Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake.
Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya
mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni
wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye
anaye sema kweli, naye ndiye anaye ongoa Njia.
Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na
ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si
lawama juu yenu kwa mlivyo kosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya
nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na
jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini
wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha
andikwa Kitabuni.
Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilio juu yenu. Pale yalipo
kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyo yaona. Na
Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipo kodoka, na
nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.
Na kundi moja katika miongoni mwao lilipo sema: Enyi watu wa Yathrib! Hapana
kukaa nyinyi! Rudini. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume
kwa kusema: Hakika nyumba zetu ni tupu. Wala hazikuwa tupu; hawakutaka ila
kukimbia tu.
Sema: Ni nani wa kukulindeni na Mwenyezi Mungu pindi akikutakieni uovu, au
akikutakieni rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi
Mungu.
Wana choyo juu yenu. Ikifika khofu utawaona wanakutazama na macho yao
yanazunguka, kama yule ambaye aliye zimia kwa kukaribia mauti. Na khofu
ikiondoka wanakuudhini kwa ndimi kali, nao ni mabakhili kwa kila la kheri. Hao
hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibat'ilisha vitendo vyao. Na hayo kwa
Mwenyezi Mungu ni mepesi.
Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi
watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza khabari zenu.
Na lau wakiwa pamoja nanyi hawapigani ila kidogo tu.
Na Waumini walipo yaona makundi, walisema: Haya ndiyo aliyo tuahidi Mwenyezi
Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli. Na hayo
hayakuwazidisha ila Imani na ut'iifu.
Miongoni mwa Waumini wapo watu walio timiza waliyo ahidiana na Mwenyezi Mungu.
Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi)
hata kidogo.
Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na awaadhibu
wanaafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu yao; hawakupata
kheri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika vita. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu na uweza.
Na akawateremsha wale walio wasaidia (maadui) katika Watu wa Kitabu kutoka
katika ngome zao; na akatia khofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawauwa,
na wengine mnawateka.
Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha
Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake.
Na semeni maneno mema.
Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya
kizamani. Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume
wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya
Mtume, na kukusafisheni baarabara.
Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini
wanawake, na wat'iifu wanaume na wat'iifu wanawake, na wasemao kweli wanaume na
wanawake, na wanao subiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na
wanawake, na watoao sadaka wanaume na wanawake, na wanao funga wanaume na
wanawake, na wanao jihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanao mdhukuru
Mwenyezi Mungu kwa wingi wanaume na wanawake, Mwenyezi Mungu amewaandalia
msamaha na ujira mkubwa.
Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo,
Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye
kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.
Na ulipo mwambia yule Mwenyezi Mungu aliye mneemesha, nawe ukamneemesha:
Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyo taka
Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye
mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipo kwisha haja naye tulikuoza wewe,
ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapo kuwa
wamekwisha timiza nao shuruti za t'alaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye
kutekelezwa.
Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyo mhalalishia Mwenyezi Mungu. Huo ndio mwendo
wa Mwenyezi Mungu kwa walio pita zamani. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni kudura
iliyo kwisha kadiriwa.
(Hao wa zamani) walio kuwa wakifikisha risala za Mwenyezi Mungu na wanamwogopa
Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu
ndiye atoshaye kuhisabu.
Enyi mlio amini! Mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa t'alaka kabla ya
kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayo ihisabu. Basi wapeni cha kuwaliwaza, na
muwawache kwa kuwachana kwa wema.
Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako ulio wapa mahari yao, na ulio wamiliki kwa
mkono wako wa kulia katika alio kupa Mwenyezi Mungu, na mabinti ami zako, na
mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama
yako walio hama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii,
kama mwenyewe Nabii akitaka kumwoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini
wengine. Sisi tunajua tuliyo wafaridhia wao katika wake zao na wanawake ilio
wamiliki mikono yao ya kulia. Ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kusamehe, Mwenye kurehemu.
Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze umtakaye. Na kama
ukimtaka yule uliye mtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya hivi kutapelekea
yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile unacho wapa
wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu, na Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kujua, Mwenye hikima.
Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha kwa wake
wengine ingawa uzuri wao ukikupendeza; isipo kuwa yule uliye mmiliki kwa mkono
wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachungua kila kitu.
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba za Nabii ila mpewe ruhusa kwenda kula, sio
kungojea kiwive. Lakini mtakapo itwa basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni,
wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii naye anakustahini, lakini
Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapo wauliza wakeze haja waulizeni
nyuma ya mapazia. Hivyo ndio usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala
haikufalieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake
kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Hapana ubaya kwao (wake za Mtume) kuonana na baba zao, wala watoto wao, wala
ndugu zao, wala watoto wa ndugu zao wanaume, wala watoto wa ndugu zao wanawake,
wala wanawake wenzao, wala wale iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Na enyi
wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila
kitu.
Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie
nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Kama wanaafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitna katika
Madina hawatoacha, basi kwa yakini tutakusalitisha juu yao, kisha hawatakaa humo
karibu yako ila muda mchache tu.
Enyi mlio amini! Msiwe kama wale walio mtaabisha Musa, lakini Mwenyezi Mungu
akamtakasa na waliyo yasema, naye alikuwa mwenye hishima mbele ya Mwenyezi
Mungu.
Apate kukutengenezeeni vitendo vyenu na akusameheni madhambi yenu. Na anaye
mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa.
Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima; na vyote
hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanaadamu akaichukua. Hakika
yeye amekuwa dhaalimu mjinga.
Kwa hivyo Mwenyezi Mungu anawaadhibu wanaafiki wanaume, na wanaafiki wanawake,
na washirikina wanaume, na washirikina wanawake; na anawapokelea toba Waumini
wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye
kurehemu.