Siku mtapo iona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye
mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini
adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.
Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi
tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na
kipande cha damu ilio gandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo
na kisicho kuwa na umbo, ili tukubainishieni. Nasi tunakiweka katika matumbo ya
uzazi tunacho kitaka mpaka muda ulio wekwa. Kisha tunakutoeni kwa hali ya mtoto
mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanao kufa, na wapo
katika nyinyi wanao rudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui
kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapo
yateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea
mizuri.
Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri
hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na
Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.
Anaye dhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na Akhera na
afunge kamba kwenye dari kisha aikate. Atazame je hila yake itaondoa hayo yaliyo
mkasirisha?
Hakika walio amini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na
wale walio shiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya
Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.
Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu viliomo mbinguni na viliomo katika
ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi
miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anaye fedheheshwa na
Mwenyezi Mungu hana wa kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda apendayo.
Hawa wagomvi wawili walio gombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi walio kufuru
watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayo chemka.
Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani
zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya mikononi ya dhahabu
na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri.
Hakika wale walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti
Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na
wageni. Na kila atakaye taka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi tutamwonjesha
adhabu chungu.
Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe
na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanao izunguka kwa kut'ufu,
na wanao kaa hapo kwa ibada, na wanao rukuu, na wanao sujudu.
Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku
maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni
mwenye shida aliye fakiri.
Ndio hivyo iwe! Na anaye vitukuza vitakatifu vya Mwenyezi Mungu basi hayo ndiyo
kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na mmehalalishiwa nyama hoa ila wale mlio
somewa. Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni na usemi wa uwongo.
Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha. Na anaye
mshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha
ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahala mbali.
Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina
la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyo ruzukiwa katika wanyama wa mifugo. Basi
Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake tu, na wabashirie
wanyenyekevu,
Na ngamia wa sadaka tumekufanyieni kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Mwenyezi
Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao
wanapo simama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni walio
kinai na wanao lazimika kuomba. Ndio kama hivi tumewafanya hawa wanyama dhalili
kwenu ili mpate kushukuru.
Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia uchamngu
wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyo
kuongoeni. Na wabashirie wafanyao mema.
Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola
wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa
watu, basi hapana shaka zingeli vunjwa nymba za wat'awa, na makanisa, na
masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa
wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu.
Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na
wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya
mambo yote.
Je! Hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au
masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazo pofuka
ni nyoyo ziliomo vifuani.
Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi
yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo
hisabu nyinyi.
Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anapo soma, Shet'ani hutumbukiza
katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayo yatia Shet'ani; kisha
Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye
hikima.
Hayo ni ili alifanye lile analo litia Shet'ani liwe ni fitna kwa wale wenye
maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni ngumu. Na hakika
madhaalimu wamo katika mfarakano wa mbali.
Na ili walio pewa ilimu wajue kuwa hayo ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi na
waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye anaye waongoa
wenye kuamini kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Na walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au wakafa, bila ya
shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mbora
wa wanao ruzuku.
Ndio namna hivi. Na anaye lipiza mfano wa alivyo adhibiwa, kisha akadhulumiwa,
basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu
Mwenye maghfira.
Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huuingiza
mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.
Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Wa Kweli, na kwamba wale wanao waomba
badala yake, ni baat'ili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Aliye Juu na ndiye
Mkubwa.
Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu viliomo katika ardhi, na
marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya
ardhi ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu,
Mwenye kurehemu.
Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazo zishika. Basi wasizozane nawe katika
jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi. Hakika wewe uko kwenye
Uwongofu Ulio Nyooka.
Na wanapo somewa Aya zetu zilizo wazi utaona chuki katika nyuso za walio kufuru.
Hukaribia kuwavamia wale wanao wasomea hizo Aya zetu. Sema: Je! Nikwambieni
yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi Mungu amewaahidi walio
kufuru, na ni marudio mabaya hayo.
Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnao waomba badala ya
Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi
akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka
na mwenye kutakiwa.
Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyo stahiki jihadi yake.
Yeye amekuteueni. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila
ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni Waislamu tangu zamani, na
katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume shahidi juu yenu, na nyinyi muwe
mashahidi kwa watu. Basi shikeni Sala na toeni Zaka na shikamaneni na Mwenyezi
Mungu. Yeye ndiye Mlinzi wenu, Mlinzi bora kabisa, na Msaidizi bora kabisa.