Yeye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akakaa vyema juu
ya enzi. Anayajua yanayo ingia katika ardhi na yanayo toka humo, na yanayo
teremka kutoka mbinguni, na yanayo panda humo. Naye yu pamoja nanyi popote
mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayo yatenda.
Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyo kufanyeni nyinyi
kuwa ni waangalizi wake. Basi walio amini miongoni mwenu, na wakatoa, wana
malipo makubwa.
Na mna nini hata hamumuamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anakuiteni mumuamini
Mola wenu Mlezi? Naye amekwisha chukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini.
Yeye ndiye anaye mteremshia mja wake Aya zinazo bainisha wazi ili akutoeni
gizani muingie kwenye nuru. Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni Mpole, Mwenye
kurehemu.
Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu
na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni mwenu wenye kutoa kabla ya
Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao walio
toa baadae na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidia wema. Na
Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Siku utakapo waona Waumini wanaume na Waumini wanawake, nuru yao iko mbele yao,
na kuliani kwao: Furaha yenu leo - Bustani zipitazo mito kati yake mtakaa humo
milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
Siku wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake watapo waambia walio amini:
Tungojeni ili tupate mwangaza katika nuru yenu. Waambiwe: Rejeeni nyuma yenu
mkaitafute nuru! Utiwe baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na
nje upande wake wa mbele kuna adhabu.
Watawaita wawaambie: Kwani vile hatukuwa pamoja nanyi? Watawaambia: Ndiyo,
lakini mlijifitini wenyewe, na mkasitasita, na mkatia shaka, na matamanio ya
nafsi zenu yakakudanganyeni. mpaka ilipo kuja amri ya Mwenyezi Mungu, na
mdanganyifu akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu.
Je! Wakati haujafika bado kwa walio amini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka
Mwenyezi Mungu na haki iliyo teremka? Wala wasiwe kama walio pewa Kitabu kabla
yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi wao wakawa
wapotovu.
Kwa hakika wanaume wanao toa sadaka, na wanawake wanao toa sadaka, na
wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, watazidishiwa mardufu na watapata
malipo ya ukarimu.
Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio Masidiqi na Mashahidi
mbele ya Mola wao Mlezi. Wao watapata malipo yao na nuru yao. Na walio kufuru na
wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio watu wa Motoni.
Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na
kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake
ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona
yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira
kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni
starehe ya udanganyifu.
Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni kama upana
wa mbingu na ardhi, iliyo wekewa walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake.
Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye fadhila kuu.
Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu
pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye
nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anaye mnusuru Yeye
na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye
kushinda.
Na bila ya shaka tulimtuma Nuhu na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao
Unabii na Kitabu. Basi wapo miongoni mwao walio ongoka, na wengi katika wao ni
wapotovu.
Tena tukafuatisha nyuma yao Mitume wengine, na tukamfuatisha Isa bin Mariamu, na
tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za walio mfuata upole na rehema. Na
umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta
radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyo takiwa kuufuata. Basi wale
walio amini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni wapotovu.
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atakupeni
sehemu mbili katika rehema yake, na atakujaalieni muwe na nuru ya kwenda nayo.
Na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uweza wowote juu ya fadhila za
Mwenyezi Mungu. Na fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa
amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.