mbele yake, na kwamba [mwanamke] anakuwa karibu zaidi na Wajhi wa Mola wake anapokuwa nyumbani kwake”[Imepokelewa na At Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Ijumaa, milango ya safar, Hadiyth namba 1090, na amesema kuwa: Hadiythi hasan ghariybu; na Ibnu Hibbaan, katika Kitabu cha Mapambo na kujitia manukato [At Tatwayyub], mlango wa Adabu za kulala, Hadiyth namba 5714; na Ibnu Khuzaymah, katika Kitabu cha Imaamah katika swallah, mkusanyiko wa milango ya Swallah za wanawake katika jama’a’h, mlango wa ukhiyari wa swallah ya mwanmke katika nyumba ake, Hadiyth namba 1596]. 

Hivyo kinachotakikana kwa mwanamke yeyote yule mwenye kumwamini Allaah na Siku ya Qiyamaah kujizuwia na kujihadhari kadiri awezavo kutoka nyumbani kwake, kwani akisalimika yeye katika nafsi yake, basi aelewe vyema kuwa walioko nje ambao watamtazama au watamuona hawatosalimika naye; hivyo akidharurika kutoka hutakiwa atoke katika hali inayokubalika kisharia, na iwe njia yake sehemu zisizokuwa na wanaume wengi [njia yake isiwe katika masoko, maduka na kadhalika], na ajichunge kusikiwa sauti yake, na ajitahidi kutumia njia ambazo hatawashughulisha wataomtazama.
Aayah iliyotangulia haimaanishi wala haiashirii kuwa Waumini wa kike wanatakiwa wabakie majumbani mwao tu mpaka wafishwe na mauti; na wala haimaanishi kuwa wamenyimwa au kuporwa haki zao ikiwemo fursa ya kutoka majumbani mwao kwa ajili ya kutimiza haja zao za kawaida na zilizo muhimu au dharura kama wanavyodai wale waliojipachika jina la kuwa wao ni watetezi wa haki za wanawake.
Mwanamke hakuruhusiwa kutoka nyumbani kwake hata kwa lengo la kwenda kutekeleza ibadah wachilia mbali kutoka kwenda kufanya kazi isipokuwa baada ya kutimiza vidhibiti alivyowekea na Muumba wake pale atokapo nyumbani kwake; kisharia mwanamke anatakiwa asizuiliwe anapotaka kwenda kutekeleza ibadah msikitini [ijapokuwa mwanamke kuswali nyumbani kwake ni bora zaidi] kama alivyoshauri na kuamrisha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kusema:
”Mwanamke wa mmoja wenu atakapo omba ruhusa kwenda msikitini basi asimzuiliye” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Ndoa, mlango wa kumuomba idhini mwanamke mumewe katika kutoka kwenda msikitini na kwingineko…, Hadiyth namba 4865; na Muslim, katika Kitabu cha Swalaah, mlango kutoka wanawake kwenda misikitini ikiwa hakutopelekea fitina…., Hadiyth namba 671, 672 na 673].


Juu ya kuwa huku utokaji wa mwanamke wa kwenda msikitini umeruhusiwa kwa amri ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuna awezae kuuzuia wala kuupinga na wala kuutafsiri vyenginevo, hata hivyo kwa kuwa walio nje hawawezi kujizuia na kutofitinishwa na mwanamke kwa yale aliyoyazua huyu mwanamke wakati aendapo huko msikitini na kwingineko, basi wingine kumewapelekea kuona na kusema kuwa lau Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angaliona yale waliyoyazua wanawake wa siku hizi [hayo yalisemwa katika zama za Swahaba Radhiya Allaahu ‘anhum] basi angaliwakataza kwenda misikitini kama alivyoonelea mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) jambo lililompelekea kufikia kusema:
”Lau Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameyaona yale waliyoyazua wanawake, basi angaliwazuia wanamke kwenda msikitini kama walivyozuiliwa wanawake wa banii Is-raaiyl” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Swalaah, mlango kutoka wanawake kwenda misikitini ikiwa hakutopelekea fitina…., Hadiyth namba 681; na Ahmad, katika Musnad, Musnad wa Kumi waliobashiriwa Jannah, Saadis ‘Ashar Al-Answaar, Hadiyth namba 25401]. 

Hii ni kusema kuwa hakuna awezae kuwanyima au kuwazuilia wanawake haki waliyopewa na Mjumbe wa Allaah(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuruhusiwa kwenda misikitini watakapoiomba kwa waume zao; lakini ni vyema ieleweke kuwa haki hiyo inatakiwa ichukuliwe kwa adabu zake na kwa vidhibiti vyake vya kisharia vilivyothibiti vyenye kuhusiana na utokaji wa mwanamke. 

Kutoka kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema:”Siku moja Sawdah (Radhiya Allaahu 'anhaa, ambaye ni katika mama wa Waumini kwa kuwa ni katika wake za Mjumbewa AllaahSwalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam] alitoka usiku – baada ya kufaradhishwa hijaab- kwa ajili ya kutimiza haja zake, na (Radhiya Allaahu 'anhaa) alikuwa mwanamke mahashumu , mkubwa wa umbo, hafichikani kwa anaemjua, basi ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuona , akamwambia: Ee Sawdah, kwa Jina la Allaah huwezi kujificha kwetu [kwa maana kuwa atakavyo jifunika vyovyote vile wenye kumjua watamtambuwa tu], hivyo [utokapo] tafuta namna ya kutoka kwako, [bibi ‘Aaishah Radhiya Allaahu 'anhaa] akasema: Basi alijirejea zake kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamueleza yalioyomtokezea, na yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kwenye chumba change, alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akila chakula cha usiku ……..; basi Allaah Akamshushia juu yake, ilipomalizika alisema:Kwa hakika mmeruhusiwa [wanawake] kutoka kwa ajili ya kutimiza haja zenu” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Ndoa, mlango wa kutoka wanawake kwa ajili ya kutimiza haja zao…, Hadiyth namba 4864; na Muslim, katika Kitabu cha As Salaamu, mlango wa uhalali wa kutoka wanawake kwenda kukidhi haja ya kibinaadamu, Hadiyth namba 4041]. 

Muumini wa kike hatarajiwi kuwa mzururaji ovyo na mpitaji huku na kule kama mnyama asiye na msimamizi; bali hutarajiwa kutoka kwa kutimiza mahitaji yake kwa vidhibiti vya kisharia; kama vile pale atokapo awe amejisitiri mwili wake, asioneshe mapambo yake, na wala asijipake manukato, na wala asijishauwe wala kujichezesha chezesha.
Miongoni mwa yaliyo muhimu pia ambayo huenda yakampelekea mwanamke kutoka nyumbani kwake baada ya kuruhusiwa na mumewe ni huku kutoka kwake na kwenda kujitafutia elimu, au kwenda kufanya kazi katika zile kazi alizoruhusiwa mwanamke zenye kwenda sambamba na umbile lake la kike na kwa masharti yanayoeleweka kama:
·         kazi yenyewe iwe ni ya halali.
·         Maadili ya ufanyaji kazi uwe katika mipaka ya Uislamu.
·         Pasiwepo mchanganyiko baina ya wanawake na wanaume.
·         Kazi yenyewe isiathiri majukumu yake ya nyumbani kama mke.
Mwanamke ameruhusiwa kutoka kwenda kufanya kazi akihitajika kama ni mwanamke na pia pakihitajika hilo, na sio tu kufanya kazi kwa lengo la kujiengezea pato na kutafuta anasa za kupita za kidunia, bali ameruhusiwa kufanya kazi zilizo muhimu na kwa dharura kama inavyodhihirika na kubainika katika Kauli Yake Allaah:
 “Na [Muwsaa] alipo yafikia maji ya Madyana alikuta umati wa watu wananywesha [wanyama wao], na akakuta pasina wao wanawake wawili wanawazuia wanyama wao. [Muwsaa] Alisema: Mna nini? Wakajibu: Hatunyweshi sisi mpaka wamalize wachunga [wakiume]. Na baba yetu ni mzee sana.[Al Qaswasw 28:23].


Hivyo katazo hili ni kwa wanawake wenye kupenda kutoka majumbani mwao makusudi bila ya kutaka kutimiza haja muhimu wala dharura, bali hutoka kwa ajili nyingine zisizo kubalika kisharia; na pia hii ruhusa ya mwanamke kufanya kazi ni kwa dharura na sio vyenginevo.   
Ikiwa mwanamke Muumini atagundua kuwa anahitaji kufanya kazi kutokana na umahiri wake katika fani ambayo inahitajika ishikwe na mwanamke na kwa sababu ya umuhimu fulani [dharura], basi huyo ameruhusiwa kutoka nyumbani kwake na kwenda kuitekeleza hiyo kazi [kama ilivyodhihirika katika Aayah iliyotangulia hapa juu], kwani katika Aayah kumewekwa wazi kuwa wasichana wawili walikuwa wakinyesheza wanyama kwa dharura kuwa baba yao alikuwa hawezi kwa uzee wake, na juu ya huko kuruhusiwa kwao kufanya kazi kwa dharura hawakuwa wakichanganyika na wanaume wenye kuweza kuwaoa.   

Kuna mifano mingi tu ya Swahaabiyyat [Radhiya Allaahu ‘anhunna] waliokuwa wakitoka majumbani mwao na kwenda kufanya kazi si kwa lengo la kujiengezea kipato wala kutafuta anasa za kidunia, bali kwa kuwa jamii inawahitaji na kwa dharura; Rufaydah al-Ansaariyyah [Radhiya Allaahu ‘anhaa] alikuwa akiwahudumia waliojeruhiwa vitani katika hema lake lililosimamishwa Msikitini.


Kwa mwanamke mwenye kumwamini Allaah na Siku ya Qiyamaah hutarajiwa aelewe kuwa kukatazwa kutoka nyumbani kwake bila ya dharuani ni katika mikakati ya Uislamu iliyomuwekea kwa lengo la kumlinda na kumpa hadhi isiyonunulika wala kadirika.
Uislamu umempa Muumini wake wa kike heshima ya pekee na ya hali ya juu kwa kuwa yeye [Muumini wa kike] ndiye mrithi wa pekee wa kizazi cha waislamu kilichopita, kizazi kilichoshikamana na Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mwenendo wa Swahaabiyyat (Radhiya Allaahu ‘anhunna); pia yeye [Muumini wa kike] ndie msimamizi, mchungaji, mtoaji wa malezi ya Kiislamu na mpandiliaji na mpaliliaji wa iymaan ya Kiislamu kwa kizazi kipya; iymaan ya kuweza kukifikisha kizazi kuweza kumjua na kumuelewa Allaah, kuelewa Dini Yake, kumuelewa Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutakakompeleka kumfikisha kumpenda na kumfuata (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama kutakiwavo na kadhalika katika yenye kuweza kumfikisha mtoto kujielewa kuwa yeye Ameumbwa, na aliye muumba Amemletea wa kumuiga katika kila lenye kuhusiana na maisha yake, na kuwa na yakini kuwa kuna Siku atasimamishwa mbele ya huyo Aliye muumba. 
Dada yangu katika iymaan elewa na kuwa na yakini kuwa kutakiwa kwako kubakia katika nyumba yako ni kwa kuwa Uislamu umekubebesha dhamana adhimu, dhamana kubwa mno ambayo utakuja kuulizwa kwayo.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Tanabahini! Nyie nyote ni wachunga, na nyie nyote mtaulizwa kwa mlichokichunga; kiongozi wa watu ni mchunga na ataulizwa kwa kile alichokichunga, na mwanamume ni mchunga wa familia wake na ataulizwa kwa alichokichunga, na mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mume wake na watoto wake naye ataulizwa kwa alichokichunga, na mtumwa ni mchunga wa mali ya bwana wake naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake; “Tanabahini! Nyie nyote ni wachunga na nyie nyote mtaulizwa kwa mlichokichunga” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Ndoa, mlango wa mwanamke ni mchungaji katika nyumba ya mumewe, Hadiyth namba 4828 na Muslim, katika Kitabu cha Al-Imaarah, mlango wa fadhila za Imamu mwadilifu…., Hadiyth namba 3414].
Hivyo dada yangu katika iymaan kutakiwa na Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuto toka nyumbani kwako isipokluwa kwa dharura ni kwa malengo Ayajuayao Allaah yakiwemo kuhifadhika, kuheshimika, na kukingika; hivyo katazo hili si lenye kukukandamiza wala kukunyanyasa au kukunyang’ana uhuru wako wala hadhi yako kama wanavyodai na kuzua wenye kujipachika jina la watetezi wa haki zako na za wanawake wenzako; neno la haki lakini limekusudia na kutakia batili; kwani hakuna mwenye kuipata au kupewai haki yake, iwaje tena wawe wanatetea haki za wanawake, na hali wao ndio wanyang’anyi wa haki ya kila mwenye haki awe mwanamume au mwanamke!
Dada yangu katika iymaan, jiweke kitako chini ujiulize; ni nani atalea kizazi kipya cha Kiislamu na kukitunza kukielimisha kama inavyotakiwa?  Nani atatunza na kusimamia maslaha ya majumba, furaha ya familia na kadhalika?
Dada yangu katika iymaan, ni vyema kushikilia na kushikamana  na lile Alilokuamrisha Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kujilazimisha kubakia nyumbani kwako isipokuwa kwa dharura au haja yenye kukubalika kisharia na ikilazimika utoke basi toka huku ukijipamba kwa adabu za kisharia na vidhibiti vyake.


 Posted By Posted juu ya Friday, June 29 @ 17:43:58 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili:
Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa Rafiki





Mada zinazohusiana

Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili

 

Ẹsin Islam الدين الإسلامي Religion of Islam Addinin Musulunci Agama Islam Religión del Islam 伊斯兰教 Dini ya Kiislamu Религия Ислам Religião do Islã イスラム教 Esin Islam 이슬람의 종교 Portal African Muslim Website - Arabic English African Islamic Website For World News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Articles, Radio, Audio, Video, Quran, Hadith, TV Channels, Fatwas, Muslim News, Newspapers, Magazines Headlines, Forums, College, Schools, Universities, Mosques, Quranic, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Ramadan, Vidoes, Books, Fasting, PDFs On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com