Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda
zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi.
Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu
ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka
mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Mwenyezi
Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya.
Basi wanapo fikia muda wao, ima warejeeni muwaweke kwa wema, au farikianeni nao
kwa wema. Na mshuhudishe mashahidi wawili waadilifu miongoni mwenu. Na
simamisheni ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo ndivyo anavyo agizwa
anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na anaye mcha Mwenyezi Mungu
humtengezea njia ya kutokea.
Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia. Na anaye mtegemea Mwenyezi Mungu Yeye
humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia
kila kitu na kipimo chake.
Na wale walio sita hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka, basi
muda wa eda yao ni miezi mitatu, pamoja na ambao hawapati hedhi. Na wenye mimba
eda yao mpaka watakapo zaa. Na anaye mcha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu
humfanyia mambo yake kuwa mepesi.
Wawekeni humo humo mnamo kaa nyinyi kwa kadiri ya pato lenu, wala msiwaletee
madhara kwa kuwadhiki. Na wakiwa wana mimba, wagharimieni mpaka wajifungue. Na
wakikunyonyesheeni, basi wapeni ujira wao, na shaurianeni kwa wema. Na mkiona
uzito kati yenu, basi amnyonyeshee mwanamke mwengine.
Mwenye wasaa atoe kadiri ya wasaa wake, na mwenye dhiki atoe katika alicho mpa
Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa kadiri ya alicho mpa.
Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji.
Mtume anaye kusomeeni Aya za Mwenyezi Mungu zinazo bainisha, ili kuwatoa walio
amini na wakatenda mema kutoka gizani kuwapeleka kwenye nuru. Na mwenye
kumuamini Mwenyezi Mungu, na akatenda mema, atamwingiza katika Bustani zipitazo
mito kati yake, wadumu humo milele. Mwenyezi Mungu amekwisha mpa riziki nzuri.
Mwenyezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba, na ardhi kwa mfano wa hizo.
Amri zake zinashuka baina yao, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza
juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kukijua
vilivyo kwa ilimu yake.