Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 
Kazi Katika Uislam: UTANGULIZI, HADHI YA KAZI, KAZI ZILIZOHARAMISHWA,
 
Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis
Uislamu Na Shari'ah Zake
UTANGULIZI

Kulingana na Kamusi ya Kiingereza ya Collins, kazi imefafanuliwa kama juhudi za kimwili au kiakili zilizoelekezwa kufanya/ kutengeneza kitu, malipo anayopewa kwa amali, biashara, utaalamu, shughuli au ufahamu.Katika Uislam, kazi inamaanisha juhudi au uajiriwa unaofanywa ili mtu kupata pato la halali na katika mipaka ya maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kanuni Zake. Pale Muislam anapofanya hivyo kwa nia safi na ikhlasi, anapata ujira kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).

 Katika Uislam dunia ni sehemu ya kuvuna kwa ajili ya Akhera. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
“Na utafute, kwa Aliyokupa Allaah, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Allaah alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Allaah hawapendi mafisadi” (28: 77).
Na Anasema vilevile: “Na Tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha” (78: 11).
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuwekea mchana hasa ili tuweze kuhangaika kimaisha.
 Kwa sababu sisi tuko katika ardhi hii, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametufundisha du’aa ifuatayo ya sisi kutaka kheri za nyumba mbili. Anasema Aliyetukuka: “Na katika wao wapo wanaosema: Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto! Hao ndio watakaopata sehemu yao kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu” (2: 201 – 202).
Waislam katika eneo la Afrika Mashariki wanachukuliwa kuwa sawa na wavivu kwa sababu ya jinsi walivyojiweka katika hali ya uzembe wa hali ya juu. Utawaona vijana wenye miili imara wanakaa mabarabarani, kwenye mabustani na mabarazani, nje ya Msikiti na sehemu nyengine za anasa wakizembea na kuzungumza mambo ya upuuzi. Pia vijana waliohamia nchi za kimagharibi kwa sababu ya ruzuku inayotolewa na serikali wamechukua mienendo hiyo mibaya.
Si halali kwa Muislam kutofanya kazi ili kujikimu kimaisha kwa kisingizio cha kuyaweka maisha yake kuwa wakfu kwa ajili ya kufanya ‘Ibaadah au kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa njia hiyo. Pia haifai kwao kutegemea sadaka japokuwa wana uwezo wa kufanya kazi kwa juhudi na nguvu zao. Katika hili, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sadaka si halali kwa tajiri wala mwenye uwezo wa kimwili” (at-Tirmidhiy).
Katika riwaya nyengine ya Abu Daawuud na an-Nasaa’iy, ‘Ubaydullah ibn ‘Adiyy al-Khiyaar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameripoti: “Watu wawili waliniambia kuwa walikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati wa Hijjatul Widaa alipokuwa akigawa Zakaah. Walimtaka usaidizi. Aliwatazama kuanzia utosini hadi chini na kuwaona kuwa wamejenga vizuri na wenye nguvu. Aliwaambia: ‘Ikiwa mwataka, nitawapatia (Zakaah), lakini hakuna Zakaah kwa aliye tajiri wala kwa yule mwenye nguvu anayeweza kupata pato”.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakataza Waislam kuomba omba pasi na dharura yoyote, hivyo kukosa heshima na hadhi. Hili lengo lake ni kuwafundisha na kuwahimiza Waislam kulinda na kuwa mbali na mienendo ya kupe kwa kuwanyonya wenziwe (watu wengine).
HADHI YA KAZI
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anataja misingi inayotakiwa katika kufanya ukulima. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameitandaza ardhi na kuifanya kuwa muruwa na yenye rutuba kwa ajili ya ukulima na kumeza pamoja na kupata mazao. Zipo ayah nyingi kuhusu hilo lakini unaweza kutazama baadhi yake kwa mfano “Na ardhi Tumeitandaza na humo tumeweka milima, na tumeotesha kila kitu kwa kiasi chake. Na Tumekujaalieni humo vitu vya maisha yenu, na ya hao ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku. Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu” (15: 19-22)
 
“Na ardhi ameiweka kwa ajili ya viumbe. Humo yamo matunda na mitende yenye mafumba. Na nafaka zenye makapi, na rehani. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu Mlezi mnayoikanusha” (55: 10-13)
 
“Na Mwenyezi Mungu Amekukunjulieni ardhi kama busati. Ili mtembee humo katika njia zilizo pana.” (71: 19-20)
 
“Hebu mtu na atazame chakula chake. Sisi Tumemimina maji kwa nguvu, Tena Tukaipasua pasua ardhi kwa nguvu, Kisha Tukaotesha humo nafaka, Na zabibu, na mimea ya majani,” (80: 24-28) na kadhalika.
 
Katika ayah zote hizo kuna kuhimizwa watu kuwa wakulima na kutilia maanani ukulima. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Pindi Muislam anapopanda mti au mmea, hakuna ndege wala mwanaadamu atakayekula kwayo isipokuwa anaandikiwa sadaka” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Na katika Hadiyth nyingine anasema: “Kikisimama Qiyaama na mkononi mwa mmoja wenu ana mche akaweza kuumeza basi afanye hivyo kwani atapata ujira kwayo”. Hii ni hima ya hali ya juu aliyotupatia Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata katika wakati mgumu kama huo wa Qiyaama ambapo mambo yote yatabadilika.
Mbali na ukulima, Muislam anaweza kujishughulisha na sayansi za msingi, viwanda na taalamu nyengine kwa idadi kubwa inayoweza kukidhi mahitaji yetu ya kijamii.
Qur-aan imetaja viwanda na taaluma nyingi na kuziita ni fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza kuwa:
Nabii Daawuud (‘Alayhis Salaam) alikuwa mfua vyuma hivyo akitengeneza nguo za chuma za kivita.
“Na tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru”21: 80
“Na tulimpa Daawuuud fadhila kutoka kwetu, (tukasema): Enyi milima! Karirini kumtakasa Mwenyeezi Mungu pamoja naye! Na ndege pia. Na tukamlainishia chuma. (Tukamwambia:) Tengeneza nguo za chuma pana, na kadiria sawa katika kuunganisha. Na tendeni mema. Hakika Mimi nayaona vyema mnayo yatenda” (34: 10-11)
Nabii Sulaymaan (‘Alayhis Salaam) alikuwa mjengaji
“Na Sulaymaan tuliufanya upepo umtumikie. Safari yake ya asubuhi ni mwendo wa mwezi mmoja, na safari yake ya jioni ni mwendo wa mwezi mmoja. Na tukamyayushia chemchem ya shaba. Na katika majini walikuwako walio kuwa wakifanya kazi mbele yake kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na kila anayejitenga na amri yetu katika wao, tunamwonjesha adhabu ya Moto unaowaka. Walikuwa wakimfanyia alipendalo, kama mihrabu, na masanamu, na madeste makubwa kama mahodhi, na masufuria makubwa yasiyo ondolewa mahala pake. Enyi watu wa Daawuud! Fanyeni kazi kwa kushukuru. Ni wachache katika waja wangu wanao shukuru” (34: 12-13),
Dhul Qarnayn alitengeneza ukuta mrefu kama kizuizi dhidi ya maadui
“Akasema: Yale Mola wangu aliyo niwezesha ni bora zaidi. Lakini nyinyi nisaidieni kwa nguvu zenu. Nitakujengeeni kizuizi baina yenu na wao. Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema: Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie. Basi hawakuweza kuukwea, wala hawakuweza kuutoboa” (18: 95-97)
Nabii Nuuh (‘Alayhis Salaam) alikuwa seremala
“Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usinisemeze kuwatetea walio dhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa. Na akawa anaunda jahazi, na kila wakipita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Yeye akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli na sisi tunakukejelini kama mnavyo tukejeli” (11: 37-38).
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) pia Anatutajia merikebu kubwa sana kama milima, ambazo zinavuka baharini
“Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyo kwenda na kurejea baharini kama vilima” (42: 32).
Zaidi ya hayo, Qur-aan imetufahamisha kuwa chuma kina thamani kwa kutilia mkazo jambo hilo.
 
Anasema Aliyetukuka: “Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu Amjue anaye mnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu” (57: 25).
Kazi yoyote yenye kukidhi mahitaji ya jamii au inayoleta faida ya kihakika inachukuliwa kuwa ni nzuri, ilimradi anayeifanya aifanye kwa njia nzuri, kama inavyotakikana na Uislam. Baadhi ya watu wanazitweza baadhi ya kazi, lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatufundisha kuwa heshima na hadhi ya mtu imefungamana na yeye kufanya kazi – kazi aina yoyote ila zile zilizo haramishwa. Hivyo, Uislam ulinyanyua hadhi na vyeo vya kazi nyingi ambazo watu walikuwa wanaziona kuwa duni.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni bora kwa mtu kuchukua kamba na kuleta mzigo wa kuni mgongoni mwake na kuzuiza ili Allaah Ailinde heshima yake, kuliko yeye kuomba kutoka kwa watu bila kujali kama watampatia au watamnyima” (al-Bukhaariy na Muslim).
Ndio yule Swahaba alipokariri kuja kumtaka msaada Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza kama ana akiba yoyote nyumbani kwake. yule bwana akamwambia anacho kitambara. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwagizia akilete, na kilipoletwa alikinadi nacho kikanunuliwa kwa dinari mbili. Moja kati ya hizo dinari mbili Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia anunulie chakula na akiache nyumbani. Ya pili Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe alikwenda sokoni na kununua kile chuma cha shoka na kumtilia mpini kwa mkono wake. Kisha alimwambia asionekane pale mpaka baada ya muda fulani. Swahaba huyo alielekea msituni ili kukata kuni. Baada ya muda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikutana na huyo bwana kukiwa na sauti ya pesa zikilia m*****oni kwake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia hii ni bora kabisa kuliko kuomba omba.
Mitume na Manabii (‘Alayhimus Salaam) ndio ruwaza njema kwetu. Wao walifanikiwa katika kazi zao kwa kiasi kikubwa. Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Daawud alikuwa mtengenezaji makoti ya chuma na ngao zake, Aadam alikuwa mkulima, Nuuh alikuwa seremala, Idriys mshonaji na Muusa mchungaji” (Al-Haakim).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hakumtuma Mtume bila ya yeye kuchunga kondoo”. Wakamuuliza Maswahaba: “Hata wewe, ewe Mtume wa Allaah?” Akajibu: “Hata mimi, nilikuwa nikichunga kondoo wa watu wa Makkah kwa ujira” (Al-Bukhaariy).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaambia Maswahaba zake hivi ili kuwafunza kuwa heshima inakuwa kwa wale wanaofanya kazi, na sio wale wenye kukaa na kuzembea na kuwa kupe kuwala wengine. Nasi tunaakiwa tufuate mtindo huo wa kufanya kazi. Zipo fursa nyingi, ambazo zinaonekana na sisi Waislam kama ni kazi duni zinazotuteremsha vyeo ambapo wengi wanaishi kwa kufanya kazi hizo na vile vile kuwa na hadhi zao nzuri. Na hivyo kuwa na heshima na hakuna wa kumkebehi au kumdharau kwa kuwa yeye anafanya juhudi na anakula kwa jasho lake.
Uislam umetuhimiza sisi kufanya biashara, na kuziita kutafuta fadhila ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Tafadhali tazama ayah zifuatazo kuhusu mas-ala hayo 2: 198; 24: 37; 28: 57; 73: 20 na kadhalika.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanya biashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (At-Tirmidhiy na al-Haakim). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe aliweka nidhamu kabambe na kanuni za kibiashara mbali na ghushi (udanganyifu), kuwasilisha kwa namna nyengine, kuficha bidhaa na kufanyiana hiyana.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupigia mfano wa jinsi ndege anavyofanya juhudi kutafuta riziki na akakuita kuwa ni kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika hilo. Hivyo kumtegemea Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni mwanzo kumfunga ngamia kisha kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) asimfanye atoroke. Imepokewa kwa ‘Umar ibn al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Ikiwa nyinyi mtamtegemea Allaah upeo wa kumtegemea basi Atawaruzuku nyinyi kama Anavyomruzuku ndege. Anatoka katika kiota chake asubuhi tumbo lake likiwa tupu na anarudi ikiwa tumbo lake limejaa” (At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Sahihi).  
KAZI ZILIZOHARAMISHWA
Uislam umeharamisha baadhi ya kazi, ambazo zinakwenda kinyume na kiini cha misingi yake. Ni haramu kumeza, kula au kuvuta mti kama hashiysh, tumbaku, marijuana, na mihadarati mingineyo ambayo ni haramu kuliwa, kutafunwa au kuvutwa, kwa kuwa mimea kama hiyo haina matumizi mengine ila ya kuleta madhara. Pia si sababu sahihi kwa Muislam kusema anapanda miti au anafuga wanyama kwa ajili ya kuwauzia wasiokuwa Waislam, kwani Muislam haruhusiwi kushiriki katika kueneza vilivyo haramu na vyenye madhara.
Uislam pia umekataza taalamu fulani na viwanda kwa wafuasi wake kwa sababu zina madhara kwa itikadi, maadili, heshima, muruwa na kadhalika. Mfano ni kama ukahaba ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Wala msiwashurutishe vijakazi vyenu kufanya zinaa kwa ajili ya kutafuta pato la maisha ya dunia, ilhali wao wanataka kujihishimu. Na atakaye walazimisha basi Allaah baada ya kulazimishwa kwao huko, Atawasamehe, kwani Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu” (24: 33).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia alikataza hilo, bila kuangalia wala kujali nani atafaidika kwayo. Uislam umekataza dansi, muziki hata nyimbo zenye kuamsha hisia za kiume au kike au shughuli nyingine yoyote kama hiyo, kama nyimbo zenye kuashiria au zilizo chafu au michezo ya kuigiza yenye kuelekeza kwenye uasherati na kadhalika. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).
Utengenezaji wa vileo, mihadarati na masanamu pia umeharamishwa. Uislam umekataza biashara yenye dhulma, udanganyifu, kuongeza faida kubwa sana katika biashara au kueneza vitu vya haramu. Pia ni haramu kufanya biashara ya pombe, nguruwe, masanamu au kitu chengine chochote ambacho utumiaji wake umeharamishwa na Uislam. Wafanya biashara wawe na tahadhari ya kughushi, kugeuza au kuvuruga vipimo na ratili, kuzuilia na kuficha bidhaa ili asiwe ni mwenye kukosa ulinzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Pia atahadhari kwa hilo, kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema yafuatayo kuhusu kupunja katika kupima: “Ole wao hao wapunjao! Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe. Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza” (83: 1-3).
Watu wa Madyan, waliotumiwa Mtume Shu‘ayb (‘Alayhis Salaam) ili kuwaonya dhidi ya kupunja wanapopima waliadhibiwa vikali sana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumkadhibisha Nabii wao (Tazama 7: 85-93 na 11: 84-95).
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatoa onyo kali kwa mwenye kuchukua na kutoa riba na Ametangaza vita dhidi yao.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyeezi Mungu, na acheni riba zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini, Basi mkitofanya jitangazieni vita na Mwenyeezi Mungu na Mtume Wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe” (2: 278-279). 
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Dirhamu moja ya riba ambayo mtu ataitumia kwa kujua ni mbaya zaidi kuliko kufanya zinaa mara 36” (Ahmad).
Haifai kabisa kuficha vyakula ili kupata faida nyingi zaidi au kuficha kasoro ya bidhaa yoyote unayouza.
 
SIFA NZURI ZA MFANYAKAZI MUISLAM
Mfanyakazi Muislam mzuri ana sifa maridhawa zifuatazo:
 
1. Mjuzi na Mwenye Elimu: Ujuzi na elimu ni sifa muhimu sana ili shughuli zote ziendeshwe kitaalamu kama inavyotakiwa. Ndio Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) alimwambia mfalme wa Misri yafuatayo: “Yusuuf akasema: Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi” (12: 55).
 
2.   Uaminifu na Nguvu: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anazungumzia kuhusu tazkiya aliyotoa binti ya mzee mkongwe kwa babake kwa sifa alizokuwa nazo Muusa (‘Alayhis Salaam): “Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu” (28: 26).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfanyabiashara muaminifu atakuwa pamoja na Manabii, wakweli na mashahidi” (At-Tirmidhiy na al-Haakim). Muislam ni lazima awe muaminifu katika shughuli zake zote na kutokuwa muaminifu ni kuwa na moja wapo wa alama ya unafiki.
3.   Kutunza Vitu vilivyo chini yake: Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anamzungumzia Nabii Yuusuf (‘Alayhis Salaam) pale aliposema: “Nifanye mshika khazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mjuzi” (12: 55). 
4.    Bidii na Juhudi: Pato la kufanya kwa mikono yako ndio kazi bora kabisa ambayo mtu anaweza kufanya. Imepokewa na Rafi‘ ibn Khadij (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa ni pato gani lililo bora zaidi, naye akajibu: “Ni mtu kufanya kazi kwa mikono yake na kila biashara iliyokubaliwa (na sheria)” (Ahmad na at-Tirmidhiy).
Mitume wote (‘Alayhimus Salaam) walikuwa wakila kwa pato la jasho lao kwa kufanya kazi.
 
5. Kutunza Wakati wa Kazi: Hii ni sifa ya Muumini aliyejikita katika Iymaan. Mtu anapoanza kazi huwa ana mkataba na mkubwa wa kampuni au shirika na kila mfanyakazi huwa ana masaa yake ya kuwa kazini. Kutotekeleza hilo huwa unajiingiza katika sifa ya unafiki kwani Muislam mwema na mzuri ni yue anayetunza mkataba na ahadi.

SIFA NZURI ZA MWAJIRI MUISLAM
Mwajiri Muislam ni lazima afikirie na azingatie zile hisia za wanaadamu wenziwe. Hivyo, asimtwike mwajiriwa kwa kumpatia kazi au mzigo asiouweza. Tazama jinsi gani yule mzee mkongwe na mcha Mungu alivyomwambia Nabii Muusa (‘Alayhis Salaam): “Akasema: Mimi nataka kukuoza mmojawapo katika binti zangu hawa wawili kwa kunitumikia miaka minane. Ukitimiza kumi, khiari yako; lakini mimi sitaki kukutaabisha. InshaAllaah utanikuta miongoni mwa watu wema” (28: 27).
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema yafuatayo kuhusu hayo kama ilivyopokewa na Safwaan kutoka kwa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba amesema: “Tahadharini sana, kwani yeyote atakayemdhulumu mtu aliyeandikiana naye mkataba, au akampunja haki yake, au akamlazimisha kufanya kazi ngumu upeo wa nguvu zake, au akamchukulia chochote pasi na idhini yake, mimi nitamtetea Siku ya Qiyaama” (Abu Daawuud).
Mwajiri hafai kumtwika mzigo mkubwa hata mtumwa wake kwa kumpatia kazi zaidi ya uwezo wake, basi mwajiriwa ndio haifai zaidi. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ni muhimu sana kumlisha mtumwa, kumvisha (sawa sawa) na kutomtwika mzigo wa kupita uwezo wake” (Muslim).
Katika riwaya ya Imaam Maalik, Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amepokea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtumwa anafaa apatiwe chakula na mavazi kwa njia ya kawaida, na anawajibika kufanya zile kazi anazoweza bila ya shida”. Maalik amesema kuwa ‘Umar ibn al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akienda vijijini kila siku ya Jumamosi na pindi anapomuona mtumwa anafanya kazi inayopita uwezo na nguvu zake basi alikuwa akimpunguzia.
Mfanyakazi anatakiwa alipwe ujira au mshahara wake kikamilifu pindi tu anapomaliza kazi yake hiyo au mwisho wa mwezi. Kuhusu hili amepokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana, lakini mfanyakazi analipwa ujira wake kamili pale tu anapomaliza kazi yake” (Ahmad na at-Tirmidhiy). Na katika riwaya nyengine: “Kabla jasho lake halijakauka”.
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anamchukia na Atakuwa dhidi ya mwajiri asiyelipa ujira au mshahara kwa ukamilifu kwa waajiriwa wake. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Anasema: ‘Nitakuwa dhidi ya watu watatu Siku ya Qiyaama:
1.      Mtu anayefanya ahadi kwa jina Langu, lakini anafanya khiyana,
2.      Mtu anayemuuza mtu huru (kama mtumwa) na kula thamani yake, na
3.      Mwajiri anayemwandika kibarua ambaye anafanya kazi yake kiukamilifu lakini yeye hamlipi ujira wake’” (Al-Bukhaariy).
 
HITIMISHO
Kwa muono wa Uislam, Waumini wa kweli ni wale wenye kutekeleza amali na kutia bidii katika kazi zao za halali, ambao sifa zao za kipekee ni kuwa shughuli za hii dunia haziwafanyi wao kusahau wajibu wao kwa Mola wao Mlezi. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Allaah, na kushika Swalah, na kutoa Zakaah. Wanaikhofu Siku ambayo nyoyo na macho yatageuka” (24: 37).
Muislam mzuri ni yule ambaye baada ya amali yoyote ya ‘Ibaadah moja anajitupa uwanjani ili kutafuta fadhila za Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema: “Na itakapo kwisha Swalah, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Allaah, na mkumbukeni Allaah kwa wingi ili mpate kufanikiwa” (62: 10). Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa hima na sisitizo Alilotupatia kwa kazi Hakuiacha hata siku tukufu na siku kuu ya wiki, Ijumaa iwe sisi hatufanyi kazi bali Anataka baada ya Swalah ya Ijumaa tutawanyike katika ardhi ili tufanye kazi na tupate riziki ya halali.
Muislam anapotunukiwa fadhila na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), anafaa amuhimidi na kumshukuru Muumba wake kwa kushikilia amri Zake na kukaa mbali na makatazo Yake. Huu ni mtihani kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), kwani Yeye Anasema: “Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu” (27: 40).
Lau waajiri Waislam watachukua maagizo haya na kujipamba na sifa tulizozitaja zilizowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waajiriwa nao wakatekeleza wajibu na majukumu yao basi hakungekuwa na matatizo aina yoyote katika jamii yetu ya Kiislam. Inabidi sisi turudi katika Uislam sahihi uliokamilishwa na Mtume wetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tupate kufanikiwa hapa duniani na kesho Akhera.


 Posted By Posted juu ya Thursday, May 10 @ 19:30:51 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis:
Jinsi Ya Kumfurahisha Mkeo


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa RafikiMada zinazohusiana

Ulimwengu wa Kiislamu na masuala ya Kiis

 

EsinIslam The Muslim World Portal For Islamics, News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Quranic Islamic Articles, Radio, Audio Quran, TV Channels, Fatwa Rulings, Muslim News Newspapers Magazines Headlines Articles Forums Schools, Universities, Colleges, Mosques, Qur'an, Hadith, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Fasting Ramadan, Vidoes, Books On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com