Enyi mlio amini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye
kwa kelele kama mnavyo semezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu
vikaharibika, na hali hamtambui.
Kwa hakika wanao teremsha sauti zao mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, hao ndio
Mwenyezi Mungu amezisafisha nyoyo zao kwa uchamngu. Hao watakuwa na maghfira na
ujira mkubwa.
Na jueni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko nanyi. Lau angeli kut'iini katika
mambo mengi, bila ya shaka mngeli taabika. Lakini Mwenyezi Mungu amekupendezeeni
Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na amekufanyeni muuchukie ukafiri, na
upotovu, na uasi. Hao ndio walio ongoka,
Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa
moja la hao linamdhulumu mwenzie, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee
kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirudi basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na
hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki.
Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau
wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima,
wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha
amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu.
Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi.
Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi
anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni
Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na
tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu
zaidi kati yenu kwa Mwenyezi Mungu ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye khabari.
Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani
Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake,
hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
Hakika Waumini ni wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake tena wasitie
shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na
nafsi zao. Hao ndio wakweli.
Wanakusimbulia kuwa wamesilimu! Sema: Msinisimbulie kwa kusilimu kwenu. Bali
Mwenyezi Mungu ndiye aliye kufanyieni hisani kwa kukuongoeni kwenye Imani, ikiwa
nyinyi ni wakweli.