Je! Mwawaona wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba
nini katika ardhi; au hao wanayo shirika katika mbingu? Nileteeni Kitabu kilicho
kuwa kabla ya hiki, au alama yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
Au wanasema: Ameizua mwenyewe! Sema: Ikiwa nimeizua mimi, basi nyinyi hamwezi
kunifaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Yeye anajua zaidi hayo mnayo ropokwa;
anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi. Na Yeye ndiye Mwenye kusamehe,
Mwenye kurehemu.
Sema: Mimi si kiroja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyo fanywa wala
nyinyi. Mimi nafuata niliyo funuliwa tu kwa Wahyi, wala mimi si chochote ila ni
mwonyaji mwenye kudhihirisha wazi.
Sema: Mwaonaje yakiwa haya ni kweli yametoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi
mmeyakataa, na akashuhudia shahidi miongoni mwa Wana wa Israili juu ya mfano wa
haya, na akaamini, na nyinyi mnafanya kiburi? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi
watu wenye kudhulumu.
Na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa, kuwa chenye uwongozi na rehema. Na
hichi ni Kitabu cha kusadikisha na kilicho kuja kwa lugha ya Kiarabu, ili
kiwaonye walio dhulumu, na kiwe ni bishara kwa watendao mema.
Na tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua
mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata
kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na
akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema
zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na
unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa
Waislamu.
Hao ndio tunao wapokelea bora ya vitendo vyao walivyo vitenda, na tunayasamehe
makosa yao. Watakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Miadi ya kweli hiyo walio
ahidiwa.
Na ambaye amewafyonya wazazi wake na akawaambia: Ati ndio mnanitisha kuwa
nitafufuliwa, na hali vizazi vingi vimekwisha pita kabla yangu! Na hao wazazi
humwomba msaada Mwenyezi Mungu (na humwambia mtoto wao): Ole wako! Amini! Hakika
ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na yeye husema: Hayakuwa haya ila ni visa vya
watu wa kale.
Hao ndio ambao imehakikikishwa hukumu juu yao kama mataifa yaliyo kwisha pita
kabla yao miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa wenye kukhasiri.
Na siku watakapo letwa walio kufuru kwenye Moto wataambiwa: Nyinyi mlitwaa vitu
vyenu vizuri katika uhai wa duniani, na mkastareheshwa navyo. Basi leo ndio
mnalipwa adhabu ya fedheha kwa mlivyo kuwa mkitakabari katika ardhi bila ya
haki, na kwa sababu mlikuwa mkifanya upotovu.
Na mtaje ndugu wa kina A'di, alipo waonya watu wake kwenye vilima vya mchanga.
Na kwa yakini waonyaji wengi walitokea kabla yake na baada yake kuwaambia:
Msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nakukhofieni isikupateni
adhabu ya siku iliyo kuu.
Basi walipo liona wingu likielekea kwenye mabonde yao, walisema: Wingu hili la
kutunyeshea mvua! Kumbe sivyo, haya ni hayo mliyo yahimiza, upepo ambao ndani
yake imo adhabu chungu!
Na bila ya shaka tuliwaweka vizuri sio kama tulivyo kuwekeni nyinyi; na tuliwapa
masikio, na macho, na nyoyo. Na hayakuwafaa kitu masikio yao, wala macho yao,
wala nyoyo zao kwa lolote. Kwani hao walikuwa wakizikataa Ishara za Mwenyezi
Mungu, na yale waliyo kuwa wakiyafanyia maskhara ndiyo yakawazunguka.
Basi mbona wale walio washika badala ya Mwenyezi Mungu, kuwa ati hao ndio
wawakurubishe, hawakuwanusuru? Bali waliwapotea! Na huo ndio uwongo walio kuwa
wakiuzua.
Na wakati tulipo waleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza Qur'ani. Basi
walipo ihudhuria walisema: Sikilizeni! Na ilipo kwisha somwa, walirudi kwa kaumu
yao kwenda kuwaonya.
Wakasema: Enyi kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho teremshwa baada ya
Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho ongoza kwenye Haki na
kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Na wasio mwitikia Mwitaji wa Mwenyezi Mungu basi hao hawatashinda katika ardhi,
wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio dhaahiri.
Je! Hawaoni ya kwamba Mwenyezi Mungu, aliye ziumba mbingu na ardhi, na hakuchoka
kwa kuziumba, kuwa ni Muweza wa kuwafufua wafu? Kwani? Hakika Yeye ni Muweza wa
kila kitu.
Na siku watakapo letwa makafiri Motoni wakaambiwa: Je! Haya si kweli? Watasema:
Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu Mlezi, ni kweli! Atasema: Basi onjeni adhabu kwa
sababu ya kule kukataa kwenu.
Basi subiri, kama walivyo subiri Mitume wenye stahmala kubwa, wala usiwafanyie
haraka. Siku watakayo yaona waliyo ahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa
ulimwenguni ila saa moja ya mchana. Huu ndio ufikisho! Kwani huangamizwa wengine
isipo kuwa walio waovu tu?